*Changamoto za Watoa Huduma Zatafutiwa Mwarobaini
Na Mwandishi Wetu
Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imeweka bayana dhamira yake kuboresha
sekta ya mawasiliano nchini kwa kuhakikisha watoa huduma za mawasiliano
wanazingatia kutoa huduma za mawasiliano zenye ubora na ufanisi.
Hayo
yalibainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt Jabiri Bakari katika kikao
kazi na wadau wa sekta ya mawasiliano Kanda ya Ziwa kufanya kupokea
hoja mbalimbali na maoni ili kuboresha sekta ya mawasiliano nchini.
Kikao
kazi hicho kilihusisha watoa huduma za utangazaji kwa njia ya redio,
televisheni na mitandao, televisheni za kebo, watoa huduma za
mawasiliano ya simu, wamiliki wa kampuni za usafirishaji wa vifurushi na
vipeto, watoa huduma za intaneti pamoja na umoja wa mafundi simu kanda
ya ziwa na kufanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza
kikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
Dkt. Jabiri Bakari akiambatana na Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa Mhandisi
Francis Mihayo na Meneja wa Sehemu ya Masuala ya Wateja TCRA Bw.
Thadayo Ringo.
Akitoa
ufafanuzi kuhusu usalama mtandaoni, Mkurugenzi Mkuu Jabiri alisisitiza
kuwa, TCRA kwa kushirikiana na wadau wengine wa usalama mtandaoni
itaendelea kuhakikisha inatoa ushirikiano stahiki kwa Vyombo
vinavyolinda usalama wa watumiaji huduma za mawasiliano nchini, ili
watumiaji wajisikie huru kutumia huduma hizo pasipo wasiwasi wa usalama
wao wakati wote wanapokuwa kwenye mazingira ya mtandaoni.
“Mbinu
za wahalifu pia zimebadilika, kutoka kwenye kutenda uhalifu katika
mazingira ya kawaida, sasa wahalifu wamehamia mtandaoni; kwa hiyo jinsi
inavyoendelea na sisi lazima tuendelee na kujiongeza.tulitoa maelekezo
watoa huduma za mawasiliano ya simu lazima wawasiliane na wateja wao kwa
kutumia namba 100 kwa hiyo ukipata taarifa ya simu namba nyingine na
ukakubaliana maana yake kuna tatizo” alisisitiza Jabiri na kuongeza kuwa
TCRA inashirikiana na Jeshi la Polisi kuhakikisha mazingira ya
mawasiliano kwenye mtandao yanaendelea kusalia salama kwa kila mtumiaji
wa huduma za mawasiliano.
“Wahalifu
wanavyobadilika na sisi tunabadilika; kwa hiyo niseme tuna kazi kwenye
hilo eneo, huu ni uhalifu kama uhalifu mwingine kwa hiyo taarifa za
uhalifu kwenye mtandao zinapaswa kwenda kwenye Kituo cha Polisi; Polisi
wana Kitengo cha kushughulikia uhalifu mtandaoni, nasi tumeendelea
kushirikiana nao, ili kushughulikia na kudhibiti uhalifu wa aina hii
kama wanavyoshughulikia uhalifu wa namna nyingine” alisisitiza Jabiri
akijibu baadhi ya hoja za washiriki wa kikao hicho waliotaka kupata
ufafanuzi wa namna Mamlaka hiyo inavyodhibiti uhalifu mtandaoni.
Kuhusu
faragha ya taarifa za mtumiaji wa huduma za mtandao, Mkurugenzi Mkuu
Dkt.Jabiri alibainisha kuwa, usalama wa taarifa za mtumiaji wa huduma za
mtandao unalindwa kwa mujibu wa Sheria ya Makosa Mtandaoni, hata hivyo
mchakato wa sheria kamili itakayolinda faragha za mtumiaji wa huduma za
mawasiliano unaendelea na Matarajio na kwa sheria hiyo kuanza kutumika
hivi karibuni, alisisitiza Jabiri na kuongeza; “Watoa huduma ambao
wanabeba taarifa za watu (personal data), wanawajibika kwa namna moja au
nyingine kuhakikisha kwamba faragha ya mtumiaji wa huduma zao
inalindwa, wakati hii sheria haijafika, sheria ya Uhalifu Mtandaoni
haijawaacha pia; na ndiyo maana falsafa tuliyonayo hivi sasa ni
kuhakikisha tunaongeza jitihada za Ufuatiliaji kwa watoa huduma wetu
wote” alisisitiza Jabiri.
Aidha,
Jabiri aliwaeleza wadau hao kuwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
inaandaa kituo cha taarifa cha kimtandao ‘portal’ kiitwacho Tanzanite
mahali ambapo watoa huduma za mawasiliano na wadau watapata taarifa
mbalimbali zinazohusu sekta ya mawasiliano.
“Ninyi
watoa huduma ndiyo wateja wetu, lakini na ninyi watoa huduma mnao
wateja mnaowahudumia, kwa hiyo tumeboresha huduma kwa kuweka mazingira
wezeshi; tumeweka fursa ambayo sasa unaweza kupata fursa ya kujadiliana
masuala ya sekta na wahandisi, wanasheria, na wachumi wakakushauri zaidi
jinsi ya kuboresha na kupanua huduma unazotoa na kuongeza tija ili
kuwahudumia wananchi katika sekta pana ya mawasiliano. Tumeboresha
dawati hili la huduma kwa mteja lipo ofisi za Makao makuu na
tutalifikisha kwenye ofisi zetu za kanda” alibainisha Jabiri.
Katika
kikao-kazi hicho TCRA imepokea hoja katika masuala ya Leseni za
Mawasiliano, usafirishaji vifurushi na vipeto, masuala ya vifurushi vya
mawasiliano ya simu, huduma za utangazaji na posta na kuahidi kuyafanyia
kazi mapendekezo ya wadau wa sekta kama yalivyopokelewa kutoka kanda ya
ziwa; ambapo Mkurugenzi Mkuu Jabiri alisisitiza kuwa lengo la kikao
hicho kama ilivyo kwa vikao vingine ni kuboresha sekta ya mawasiliano
Tanzania.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabiri
Bakari akiongoza kikao-kazi na watoa huduma za Mawasiliano katika Kanda
ya Ziwa, kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Mwanza tarehe 24 Mei, 2022 kujadili utendaji kazi na kusikiliza
changamoto zinazoikabili sekta ya mawasiliano katika kanda ya ziwa ili
kuzipatia ufumbuzi. Washiriki kutoka mikoa ya Mwanza, Kagera, Shinyanga,
Geita, Mara na Simiyu wameshiriki kikao hicho. Picha na TCRA.Baadhi ya watoa huduma za Mawasiliano katika Kanda ya Ziwa wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Dkt. Jabiri Bakari akiongoza kikao-kazi na watoa huduma katika kanda hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza tarehe 24 Mei, 2022, kujadili utendaji kazi na kusikiliza changamoto zinazoikabili sekta ya mawasiliano katika kanda ili kuzipatia ufumbuzi. Washiriki kutoka mikoa ya Mwanza, Kagera, Shinyanga, Geita, Mara na Simiyu wameshiriki kikao hicho. Picha na TCRAWatoa huduma za mawasiliano katika Kanda ya Ziwa wakishiriki kikao kazi na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kilichoongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dkt. Jabiri Bakari na kufanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza tarehe 24 Mei, 2022. Kikao hicho kililenga kujadili utendaji kazi wa watoa huduma katika kanda hiyo ambapo TCRA ilisikiliza na kupokea changamoto zinazoikabili sekta ya mawasiliano katika kanda ili kuzipatia ufumbuzi. Washiriki kutoka mikoa ya Mwanza, Kagera, Shinyanga, Geita, Mara na Simiyu wameshiriki kikao hicho. Watoa Huduma za Utangazaji kwa njia ya Redio, Televisheni na Mitandao, Televisheni za Kebo, Watoa Huduma za Mawasiliano ya Simu, Wamiliki wa Kampuni za Usafirishaji wa Vifurushi na Vipeto, Watoa Huduma za Intaneti pamoja na Umoja wa Mafundi Simu Kanda ya Ziwa. Picha na TCRA
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...