NAIBU Waziri wa Madini, Dkt.Steven Kiruswa ameshuhudia utiaji saini mkataba mnono  kati ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Kampuni ya ABSA ambapo tani 60,000 zitauzwa kwa mwezi kwa wawekezaji hao kwa kipindi cha miaka mitano.

Hafla hiyo ya utiaji saini mkataba kati ya STAMICO na mwekezaji Kampuni ya ABSA ya nchini Uswiss imefanyika leo Mei 10, 2022 jijini Dodoma.

Dkt.Kiruswa amesema, STAMICO itakusanya mapato wastani wa shilingi bilioni 4.16 kwa mwezi sawa na wastani wa shilingi bilioni 50 kwa mwaka.

Pia, STAMICO itatoa ajira zisizo za moja kwa moja 600 na fursa nyingine za ajira kwa Watanzania katika mradi huo.

Amempongeza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt.Venance Mwasse na Menejimenti yake kwa kuwa wabunifu katika kutafuta masoko nje ya nchi. Aidha ameishukuru STAMICO kwa maamuzi ya kukubaliana na Kampuni ya ABSA katika kufanya biashara nchini.

"Ni matumaini yangu kuwa makubaliano haya yaliyosainiwa yatakuwa na manufaa kwa pande zote mbili,"amesema Dkt.Kiruswa.

Akizunguzia mafanikio ya STAMICO, Dkt.Kiruswa amesema, katika kipindi cha Julai, 2021 hadi Machi 2022, katika mradi wa Kabulo, tani 17,324 za makaa ya mawe zilichimbwa ambapo tani 12,792 zenye thamani ya shilingi 1.2 ziliuzwa na kulipa serikalini shilingi 174,191,290.87 ikiwa ni mrabaha na ada ya ukaguzi.

Dkt. Kiruswa amempongeza Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelelea kuifungua nchi ili wawekezaji waweze kuja kuwekeza Tanzania.

"Niwahakikishie wawekezaji wetu wa makaa ya mawe kuwa Tanzania ni nchi salama, inayojali wawekezaji na inayozingatia sheria mbalimbali za nchi na kimataifa. Wizara itahakikisha pia inafuatilia mwenendo mzima wa mkataba huu ili kupata matokeo chanya kwa Shirika na Kampuni ya ABSA," amesema.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse amesema, tukio hilo ni matokeo ya mkakati wa kuanza uchimbaji mkubwa wa makaa ya mawe. (mass coal mining

Amesema, maandalizi yamekamilika katika ukarabati wa miundombinu ya barabara, daraja na mgodi wa chini ambapo uchimbaji umeanza.

Dkt.Mwasse amesema, STAMICO imesaini mkataba mkubwa  wakihistoria ndani ambapo STAMICO itauza tani 60,000 kwa mwezi za makaa ya mawe.

"Mkataba huu ni wa kipindi cha miaka mitano, thamani ya mkataba huu ni dola za Marekani milioni 108 na zaidi, sawa na shilingi bilioni 250 za kitanzania kwa miaka mitano,"amesema Dkt.Mwasse.

Kwa upande wake Rais wa Kampuni ya ABSA, Bw.Gerges Schmickrath ameishukuru wizara kupitia STAMICO kwa kuaminiwa kuwekeza katika mradi wa makaa ya mawe. Amesema, mradi huo utakuwa na manufaa kwa watanzania kwa kuongeza pato la Taifa.

Hafla ya utiaji saini mkataba wa makaa ya mawe ya Mkoa wa Songwe katika mgodi wa Kabulo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Wizara ya Madini na Shirika la Madini la Taifa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...