Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wanawake na Makundi maalum Dk.Doroth Gwajima amesema Wizara hiyo tayari imetekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan, alilolitoa jijini Dodoma Septemba 2021 kuhusu kuandaa mkakati kwa mashirika yasiyo ya kiserikali kupunguza utegemezi katika kutekeleza majukumu yao.
Akizungumza leo Mei 9,2022 wakati akifungua kikao cha wadau wa mashirika yasiyo ya kiserikali kwa kanda ya Mashariki kilicholenga kutoa maoni ya wadau hao katika kuweka mikakati ya kujisimamia na kupunguza utegemezi wa fedha za wafadhili Dk.Gwajima amesema Wizara hiyo imeshachukua hatua kadhaa kutekeleza maagizo ya Rais.
Waziri Dkt Gwajima amesema mashirika hayo yamekuwa yakichagiza jitihada za Serikali kuwaletea Wananchi wake maendeleo kupitia utekelezaji wa miradi ya afua mbalimbali zikiwemo za Afya, Kilimo, Elimu, Maji, Mazingira, Miundombinu, Utawala Bora, Nishati, hifadhi wa Jamii, Mifugo na Uvuvi, Uwezeshaji wa Jamii na Sekta nyingine mtambuka.
"Miradi hiyo, sio tu imewanufaisha Wananchi wetu kijamii, bali pia imechangia katika kuongeza ukuaji wa uchumi, kuboresha utoaji wa huduma na kuongeza fursa za ajira hususan kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu" amesema.
Ameongeza Wizara inashirikiana na wadau wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuandaa Mpango Mkakati wa kuyajengea uwezo Mashirika hayo ili kupunguza utegemezi na kuwa na uendelevu wa shughuli zao na utaratibu huo wa kukusanya maoni kutoka katika Mashirika hayo unafanyika katika Kanda tano ikiwemo Kanda ya Mashariki Kanda ya Kati, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa.
Amesisitiza Wizara ilianza mchakato kwa kuandaa Mkakati huo, tarehe 10 Novemba, 2021, ambapo iliunda Kamati ya wajumbe 20 ikijumuisha wataalam kutoka Wizarani, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, sekta binafsi na Wadau wengine." alisisitiza Dkt Gwajima
Aidha Waziri Dkt. Gwajima amesema Kamati iliyoundwa mpaka sasa imefanikisha kukamilika kwa andiko la majadiliano (consultation paper), nyenzo za ukusanyaji wa taarifa na maoni kutoka kwa wadau mbalimbali (stakeholders engagement tools), pamoja na ukusanyaji wa taarifa na maoni kutoka kwa wadau.
Ametumia nafasi hiyo kutoa mwito kwa wadau wengine kuendelea kuiwezesha Kamati katika shughuli nyingine zinazofuata ili kukamilisha mkakati huu utakaosaidia kukidhi malengo ya kuanzishwa kwa Mashirika yenu na matarajio ya jamii ya Watanzania.
Ametoa shukrani zake za dhati kwa Laurence Wilkes kwa niaba ya FCDO ya Ubalozi wa Uingereza, kwa kuiwezesha Kamati kufanya mikutano hii ya kukusanya maoni katika Kanda zote tano zinazoendelea" alisema Dkt Gwajima
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la CBM International na Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha kuandaa Mkakati huo Nensia Mahenge alisema Kikosi hicho kinaendelea kukusanya maoni kwa ajili ya ya kutengeneza Mpango Mkakati kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yaliyopo nchini kuweka mikakati ya kujitegemea na kuwa na uendelevu katika utekelezaji wa majukumu na miradi mbalimbali kwa wananchi.
"Kwa kuanzia Kikosi kazi chetu kilifanikiwa kukusanya maoni katika Kanda ya Ziwa iliyohusisha Mikoa ya Kigoma, Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara na baada ya mkutano huu Kamati itaendelea na kukusanya maoni katika Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Nyanda za Juu na kumalizia Kanda ya Kati", alisema Nensia.
Wakati huo huo Laurence Wilkes akizungumza kwa niaba ya FCDO ya Ubalozi wa Uingereza amesema Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ni wadau muhimu katika maendeleo ya Taifa kwani yakishirikiana na Serikali kwa ukaribu itasaidia kuendelea kutoa huduma zilizo na uhakika na muendelezo kwa wananchi.
Home
HABARI
DK.GWAJIMA ASEMA WIZARA YAO IMETEKELEZA MAAGIZO YA RAIS SAMIA KUHUSU KUANDAA MKAKATI MASHIRIKA KUPUNGUZA UTEGEMEZI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...