· Waridhishwa na Mradi wa ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama

· Wapewa picha ya hali ya uboreshaji huduma za Mahakama

Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imetembelea Mradi wa Ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma ambapo imeonyesha kuridhishwa na Mradi huo na kuipongeza Mahakama kwa uboreshaji wa miundombinu ya majengo yake.

Akizungumza leo tarehe 24 Mei, 2022 mara baada ya ukaguzi wa Mradi huo unaojengwa katika eneo la ‘NCC Link’ mkoani Dodoma, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Daniel Sillo (MB) amesema kuwa Mahakama imepiga hatua kubwa katika uboreshaji wa huduma kwa lengo la kuwafikia wananchi.

“Kwanza nichukue fursa hii kwa niaba ya Kamati yetu ya Bunge ya Bajeti kumpongeza sana Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia uboreshaji wa Mahakama hapa nchini, tumepita kwenye jengo la Kituo Jumuishi na vilevile tumekagua Mradi huu mkubwa ambao ni wa kihistoria kwa Afrika, na jengo ambalo linatajwa kuwa la sita kwa ukubwa (6) kati ya majengo ya Mahakama duniani, kwa kweli ni maboresho makubwa sana katika mustakabali wa kutoa haki,” amesema Mhe. Sillo.

Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa wao kama Kamati ya Bajeti wameridhishwa na matumizi ya fedha na mwenendo wa ujenzi wa Mradi huo na kusema kuwa ni wakati muafaka sasa kwa Wizara ya Katiba na Sheria kuendelea kuboresha taasisi nyingine zilizo chini ya mwamvuli wa Wizara hiyo ili waweze kwenda pamoja na kasi ya Mahakama.

Aidha, kabla ya kutembelea Mradi huo, Wajumbe hao walitembelea na kukagua jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Dodoma ambapo pamoja na ukaguzi walipata semina fupi iliyolenga kuwapa taswira ya hatua iliyofikiwa na Mahakama katika uboreshaji wa huduma zake.

Akizungumza wakati akiwasilisha Mada ya Utekelezaji wa Uboreshaji Huduma za Mahakama: Mafanikio na Changamoto, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amewajuza Wabunge hao kuwa safari ya uboreshaji wa huduma za Mahakama ni muhimu kwa kuwa umelenga katika kurahisisha upatikanaji wa huduma mahsusi ya Mahakama ya utoaji haki kwa wananchi.

Prof. Ole Gabriel amewahakikishia Wabunge hao kuwa Mahakama itaendelea kutunza rasilimali hizo ambazo Mahakama imeaminiwa na Serikali na kuahidi kuwa wataendelea kuwahudumia wananchi kwa weledi.

Wakichangia mada katika semina fupi iliyoandaliwa na Mahakama, Wajumbe wa Kamati hiyo akiwemo Makamo Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Omari Kigua (MB), Mhe. Dkt Charles Kimei (MB), Mhe. Shamsi Nahodha na wengine wameipongeza Mahakam ana kuiomba Wizara ya Katiba na Sheria kuboresha pia Taasisi nyingine zilizo chini ya mwamvuli ili ziweze kwenda sambamba na kasi ya uboreshaji wa huduma za Mahakama.

Naye, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Geophrey Pinda amesema kuwa Wizara inaendelea na jitihada za kuboresha Taasisi za Sheria zilizo chini yake ili kwenda na kasi ya Mahakama hatimaye wananchi waweze kupata huduma ya haki bila vikwazo vyovyote.

Mradi wa Ujenzi wa jengo la Makao makuu ya Mahakama ambao umefikia asilimia 58 ya ujenzi wake utagharimu fedha za kitanzania shilingi 129,740,285,556.02 na unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 29 Desemba, 2022.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akifafanua jambo kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakati Kamati hiyo ilipotembelea Mradi wa Ujenzi wa Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. Kamati hiyo imetembelea pia Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki mkoani humo leo tarehe 24 Mei, 2022.


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakiwa katika nyuso za furaha walipokuwa katika eneo linapojengwa jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, kulia ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel.


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakati walipotembelea jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Dodoma leo terehe 24 Mei, 2022. Mwenye suti ya 'dark blue' ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Daniel Sillo.


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakiwa katika chumba maalum kwa ajili ya Watoto wenye mashauri kilichopo ndani ya jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Dodoma.


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakifuatilia Mada ya Uboreshaji wa Huduma za Mahakama iliyotolewa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel leo tarehe 24 Mei, 2022 wakati Kamati hiyo ilipotembelea Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki -Dodoma.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Geophrey Pinda (wa pili kulia) pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakiwa katika jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Arusha wakati Kamati hiyo ilipokuwa ikikagua jengo hilo. Kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Daniel SilloKulia ni Mjumbe wa Kamati hiyo. Mhe. Ester Matiko (MB) pamoja na Wajumbe wengine.
Kikao kikiendelea.

Makamo Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Omari Kigua (MB) akizungumza katika kikao hicho.


Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mhe. Shamsi Nahodha akichangia jambo katika kikao hicho.
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mhe. Dkt. Charles Kimei akichangia jambo katika kikao hicho.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...