KATIBU Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda Profesa Godius Kahyarara amesema Serikali itahakikisha inazungumza na wadau wa sekta ya utalii nchini ili kufufua hoteli za kitalii ambazo zimefungwa ikiwa ni sehemu ya kujiandaa na ujio wa Watalii baada ya filamu ya The Royal Tour kuzinduliwa.
Akijibu swali ambalo ameulizwa na waandishi wa habari wakati wa Mkutano wa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu jijini Dar es Salaam, Profesa Kahyarara amesema filamu ya The Royal Tour itachangia ongezeko la wafanyabiashara, wawekezaji na watalii, hivyo Serikali wanao wajibu kuweka mazingira rafiki.
Akielezea zaidi kuhusu mikakati ya Serikali, amesema pamoja na mambo mengine zipo hoteli za kitalii zilifungwa kutokana na changamoto mbalimbali, hivyo wanataka zifufuliwe ili kuanza kutoa huduma.
“Kuna Shirika la NSSF ambalo lina majengo mengi ambayo ndani yake yana hoteli za nyota tano, hivyo wote hawa tukikaa na kujadiliana tutapata muafaka, tunataka kuona hoteli hizo zinafanya kazi ili wageni wanapokuja kutalii wawe na sehemu ambazo watafikia,”amesisitiza.
Amefafanua kwamba filamu ya Royal Tour itawezesha Tanzania kupokea watalii milioni 5 ifikapo 2025, hali itakayochangia ukuaji wa uchumi na kuchochea maendeleo.
“Pamoja na mipango mingine ya Serikali, katika mkataba iliyosainiwa nchini Marekani tunaratajia kutakuwa na ndege itakayofanya safari za moja kwa moja kutoka Jiji la Dallas hadi Tanzania , hii itasaidia kufanya watalii wanaotoka Marekani kutopata shida ya usafiri wanapotaka kuja nchini,”amesema.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Amos Nnko ametumia mkutano huo kueleza kwamba wataendelea kushirikiana na sekta ya utalii kuhakikisha hakuna kikwazo kinachotokea pale kasi ya watalii wanaokuja nchini itakapoongezeka.
Amefafanua sekta hiyo imefanya marekebisho ya miundombinu katika sekta za utalii kupitia fedha za mkopo usio na riba wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Sh.trilioni 1.3.Ameongeza watashirikiana wadau wa utalii kupitia Shirikisho la Watoa Huduma za Utalii (TCT).
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Kamati ya Royal Tour ambaye pia ni Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk.Hassan Abbasi ameeleza filamu hiyo imeanza kuonesha matokeo chanya kwa nchini tangu kuzinduliwa kwake.
Aidha amesema filamu ya The Royal Tour imeoneshwa kwenye vituo vya televisheni zaidi ya 300 katika nchi ya Marekani pekee.Pia filamu hii inaonekana kwenye mitandao mingi.“Ukweli filamu ya The Royal Tour ina manufaa makubwa yakiwemo ya Rais Samia kukutana na wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa zaidi ya 40 wa sekta ya filamu na utalii.”
Akitoa maelezo ya jumla kuhusu ziara ya Rais Samia nchini Marekani na Uganda, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Zuhura Yunus amesema ziara hizo zimekuwwa na mazuri kwenye sekta zote.
“Matarajio yetu ziara hizi zitachangia ongezeko la ajira 300,000 kwa kada mbalimbali ikiwemo utalii, miundombinu, afya, elimu na nyingine nyingi,”amesema Yunus alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 12,2022 Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Zuhura Yunus akizungumza na Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali vya Habari kuhusu ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan nchini Uganda na Marekani kwenye Mkutano uliofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 12 Mei, 2022.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni, na Michezo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya The Royal Tour Mhe. Dkt. Hassan Abbas akizungumza na Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali vya Habari kuhusu ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan nchini Uganda na Marekani kwenye Mkutano uliofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Profesa Godius Kahyarara akizungumza jambo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula kabla ya kuzungumza na Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali vya Habari kuhusu ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan nchini Uganda na Marekani kwenye Mkutano uliofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam leo Mei,12 2022.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Profesa Godius Kahyarara akizungumza na Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali vya Habari kuhusu ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan nchini Uganda na Marekani kwenye Mkutano uliofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 12 Mei, 2022.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni, na Michezo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya The Royal Tour Mhe. Dkt. Hassan Abbas na Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Amos Nnko wakijiandaa kuzunguza na Waanindishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali vya Habari leo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...