Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji Mstaafu Mheshimiwa Hamisa H. Kalombola ametoa wito kwa Watumishi wa Tume kufanya kazi kwa kushirikiana, bidii, weledi na uzalendo ili kuweza kufikia malengo yaliyowekwa.

Mheshimiwa Jaji Mstaafu Hamisa Kalombola amesema hayo jana alipokutana na Watumishi wa Tume wakati wa ziara yake katika Ofisi za Tume ya Utumishi wa Umma, Jijini Dodoma aliyoifanya kwa lengo la kukutana na Watumishi wa Tume na kuona namna wanavyotekeleza majukumu yao.

“Tume hii ina taswira nzuri na watu wana imani na sisi katika kazi tunazozifanya. Sijasikia habari zenye kuipa Tume yetu taswira mbaya najua mnafanya vizuri, sasa shime shikamaneni, mshirikiane na mhakikishe mnailinda taswira nzuri iliyopo. Epukeni kufanya vitendo visivyofaa na habari mbaya zenye kuichafua Tume ya Utumishi wa umma” alisema Mheshimiwa Jaji Mstaafu Kalombola.

Akizungumza kuhusu umuhimu wa ushirikiano kwa watumishi wa Tume, Mheshimiwa Jaji Mstaafu Kalombola alisema kuwa watumishi wanapaswa wakati wote kufahamu kuwa jambo kubwa katika utendaji wa kazi ni kushirikiana, kuzingatia maadili, kufanya kazi kwa pamoja, kwa kutambua kuwa watumishi wakipambana katika kazi wakiwa wengi na kwa pamoja kazi inakuwa rahisi na pale kwenye changamoto inakuwa ni rahisi kuzitafutia ufumbuzi na hatimaye kufikia malengo waliyojiwekea.

“Tufanye kazi kwa pamoja, sifa yetu kubwa iwe ni kufanya kazi kwa kushirikiana, tupendane na kila mmoja akiwa na tatizo bila kujali nafasi yake aliyo nayo basi tushikamane katika kutatua tatizo. Nimefurahi sana kwa sababu pote nilipopita katika Idara na Vitengo nimejionea kile Katibu alichonieleza kuwa mnachapa kazi. Najua wengine mmekuja hapa Dodoma makazi yenu bado yako kwingineko lakini aliyepo jirani hapa ndio ndugu yako, aliyepo Ofisi nyingine pia ni ndugu yako mshikamane” alifafanua Jaji Mstaafu Mheshimiwa Kalombola.

“Mimi ninatoka hapa nikifahamu kuwa ninyi ni wachapa kazi na ninaomba na mimi mnipe ushirikiano, tuchape kazi pamoja na kama kuna changamoto tuendelee kuchapa kazi, wakati Viongozi na mimi mwenyewe tukizishughulikia. Tukichapa kazi ni vizuri maana hata kama tunaenda kuomba watu wengine watusaidie, watatusaidia kwa sababu tunaonekana tunafanya kazi na wanaona matokeo ya kazi zetu” alisema Mheshimiwa Jaji Mstaafu Kalombola.

Kwa upande wake Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma Bw. Mathew M. Kirama alimhakikishia Mwenyekiti wa Tume kuwa yeye na Sekretarieti yake wataendelea kufanya kazi kwa bidii na kwa weledi na alimhakikishia ushirikiano.

“Mheshimiwa Mwenyekiti nikuhakikishie kuwa tupo kwa ajili ya kuiwezesha Tume yako kufanya kazi zake vizuri. Wafanyakazi wa Tume wanafanya kazi zao vizuri, kielelezo kizuri kuona kiwango cha kazi zao ni kuangalia rufaa na malalamiko yanayowasilishwa na kutolewa uamuzi na Tume. Tunaahidi kuendelea kushirikiana na Tume na pale mtakapoona pana upungufu mtaelekeza ili tuboreshe zaidi katika utendaji wa kazi zetu” 

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma Bw. Mathew M. Kirama (kulia) akifafanua jambo kwa Mwenyekiti wa Tume, Jaji mstaafu  Mhe. Hamisa H. Kalombola (katikati), wakati wa ziara ya Mwenyekiti kutembelea Watumishi wa Tume, Chimwaga Dodoma. Kushoto ni Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Tume, Bw. Bernard Marcelline.

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma Bw. Mathew M. Kirama (wa pili kushoto) akifafanua jambo kwa Mheshimiwa Jaji (Mstaafu) Hamisa H. Kalombola (kulia) Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Tume Jijini Dodoma, kuangalia utendaji kazi wa Tume. (Picha na PSC).

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Mheshimiwa Jaji Mstaafu Hamisa H. Kalombola (kulia) akiwasili katika Ofisi za Tume zilizopo Chimwaga, Dodoma kuzungumza na Watumishi wa Tume hiyo, kushoto ni Bw. Mathew M. Kirama, Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...