Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
MWENYEKITI wa Kamati ya Ushauri ya Sensa, Dkt. John Jingu amesema kuwa maandalizi ya kukamilisha zoezi la Sensa kwa mwaka 2022 yanaenda vizuri na tayari yamefika asilimia 80% kwa maeneo yaliyotengwa sanjari na maandalizi ya vifaa vitakavyotumika katika zoezi hilo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati alipokutana na Wawakilishi wa Sekta Binafsi na Wafanyabiashara kuelekea katika zoezi hilo, Dkt. Jingu amesema licha ya maandalizi hayo kufika asilimia 80%, kazi ya kukamilisha na kufanikisha zoezi hilo kwa asilimia zote 100% inaendelea sehemu mbalimbali nchini bila kuchoka.

“Kuna hatua kadha wa kadha tayari tumekamilisha, mwaka jana tulifanya majaribio ya Sensa, na tunaendelea kufanya maandalizi, maeneo tayari yametengwa na vifaa vinaendelea kununuliwa na kazi kwa ujumla inaendelea vizuri, hatuwezi kupumzika hadi siku ya mwisho ya zoezi Agosti 23, 2022”, ameeleza.

“Najua mtajiuliza juu ya ushiriki wa Sekta Binafsi na Wafanyabiashara nchini katika zoezi hili, kwa hakika Sensa hii itawasaidia kupanga Soko lao na bidhaa zao wanazozalisha sehemu mbalimbali nchini, itawasaidia kujua idadi ya watu na rika ili watoe huduma zinazostahili kwa watu hao”, amesema Dkt. Jingu.

Dkt. Jingu amesema Wafanyabiashara na Sekta Binafsi wanapaswa kufanyia kazi wito wa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kukamilisha zoezi hilo kwa kusaidia kuweka Matangazo ya Nembo ya Sensa kwenye bidhaa mbalimbali kama inavyofanya Serikali kutangaza zoezi hilo na kuhamasisha nchi nzima kupitia masuala yake mbalimbali.

Akizungumza kwa niaba ya Sekta Binafsi, Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini, Paul Makanza amesema kupitia zoezi hilo la Sensa, Sekta binafsi itafaidika na takwimu hizo za idadi ya watu na makazi na kuzifanyia kazi ipasavyo hususani katika Sekta ya Biashara kulingana na uhusiano wa Sekta hiyo na idadi ya watu.

“Sisi Sekta Binafsi tunawapongeza sana kwa hatua mliofikia hadi sasa kuelekea kukamilisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi nchini, sisi tunaunga mkono zoezi hili la kupata takwimu za Watu na Makazi kwa nchi nzima”, amesema Makanza.

Sensa ya Watu na Makazi kwa mwaka 2022 itakuwa Sensa ya Sita tangu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964. Sensa nyingine ziliwahi kufanyika mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012, zoezi hilo linafanyika kila baada ya miaka 10.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Sensa ambaye pia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) Dkt. John Jingu akizungumza na Wawakilishi Sekta Binafsi, Wafanyabiashara na wadau wengine wa Sensa ya Watu na Makazi kuelekea zoezi hilo linalotarajaliwa kufanyika Agosti 23, 2022 nchini kote.
 Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Sensa, Dkt. John Jingu (wa mbele) akisikiliza maoni ya Wajumbe wa Sekta Binafsi na Wawakilishi wa Wafanyabiashara kuelekea zoezi la Sensa ambalo linatarajiwa kufanyika nchini Agosti 23, 2022, Wa kushoto ni Mwenyekiti mwenza kutoka Visiwani Zanzibar, Thabit Faina.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Sensa ambaye pia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) Dkt. John Jingu (wa kwanza upande wa kushoto) akitazama ripoti ya taarifa ya Sensa ya Watu na Makazi iliyoandaliwa mahsusi kuelekea zoezi linatorajiwa kufanyika nchini kote, Agosti 23, 2022.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...