WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Kagera  uunde timu za kusimamia zao la kahawa kuanzia uoteshaji wa miche, kilimo chenyewe hadi mauzo ya zao hilo.

 

Akizungumza katika kikao cha wadau wa zao la kahawa alichokiongoza kwenye ukumbi wa ELCT mjini Bukoba leo mchana (Jumapili, Mei 15, 2022) Mheshimiwa Majaliwa amewataka viongozi wa Mkoa huo na wilaya  zake waandae vitalu vya miche ya kahawa na kuigawa kwa wananchi ikiwa na moja ya mbinu za kuwahamasha kulima zao hilo.

 

Amewataka viongozi na watendaji wa mkoa na wilaya kuishawishi sekta binafsi iwekeze kwenye vitalu vya miche ya kahawa ili kupata miche ya kutosha ya kuwauzia wananchi hatua ambayo itaisaidia kujipatia fedha na kutengeneza ajira.

 

Pia amewataka viongozi na watendaji wa Mkoa na wilaya wahakikishe kuwa Mfumo wa Stakabadhi za Mazao Ghalani unafanikiwa kwa kuwaelimisha wananchi faida kubwa watakazozipata kutokana na mfumo huo.

 

Amesema  ili kufanikisha mfumo huo, lazima viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Kagera (KCU) na kile cha Karagwe (KDCU) wabainishe maeneo itakapofanyika minada ya kahawa  na wahakiki na kutangaza hadharani  uwepo na wingi wa kahawa inayopigwa mnada.

 

“Hakuna mnunuzi  atakayeruhurusiwa kwenda majumbani au kwenye Chama cha Msingi kupatana bei au kununua kahawa. Kahawa yote inunuliwe kwenye maeneo ya mnada.”

 

Alisisitiza kwamba  wafanyabiashara lazima waratibiwe na wasipewe kabisa fursa  ya kujadili bei na viongozi wa vyama vya ushirika vya msingi au wananchi mashambani au majumbani kwani mipango yote ya bei na ununuzi wa kahawa inapaswa kufanyika mnadani.

 

Mheshimiwa Majaliwa ameagiza kuwa minada iwe wazi na maeneo ya inakofanyika yajulikane pia wakulima washirikishwe ili wajue bei ya mazao yao.

 

Mheshimiwa Majaliwa pia ameagiza kuwa wanachi washawishiwe kufungua akaunti benki ili malipo ya pesa zitakazotokana na mauzo ya kahawa yao yaingizwe kwenye akaunti hizo hatua ambayo itasaidia kuondoa hatari ya wakulima kuibiwa malipo yao.

 

Waziri Mkuu aliwasihi viongozi wa Serikali na wa ushirika wajiepushe na biashara ya ununuzi wa kahawa kwani endapo yatatokea mapungufu watawajibika.



Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika kikao cha Wadau wa zao la Kahawa alichokiongoza kwenye ukumbi wa ELCT mjini Bukoba, Mei 15, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi wa Mkoa wa Kagera wakati alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Bukoba  kuongoza Kikao cha Wadau wa  zao la Kahawa kwenye ukumbi wa ELCT mjini Bukoba, Mei 15, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


 

 

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...