Meneja Mtandao wa Safari na Usimamizi wa Mapato kutoka Air Tanzania Edward Nkwaki akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mdahalo huo na kueleza kuwa usafirishaji wa mizigo nje ya nchi umepamba moto na kuwataka wananchi kuchangamikia fursa katika sekta za kilimo, uvuvi na mifugo, Leo Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege la Precision Air Patrick Mwanri akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mdahalo huo na kueleza kuwa wapo sambamba na Serikali katika utoaji huduma utakaoleta manufaa kwa jamii na Taifa kwa ujumla, Leo jijini Dar es Salaam.
VIJANA wameshauriwa kutumia fursa kwa kusoma masomo ya kada za anga ili kuwa wataalam wa Taifa watakaopunguza changamoto ya wataalam wakiwemo marubani na wahandisi wa ndege.
Hayo yameelezwa leo na Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi wa Usafiri wa Anga kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Daniel Malanga wakati wa mdahalo maalum uliolenga kujadili 'Mchango wa Sekta ya Anga katika Ukuaji wa Uchumi wa Nchi' uliofanyika katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT,) na kueleza kuwa sekta ya anga inachochea ukuaji wa uchumi katika sekta nyingine ikiwemo utalii ambapo asilimia 70 ya watalii hutumia usafiri wa anga katika kufikia vivutio lukuki vilivyopo nchini.
''Pia sekta ya kilimo, uvuvi, biashara na madini inategemea sekta ya anga katika kukuza uchumi, fursa hizi lazima vijana wazitupie macho bila kuangalia dhana kuwa sekta ya anga ni kwa ajili ya watu fulani...Tunahitaji kuwa na marubani na wahandisi kutoka hapa nchini ili kuweza kuipeleka sekta hii mbele zaidi.'' Amesema.
Kuhusiana na changamoto ya marubani na wahandisi kwa kampuni binafsi za ndege Malanga amesema kuwa, changamoto hiyo ipo kwa baadhi ya kampuni za ndege na hutokana na gharama kubwa za mafunzo na uhaba wa vyuo vya kutoa mafunzo kwa wataalam hao na juhudi zinachukuliwa na Serikali chuo cha Taifa cha Usafirishaji ili kukabiliana na changamoto hiyo.
''Serikali imeendelea kuboresha eneo hilo kwa kuhakikisha kunakuwa na vyuo vya urubani na uhandisi hapa nchini ili kupunguza gharama za kuwasomesha wataalam hao nje ya nchi pamoja na kuwaajiri wataalam kutoka nje...Sekta hii ikiboreshwa na ikiwa na ushindani mzuri faida yake itahamia katika sekta nyingine za uchumi na kuboresha maisha ya watanzania kwa ujumla.'' Ameeleza.
Aidha amesema kuwa, Mamlaka hiyo inahamasisha wanafunzi vyuoni, sekondari na shule za msingi kutumia fursa ya kusoma masomo ya sekta ya usafiri wa anga kwa kuwapika wanafunzi hao ili taifa liwe na wataalam wa kutosha na kutengeneza kesho bora kwa Taifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la ndege la Precision Air Patrick Mwanri amesema, wamekuwa daraja la kuhakikisha uchumi wa Taifa unakuwa hasa katika sekta ya utalii tangu kuanza kwa shirika hilo miaka 29 iliyopita.
Mwanri amesema, katika kukabiliana na changamoto ya uhaba wa marubani na wahandisi shirika hilo lina karakana inayotengeneza ndege na wanashirikiana na chuo cha NIT na vijana wanaosoma masomo ya uhandisi hupata fursa ya kufanya mafunzo hapo baada ya kuhitimu masomo hayo na wamekuwa wakishirikiana na baadhi ya wataalam kutoka nje ili kubadilishana nao uzoefu.
Pia amesema, shirika hilo lina kituo cha mafunzo mbalimbali ikiwemo usalama wa anga na uhandisi na kuwataka vijana kutumia fursa hiyo kwa kujinoa zaidi kitaalam.
''Precision Air tupo kwa ajili ya watanzania na tunaunga mkono juhudi za Serikali inayopanua miundombinu na kuboresha viwanja vya ndege kwa kulipa kodi ili fedha hizo ziende kufanya kazi katika miundombinu ya ndege ili kupunguza gharama na wananchi waweze kunufaika kupitia anga kwa kusafiri pamoja na kusafirisha mizigo itokanayo na sekta za kilimo, madini, uvuvi na mifugo.'' Amesema.
Akieleza namna mtandao wa utoaji huduma za usafiri wa anga ulivyoenea nchini kote Meneja wa Mtandao wa Safari na Usimamizi wa Mapato kutoka Air Tanzania CO Ltd Edward Nkwaki amesema, mtandao wa huduma umepanuka nchini kote na marekebisho ya viwanja yanaendelea katika maeneo mbalimbali ikiwemo Musoma na kueleza kuwa usafiri wa anga unachangia katika uchumi kupitia biashara na utalii na kwa sasa usafirishaji wa mizigo nje ya nchi umechangamka na kuzidi kuipamba sekta hiyo.
''Shirika lina ndege 12 na limekuwa likichangia uchumi wa Taifa kwa sekta nyingine zaidi ikiwemo Utalii na kilimo ambapo sasa parachichi ya Tanzania inasafirishwa kuelekea India pamoja na bidhaa za baharini kupelekwa nchini China..... wakulima wachangamikie fursa hizi na kwa kupitia Royal Tour iliyozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan tutegemee mafanikio makubwa zaidi kiuchumi.'' Amesema.
Nkwaki amewataka vijana kuchangamikia fursa hizo pamoja na kuwa mabalozi bora kwa jamii kwa kuwaeleza namna watakavyonufaika na sekta ya usafiri wa anga.
Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi wa Usafiri wa Anga Daniel Malanga akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mdahalo huo na kuelezaa kuwa vijana watumie fursa za sekta hiyo kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla hasa kwa kutengeneza marubani na wahandisi wa kutosha, Leo jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa UVCCM tawi la NIT Riziki Mafungu akizungumza wakati wa mdahalo huo na kuwataka vijana kutumia fursa kwa kusoma fani za sekta ya anga ili kuleta tija kwa jamii na taifa kwa ujumla, Leo jijini Dar s Salaam.
Baadhi ya wanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT,) wakifuatilia na changia mada juu ya mdahalo huo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...