Na Janeth Bocco, Dodoma
TUME ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) wamejipanga kutatua changamoto zilizopo kwenye Sekta ya Ushirika kupitia tafiti zilizofanyika na uzoefu wa wadau mbalimbali kwa kupitia kongamano la pili la Tafifi za Ushirika la mwaka 2022

Kauli hiyo imetolewa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) Dkt. Benson O. Ndiege katika taarfa kwa vyombo vya Habari aloitoa ambapo amesema kuwa kongamano hilo linalenga kutoa fursa kwa watafiti pamoja na wadau wengine wa Sekta ya Ushirika kukutana na wanachama, viongozi na watendaji wa vyama vya Ushirika, ili kujadiliana matokeo ya utafiti na utatuzi wa changamoto mbalimbali.

Dkt. Ndiege amesema kuwa Kongamano la Pili la Tafiti za Ushirika limeandaliwa kwa kushirikisha Wadau mbalimbali ambapo litafanyika Jijini Dodoma kwa siku tatu kuanzia tarehe 11 – 13 Mei, 2022 kwenye ukumbi wa PSSSF.

“Mgeni Rasmi katika Ufunguzi wa Kongamano hili atakuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde na Tafiti mbalimbali zinazohusu Sekta ya Ushirika zimekuwa zikifanywa na wadau mbalimbali wakiwemo Vyuo vya Elimu ya Juu, Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali, Wadau wa Ushirika na wengine”, ameeleza Dkt. Ndiege

Ndiege ameongeza kuwa Tafiti hizo zimekuwa zikitoa mapendekezo ya utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazokabili maendeleo ya Ushirika nchini.

Hata hivyo, Dkt. Ndiege ameeleza kuwa walengwa wakubwa ambao ni wanachama, viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika wamekuwa hawapati fursa ya kupata matokeo ya tafiti hizo na mapendekezo yake.

Aidha, Dkt. Ndiege amesema Tafiti nyingi zimekuwa zikichapishwa kwenye Majarida ya Kitaaluma, Mitandao na mara nyingi kuandikwa kwa lugha ya kiingereza; lugha ambayo siyo rafiki kwa wanaushirika wengi; hivyo mapendekezo mengi yamekuwa hayafanyiwi kazi.

“Hivyo, tunawakaribisha washiriki wote katika Kongamano hili muhimu kwa Maendeleo ya Sekta ya Ushirika nchini, Ushirika – Pamoja Tujenge Uchumi”, amesisitiza Dkt. Ndiege.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...