Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa ametoa siku saba kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Amos Makalla kukutana na LATRA, Wadau na Wamiliki wa Mabasi kuweka uratibu mzuri wa kusimamia maelekezo ya Serikali kwa Mabasi yote kushusha na kupakia abiria ndani ya Kituo kikuu cha Mabasi cha Magufuli - Dar es salaam.

Bashungwa ametoa maelekezo hayo leo mei 30, 2022 wakati akikagua mradi wa Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli “Magufuli Bus Terminal” kilichopo wilaya ya Ubungo Dar es salaam, amesema Serikali imetumia kiasi cha shilingi bilioni 50 kujenga kituo hicho hivyo Serikali haitakubaliana na watu ambao hawazingatii utaratibu uliowekwa katika kituo hicho.

“Ninafahamu kuwa Mkuu wa Mkoa, Amos Makalla ameshapokea changamoto ya Mabasi kutoingia ndani ya kituo hiki cha Magufuli na mimi nimekuta changamoto bado iko pale pale, sasa kwa sababu ameshanza kulifanyia kazi nampa siku saba awe amekutana na LATRA pamoja na wadu wa mabasi (TABOA) kuangalia utaratibu wa mabasi yote kuingia ndani ya kituo kushusha na kupakia abiria” amesema Bashungwa.

Bashugwa ametoa siku kumi na nne kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ubungo, Kamati ya fedha na uongozi wa kituo cha Mabasi cha Magufuli kufanya mapitio na kupeleka mapendekezo ya changamoto ya Wapangaji katika kituo hicho ya kulalamikia kiwango kikubwa cha kodi ya pango ambapo wameeleza kwa sasa kiwango cha pango ni shilingi 40,000 kwa mita moja ya mraba.

Aidha, Ameagiza kuondolewa kwa Magari yote mabovu yaliyoegeshwa kwa muda mrefu ndani ya kituo hicho ambayo ni zaidi ya 40 yanayosababisha ufinyu wa eneo ili kutoa nafasi kwa magari mengine kupata maegesho ndani ya kituo.

Vile vile, Bashungwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya Ubungo, Kheri James kuweka utaratibu wa kukutana mara kwa mara na Wadau wa Kituo cha Magufuli, Mawakala na Makalani ili kusikiza na kuweka utaratibu wa kutatua changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza katika kituo hicho na kuzifanyia kazi kwa ushirikiano.

Wakati huo huo, amelekeza uongozi wa Wilaya Ubungo kuendelea kusimamia mpango uliopo kwenye ramani ya kituo hicho kwa kuweka kipaumbele cha kuboresha na kujenga miundombinu ya wafanyabiashara wadogo ili stendi hiyo iwe na manufaa kwa wanaanchi kulingana na Maelekezo ya Mheshimiwa Rais.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...