Changamoto ya Miundombinu katika Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga huenda ikawa historia baada ya Wilaya hiyo kupata Bajeti ya Shilingi Bilioni 2.48/- zikiwemo fedha zinazotokana na tozo za Mafuta ya Petroli na Dizeli ili kutengeneza Miundombinu hiyo.
Akiwa ziarani Wilayani humo katika ukaguzi wa Miradi mbalimbali, Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amesema ameridhishwa na ujenzi wa Daraja la Soka Ipeja-Itilima linalounganisha wilaya za Kishapu na Itilima lilogharimu kiasi cha fedha Shilingi Milioni 486, huku akiwapongeza Mamlaka ya Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Kishapu kwa kazi nzuri ya ujenzi wa Daraja hilo.
“Nimewasiliana na Mhe. Rais Samia nikamwambia kuwa nipo Shinyanga, yeye akaniambia nije hapa Wilaya ya Kishapu kutokana na kuleta fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi mbalimbali, nimeridhika kuona fedha zimeelekezwa kwenye Mradi huu wa Daraja na Mradi unaenda kukamilika kwa asilimia 100%”, Chongolo amesema
“Sio mnapewa Bilioni Moja mnapeleka kwenye miradi 40, ambayo haikamiliki, hizo zama zimepita tunataka fedha zielekezwe kwenye mradi unaokwenda kukamilika kwa asilimia 100”, ameeleza
Akitoa taarifa ya Ujenzi wa Daraja hilo, Meneja wa TARURA, Wilaya ya Kishapu, Mhandisi Willfred Gutta amesema Miradi ya Barabara katika Wilaya hiyo inatekelezwa kwa jumla ya fedha Tsh. Bilioni 2.48/-.
Mhandisi Gutta amesema, “Shilingi Milioni 100/- ni fedha za Usimamizi wa Miradi, Shilingi Bilioni 1/- ni fedha zitokanazo na tozo ya Mafuta ya Petroli na Dizeli, Shilingi Milioni 500/- ni fedha za Mfuko wa Jimbo na Shilingi Milioni 987/- ni fedha za matengenezo ya kawaida ya Barabara”.
Amesema katika utekelezaji wa Bajeti hiyo, TARURA wameingia mikataba Tisa ya matengenezo ya Barabara hizo katika Wilaya ya Kishapu na Kata zake Tisa, huku akitoa taarifa ya kukamilisha Miradi mitatu kwa asilimia 100% ikiwemo Daraja hilo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kishapu, Mhe. Boniface Butondo amesema wanaendelea kushirikiana kusimamia vizuri Miradi mbalimbali Wilayani humo ili kuendana sawa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Wananchi waone matokeo ya Kodi zao wanazotoa.
“Daraja hili linalokamilika sasa, tangu kupatikana Uhuru wa Tanzania, Wilaya ya Kishapu ilikuwa na changamoto kubwa hususani katika Kata zake zinazounganishwa na kutoa huduma mbalimbali na Manispaa ya Shinyanga”, amesema Mhe. Butondo.
Pia amesema Daraja hilo litakuwa mkombozi kwa Wakazi hao wa Wilaya ya Kishapu ikiwemo kutoa huduma bora kwa Wakina Mama Wajawazito waliokuwa wanapoteza maisha wakati wanaenda kupata matibabu na kujifungua, huku akimpongeza Rais wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kutoa fedha hizo na kuondoa adha ya Miundombinu ya Barabara Wilayani humo.
Muonekano wa daraja la mto Soka linalounganisha wilaya za Kishapu na Itilima mkoani Shinyanga.
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM Ndugu Daniel Chongolo akimsikiliza Mbunge wa Jimbo la Kishapu Mh. Boniface Butondo alipokuwa akizungumza na Wananchi wa Jimbo lake mara baada ya ukaguzi wa daraja kufanyika. PICHA NA MICHUZI JR-MMG.
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM Ndugu Daniel Chongolo akisalimiana na mbunge wa Jimbo la Kishapu Mh Boniface Butondo wakati alipowasili kukagua ujenzi wa daraja la mto Soka Ipaja -Itilima ambalo limekamilika likigharimu zaidi ya shilingi milioni 500 katikati ni Joseph Mkude Mkuu wa wilaya ya Kishapu.
Katibu Mkuu wa Chama cha Maoinduzi CCM Ndugu Daniel Chongolo akislimiana na Kada was CCM Ndugu Suleiman Nchambis wakati alipowasili kukagua ujenzi wa Daraja la mto Soka Ipaja -Itilima ambalo limekamilika likigharimu zaidi ya shilingi milioni 500.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Kishapu Mhandisi Willfred Gutta akisoma Taarifa ya ujenzi wa Daraja la Soka Ipeja-Itilima linalounganisha wilaya za Kishapu na Itilima wakati Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Ndugu Daniel Chongolo alipomaliza kukagua ujenzi wa daraja hilo leo Mei 30,2022,. Daraja hilo ambalo limejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 486.4 ambapo fedha zilizokuwa zimetengwa hadi kukamilisha kwa ujenzi huo ni shilingi 500.Daraja tayari limekamilika.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...