Na Joseph Lyimo
PAMOJA
na kuwa maambukizi ya virusi vya UVIKO-19 yaliwakumba baadhi ya watu na
wengine kupoteza maisha yao, bado kuna vijana wengi walichangamkia
fursa ya ugonjwa huo na kujinyanyua kiuchumi kwa kutengeneza barakoa na
vitakasa mikono.
Baadhi
ya vijana wa mkoa wa Manyara, walihamasika kuunda vikundi na kutengeneza
barakao hizo na kuziuza maeneo mbalimbali ikiwemo mahosipitalini,
kwenye nyumba za ibada, sokoni na minada na kwenye machimbo ya madini.
Serikali
kupitia Wizara ya Afya ilitoa tamko la kukubali matumizi ya barakoa
zilizotengenezwa nchini na siyo zilizotoka nje pekee ili mradi zikidhi
masharti yaliyotolewa ikiwemo mazingira ya usafi.
Mmoja
kati ya wakazi wa mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani
Manyara, Eva Mathayo ambaye alikuwa anajishughulisha na ufundi wa
cherehani anasema alitengeneza barakoa na kuwauzia watu mbalimbali ili
kujikinga na UVIKO-19.
“Watu
wengi walipenda bei zetu kwani barakoa moja tulikuwa tunauza shilingi
500 na tukapata soko zuri kwani walipenda huduma yetu,” anaeleza Eva.
Anasema
mafundi wengi waliingiza kipato kutokana na kushona barakoa kwa kutumia
vitambaa ili watu wajikinge na maambukizi ya UVIKO-19.
“Japokuwa
baadhi ya watu walikuwa wanadharau barakoa hizo tulizokuwa tunazishona
ila sijawahi kupata malalamiko hata kwa mtu mmoja kuwa amevaa barakoa
niliyoshona na akapata madhara ya UVIKO-19, mafua au kukohoa,” anaeleza
Eva.
Fundi wa kushona
nguo wa mji mdogo wa Kibaya Wilayani Kiteto, Khamis Ally anasema
alitengeneza barakao na wateja wake wengi walikuwa ni wajasiriamali wa
soko, wakulima na wafugaji mbalimbali waliokuwa wananunua kwa shilingi
500.
Fundi huyo
anaeleza kuwa walipata mafunzo ya muda mfupi kupitia idara ya afya
kwenye hospitali ya wilaya ya Kiteto, juu ya namna ya kutengeneza
barakoa hizo.
Mkazi wa
mjini Babati ambaye anafanya kazi ya kuuza samaki kwenye soko kuu la
eneo hilo Sofia Athuman anasema baada ya kupatikana kwa fursa za barakoa
za vitambaa vilivyokuwa vinashonwa na mafundi, ilikuwa nafuu kwao kwani
wataalam wa afya walitoa masharti kwa barakao za awali kutumika kila
baada ya saa mbili au nne na kisha kutumia nyingine.
“Hali
ya uchumi kwa sisi watanzania wa hali ya chini ni ngumu kwani
hatungeweza kuwa na barakoa zile zinazouzwa kwenye maduka ya dawa ambazo
kwa siku unapaswa kutumia zaidi ya nne kwani zinavaliwa kwa masaa,”
anasema.
Anasema barakoa
za kwenye maduka ya dawa zilikuwa zinauzwa kati ya shilingi 1,000 hadi
shilingi 2,000 na zinavaliwa kwa masaa kadhaa na barakoa za vitambaa
vilikuwa vinauzwa shilingi 500 na unavaa na kufua jioni ndiyo sababu
watu wengi wakakimbilia hizo.
Hata
hivyo, mratibu wa UVIKO-19 wa Wilaya ya Babati, Dkt Emmanuel Mkony
anasema vijana wameweza kujipatia fursa ya ajira kwa kutengeneza barakoa
na vitakasa mikono ila baadhi yao walitengeneza barakoa hizo nyingine
hazina viwango vya ubora ambavyo vinahitajika.
Dkt
Mkony anaeleza kuwa baadhi ya barakoa hizo malighafi zilizotumika
hazikupitisha na Wizara ya Afya na ikiwemo vitakasa mikono vingine
vilivyokuwa vinatumika kunawa mikono.
“Baadhi
ya watu walilalamika kupata madhara ya kiafya ikiwemo kubabuka mikono,
kuumwa vichwa, kupata mafua na kukohoa hivyo jamii inapaswa kutumia vitu
ambavyo vimepitishwa na wataalam wa afya,” anasema.
Kwa
upande wake mkazi wa mjini Babati Yusuf Juma anasema kupitia maambukizi
ya ugonjwa wa UVIKO-19 alichangamkia fursa ya kuuza malimao kwa baadhi
ya watu waliokuwa wakijikinga na maradhi hayo.
Anaeleza
kwamba bei ya malimao ilipanda mara dufu kutokana na matumizi yake
kuongezeka ikiaminika kuwa ukipata mchangamnyiko wa limao na tangawizi,
UVIKO-19 itatoweka.
“Biashara
ilikuwa nzuri kwani limao moja lilifika hadi shilingi 500 kutoka
shilingi 100 ya awali, yaani machungwa yalikuwa yana soko kubwa kuliko
limao ila hivi sasa limao ndiyo linaonekana la maana kuliko machungwa,”
anasema.
Mchimbaji wa
madini ya Tanzanite, Paschal Mkumbo anaeleza kuwa japokuwa hapingi suala
la utengenezaji wa barakoa hizo ila anashauri pawepo na wataalam wa
afya wanaokagua kabla ya kutumika.
Mkumbo
anasema mazingira hayakuwa masafi ya barakao hizo za vitambaa kwani
alikuwa anashuhudia watu wanavyonunua kwa mafundi wa nguo na kuzivaa
muda huo huo mdomoni bila kufua au kuzipasi.
Anasema
jamii inapaswa kupatiwa elimu kuwa barakoa ambazo zinaninginizwa tuu
bila kuwekwa kwenye mazingira ya kufunikwa zinapaswa kufanyiwa usafi
kwanza kabla ya kutumika ili kuepuka magonjwa mengine ambayo hayahusiki
na UVIKO-19.
Anaongeza
kuwa watu wanaweza kupata magonjwa mengine ya kifua ikiwemo pumu kwa
kutumia barakoa chafu bila kuzifanyia usafi hivyo kuepuka UVIKO-19 na
kupata maradhi mengine kutokana na kutofanyiwa usafi kabla.
“Mimi
siyo mtaalam wa afya, ni sawa barakoa inapaswa kuvaliwa ili kujikinga
na maambukizi ya UVIKO-19 ila wakaguzi wangepaswa kukagua kwanza na siyo
kila mwenye utaalam wa kushona nguo anatengeneza tuu barakoa yake na
watu wananunua na kuvaa bila kufua na kuipiga pasi,” anamalizia Mkumbo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...