Na Mwandishi Wetu,Michuzi TV
WAKATI Siku ya kupinga utumikishwaji wa watoto duniani ikiadhimishwa Juni 12, 2022, kampuni ya JTI Leaf Services imepongezwa kwa uamuzi wake wa kuchangia ujenzi wa shule ya bweni ya wasichana katika Wilaya ya Urambo mkoani Tabora.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni, ‘Utumikishwaji wa watoto ni kikwazo cha maendeleo endelevu, wadau tushikamane kuutokomeza’ ambayo inaenda sambamba na malengo ya JTI Leaf Services ya kutokomeza ajira kwa watoto.
Akizungumzia mradi wa shule ya sekondari ya wasichana ya bweni, Mkurugenzi wa Wilaya ya Urambo, Baraka Zikatimu ameeema mradi huo utawasaidia wanafunzi wa kike wanaoendelea na masomo yao ya sekondari katika shule hiyo inayojengwa na JTI Leaf Services kupitia programu yake ya ARISE kwa kushirikiana na Halmashauri ya Urambo.
“Mradi huu utasaidia kupunguza utumikishwaji wa watoto hasa wa kike kwani watakuwa wanakaa shuleni na kuwapa walimu wepesi wa kuwafuatilia kwa ukaribu na pia kuwaepusha na shughuli hatarishi,” alisema na kusisitiza kuwa serikali inafanya kazi kwa karibu sana na JTI Leaf Services ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa viwango ili wasichana kutoka ndani na nje ya Urambo wasajiliwe shuleni hapo,"amesema.
Ameongeza mradi huo pia unalenga kusaidia kupunguza mimba za utotoni kwani wanafunzi wengi hawatalazimika tena kutembea mwendo mrefu kwenda shuleni jambo ambalo huwaweka katika hatari ya kupata mimba kutokana na vishawishi wanavyokutana navyo barabarani.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, serikali ilitoa eneo la mradi huo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha linapimwa na kupata hati, kuwatoa wataalamu wakiwemo wahandisi wanaosimamia mradi huo, imetoa usafiri wa malighafi na pia kusisitiza kuwa mradi huo umetengeneza ajira kwa wakazi wa Urambo.
Katika hatua nyingine, Meneja Miradi ya Kijamii wa JTI Leaf Services, Oscar Lwoga alisema kuwa JTI Leaf Services kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania, Shirika la Kazi Duniani (ILO) na Winrock International walitekeleza mradi wa ARISE kwa awamu ya pili kuanzia 2016-2018.
Katika mradi huo waliangazia hasa masuala ya kujenga ufahamu, kuwajengea wananchi uwezo, kuwawezesha kiuchumi na kuhakikisha haki za mtoto zinazingatiwa kisheria.
Kwa mujibu wa Lwoga amesema JTI Leaf Services ilishirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine, kuboresha mazingira ya shule mbalimbali. Ambapo walikarabati madarasa 17 na ofisi tano za walimu mkoani Tabora, ujenzi wa shule mbili katika vijiji vya Igagara na Migungumalo.
Pia kupanua shule za msingi Mpilipili na Chali, ujenzi wa vyoo katika shule 16, ujenzi wa nyumba nne za walimu na familia zao. Wamesambaza madawati 1520 katika shule 16 na kuchimba visima 26 vya maji hasa katika jamii zinazozungukwa na shule.
Wakati huo huo Mwalimu Mkuu wa Shule ya Chali, Bwire Mbuya alisema juhudi za JTI Leaf Services katika kuboresha elimu zimechangia kupunguza ajira kwa watoto kwa asilimia 95 katika shule yake. Aliongeza kuwa wazazi wengi wamevutiwa kuwapeleka watoto shuleni kutokana na mazingira ya kufundishia ni mazuri.
JTI Leaf Services, ambayo ni sehemu ya makampuni ya JT, ni moja ya makampuni makubwa yanayojihusisha na ununuzi wa tumbaku nchini Tanzania.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...