NA BALTAZAR MASHAKA,MWANZA

MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) umelipa sh. bilioni 1.19 kwa walengwa 7,208 wa Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa (PSSN II) katika Jiji la Mwanza ziwasaidie kupambana na masikini wa kipato kwa kuanzisha miradi midogo ya kiuchumi.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana,Amina Makilagi akizungumza amesema fedha za TASAF zimeleta mafanikio makubwa kwa walengwa wilayani humu baada ya kubuni na kuanzisha miradi ya uzalishaji mali ya kuwaongezea kipato na familia zao.

Amesema ili kujikwamua na umasikini walengwa wa mpango wa PSSN II jijini humu, kabla walielimishwa kuhusu matumizi sahihi ya fedha na kujengewa uwezo ambapo baadhi yao walianzisha vikundi vya kukopeshana, biashara ya chakula,samaki, kilimo na ufugaji.

“Fedha hizo zaidi ya sh. bilioni 1.19 zilitolewa kuanzia Februari 17,2020 hadi Mei 17,2022 kwa wanufaika 7,208 jijini humo na sasa tunafuatilia kufahamu fedha wanazopata kutokana na miradi hiyo wanazitumia vyema na kufanya shughuli ni endelevu," amesema Makilagi.

Mkuu huyo wa wilaya fedha hizo zimewasaidia walengwa kuongeza idadi ya watu kwenye shughuli au biashara za kuwapatia kipato cha siku na kuwasaidia kumudu gharama za maisha.

Mmoja wa Walengwa hao Chausiku Rubi Mwaka,mkazi wa Mtaa wa Mbugani 'A' jijini Mwanza,amesema anapokea sh.48, 000 kila baada ya miezi miwili kutoka TASAF,fedha ambazo zimemsaidia kuanzisha mradi wa kukaanga na kuuza samaki na faida anayopata inamwezesha kuhudumia familia yake ya watoto watatu ambapo mtaji wake umefikia sh.250, 000.

Mama huyo ambaye ni mjane baada ya kufiwa na mumewe mwaka 2025 kupitia biashara hiyo ya samaki baada ya kupewa fedha za TASAF alifanikiwa kumsomesha binti yake ambaye kwa sasa yuko Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare, kilichopo mjini Musoma.

Mlengwa mwingine Flora Lucas,mkazi wa Mtaa wa Mulungushi Tanesco,alisema fedha anazopokea kutoka TASAF sh. 50,000 amezitumia kuanzisha mgahawa wa kuuza chakula mradi ambao umekuwa mkombozi kwake na familia yake ya watoto wanne.

Amesema matarajio yake ni kuwa mjasirimali mkubwa,endapo TASAF wataendelea kumwezesha anatamani kujenga na kumiliki nyumba ya kuishi ili kuepuka adha ya kulipa kodi ya pango inayofikia sh.800,000 kwa mwezi.

Kwa upande wake, Ofisa Ufuatiliaji wa TASAF Jiji la Mwanza, Samson Kagwe amesema mpango huo utaendelea kutoa fedha kwa kaya za walengwa jijini humu zipatazo 7,208. Alieleza kuwa matarajio ya mpango ni kuona jamii inajikwamua kiuchumi kupitia fedha hizo, hawatarajii kuona wanufaika wakitumia fedha hizo kwa mambo yasiyo na tija,wabuni shughuli mbadala za kuwaongezea kipato na wanaamini wakizingatia masharti mpango utakuwa endelevu zaidi ya mwaka 2025.

 

Chausiku Rubi Mwaka, mkazi wa Mtaa wa Mbugani 'A' wilayani Nyamagana, mmoja wa walengwa wanaonufaika na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kupitia  Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa akikaanga samaki wa biashara ili kujiongezea kipato.   


Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) ofisini kwake leo kuhusu mafanikio ya Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa wanaowezeshwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...