BAADHI ya wanaume wamekuwa wakitumia dawa za kuongeza nguvu za kiume kiholela na bila kufuata ushauri wa daktari hali inayopelekea madhara makubwa ikiwemo kifo, kuzimia, mshtuko wa moyo na tatizo la kiharusi kwa mujibu wa taaifa zisizo rasmi zilizoripoti visa vya matumizi ya dawa hizo.
Katika kuhakikisha jamii inakuwa salama Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA,) imeendelea kutoa elimu kwa jamii hasa katika kuepuka matumizi holela ya dawa za kuongeza nguvu za kiume na kujikita zaid katika kutatua matatizo ya kisaikolojia yanayochangia kwa kiasi kikubwa tatizo la upungufu wa nguvu za kiume na ikishindikana muathirika wa tatizo hilo amuone daktari ili awe kupata dawa sahihi na maelekezo ya namna ya kuzitumia.
TMDA imekuwa ikikutana na wadau mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari na wadau wa Asasi za kiraia na kutoa elimu kwa Umma ili jamii iweze kuepukana na madhara ya matumizi holela la dawa hizo, na katika mkutano uliowakutanisha na waandishi wa habari kanda ya nyanda za juu Kusini uliofanyika jijini Mbeya wiki hii Mamlaka hiyo ilieleza namna wanavyopambana katika kuhakikisha jamii inalakuwa salama dhidi ya matumizi holela ya dawa hizo.
Kwa mujibu wa TMDA upungufu wa nguvu za kiume ni matatizo katika mfumo wa uzazi wa mwanaume yanayopelekea uume kuwa na uwezo mdogo au kutokuwa na uwezo kabisa wa kuhimili tendo la ndoa kwa muda mrefu, na dawa zilizosajiliwa na Mamlaka hiyo kwa ajili ya tatizo hilo ni Sildenafil (Evoke, Erecto, Zwagra, Silmet, Njoi na Vagra,) Tadafil (Saheal na Cialis,) pamoja na Vardenafil (Levitra.)
Namna dawa za kuongeza nguvu za kiume zinavyofanya kazi
Kwa mujibu wa TMDA dawa hizo hupelekea mzunguko wa damu kuwa mzuri ndani ya mishipa ya uume na kuongeza kiwango cha damu katika sehemu hizo na kusababsha uume kusimama vizuri na zinatumika kutibu wanaume waliogundulika kuwa upungufu wa nguvu za kiume wenye uwezo mdogo na wasio na uwezo kabisa wa kuhimili tendo la ndoa kwa muda mrefu na mwanaume aliyegundulika na tatizo hilo kitaalamu daktari atamchagulia aina ya dawa na kumpa maelekezo sahihi juu ya matumizi sahihi ya dawa hizo.
Imeelezwa kuwa dawa hizo hazitafanya kazi moja kwa moja au kwa ufasaha zaidi ikiwa tatizo hilo la kupungukiwa nguvu za kiume limesababishwa na kuathirika kisaikolojia ikiwemo kutokujiamini, kukosa hamu ya kufanya mapenzi, woga au kuwa na hofu ya kimapenzi kwa mweza.
Ukweli kuhusu dawa hizi kuponyesha tatizo la nguvu za kiume
Tafiti za kitaalamu zinaonesha kuwa dawa hizi hazitibu kabisa tatizo la kupungukiwa nguvu nza kiume na haziiongezi hamu au shauku ya kufanya mapenzi, na kwa kawaida huchukua takribani dakika 30 ili kuanza kufanya kazi mwilini kama hakuna mwingiliano wa dawa nyingine mwilini na hushauriwa kutumika ndani ya saa moja kabla ya tendo na haishauriwi kutumia dawa hizo zaidi ya mara moja kwa siku.
Hali ya matumizi ya dawa za kuongeza nguvu za kiume ilivyo nchini
Matumizi ya dawa za kuongeza nguvu za kiume yamekuwa yakiongezeka siku baada ya siku hali inayoonesha kuwa wanaume wengi wameathirika na tatizo la upungufu wa nguvu za kiume na TMDA inafanya tafiti ili kuweza kugundua kiwango cha matumizi ya dawa hizo.
Matibabu bila kutumia dawa za kuongza nguvu za kiume
Matatizo ya upungufu wa nguvu za kiume husababishwwa na sababu mbalimbali ikiwemo unywaji wa pombe kupita kiasi, kutofanya mazoezi, ukubwa wa mwili, uvutaji wa sigara au dawa za kulevya, msongo wa mawazo, uwepo wa vichocheo hafifu vya nguvu za kiume na ulaji usiofaa na muathirika anaweza kuamua kupona au kupunguza kiwango cha tatizo hilo kwa kuadilisha au kuachana na sababu zinazopelekea tatizo hilo.
Katika kuhakikisha usalama na ubora wa dawa hizo katika kulinda afya za watanzaniia TMDA imekuwa ikifanya tathmini kubwa ya dawa zinazoletwa katika usajili ili kujiridhisha ubora, ufanisi na usalama kabla ya kusajiliwa, kufanya ukaguzi katika viwanda na maduka pamoja na kutoa elimu kwa Umma juu ya matumizi sahihi ya dawa hizo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...