Na Mwandishi wetu, Zanzibar Jumanne Mei 24,2022
Balozi
mdogo wa Jamhuri ya watu China aliyepo Zanzibar Bwana Zhang Zhisheng
amesema Jamhuri ya watu wa China itachukua kila juhudi kuhakikisha kuwa
uhusiano wa kihistoria baina ya nchi yake na Zanzibar katika sekta ya
habari unaendelea kuimarika kwa maslahi ya nchi hizo mbili na wananchi
wake.
Bwana Zhang
Zhisheng amesema hayo leo katika mazungumzo kati yake na uongozi wa
Idara ya Habari Maelezo Zanzibar yaliyofanyika katika ofisi za Idara ya
Habari Maelezo zilizopo Rahaleo mjini Unguja.
Amesema
mahusiano baina ya China na Zanzibar katika masuala ya habari yalianza
tokea mara tu baada ya Mapinduzi Zanzibar ya mwaka 1964, ambapo Jamhuri
ya watu wa China ilikuwa ikitoa filamu zenye maudhui ya kuwahamasisha
wananchi wa Zanzibar kufanyakazi kwa kujitegemea na kusahau kufanya kazi
walizokuwa wamezizowea kabla ya Mapinduzi yaliyowakomboa wanyonge.
Alisema
wakati huu ambapo China imepiga hatua kubwa katika maendeleo ya
kiuchumi, Zanzibar na Tanzania kwa jumla inayo nafasi ya kipekee
kujifunza mbinu na mikakati ambayo China imetumia hadi kufikia kuwa moja
kati ya mataifa yenye nguvu kiuchumi duniani.
Amesema
ameridhishwa na juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar ya awamu ya nane na Serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania katika kuimarisha sekta za kiuchumi na kijamii na kwamba
nchi yake imeshafanya mazungumzo na Serikali ya Zanzibar kuona namna
itakavyoshirikiana nayo katika sekta tofauti ikiwemo sekta ya Habari.
Naye
Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar Ndugu Hassan Khatib
Hassan ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa misaada yake
mbali mbali inayotoa katika kusaidia kuimarisha sekta ya Habari
Zanzibar
Amesema ni
Dhahiri kwamba wananchi wa Zanzibar wanayo mengi ya kujifunza kutoka
China kutokana na mafanikio makubwa ambayo nchi hiyo imeyapata na kwamba
vyombo vya habari vinaweza kuwa moja miongoni mwa njia muafaka
zitakazosaidia kufikisha elimu hiyo kwa umma.
Mkurugenzi
wa Habari Maelezo amesisitiza haja ya kuendelea kushirikiana katika
kubadilishana taarifa na namna ya kuzifikisha taarifa hizo katika ngazi
za chini, ambako wananchi wanayo mahitaji makubwa ya taarifa hizo.
Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Idara ya Habari Maelezo Bwana Yussuf Omar Chunda.
Imetolewa
Idara ya Habari Maelezo ZANZIBAR
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...