Na Prisca Ulomi, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Dodoma
Wawakilishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) wakiongozwa na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende leo tarehe 18 Juni, 2022 wameshuhudia makabidhiano ya eneo la ujenzi wa Ofisi za Makao Makuu ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali lenye ukubwa wa mita za mraba 17,342.
Makabidhiano hayo yamefanyika kwenye Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma baina ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ambaye ni Mshauri Elekezi aliyewakilishwa na Msanifu Majengo Weja Ng’olo na Kampuni ya Ujenzi ya SUMA JKT ambae ni Mkandarasi iliyowakilishwa na Mkadiriaji Majenzi, Jacob Ghati.
Akikabidhi eneo hilo, Mwakilishi wa TBA, Ng’olo ameeleza kuwa jengo la Ofisi linalotarajiwa kujengwa ni la kisasa na ni miongoni mwa majengo yenye muonekano mzuri katika Mji wa Serikali Mtumba. Jengo hili litakuwa na miundombinu mbalimbali ikiwemo vyumba vya Ofisi 127, maegesho ya magari 111, maktaba, kumbi 2 za mikutano zenye nafasi 108 kila mmoja, kumbi 2 za kutolea mafunzo zenye nafasi 42 kila mmoja, maabara ya kompyuta, vyumba vidogo 10 vya mikutano na chumba cha akina mama wanyonyeshao. Ujenzi wa jengo hilo unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi kumi na nane (18).
Akizungumza kwa niaba ya Mkandarasi, Gati amesema kuwa wako tayari kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa mujibu wa mkataba na kwa kushirikiana na Mshauri Elekezi (TBA) na Mshitiri (OWMS).
Kwa upande wake, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Luhende amewatakia Mkandarasi na Mshauri Elekezi utekelezaji mwema wa majukumu yao kwa mujibu wa mkataba na kwa kuzingatia weledi. Pia amewahakikishia kuwa Ofisi ya Wakili Mkuu Serikali itawapa ushirikiano unaostahili.
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende akikata utepe kwa ajili ya makabidhiano ya nyaraka za ujenzi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali inayotarajiwa kujengwa katika Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma. Wa kwanza kulia ni Mhasibu Mkuu wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, CPA. Devotha Ngulugulu.
Naibu
Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende (aliyesimama katikati)
akiwa na wawakilishi wa Kampuni ya Ujenzi ya SUMA JKT na TBA pamoja na
baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali baada ya hafla
fupi ya kukabidhi eneo la ujenzi wa jengo la makao makuu ya Ofisi ya
Wakili Mkuu wa Serikali lililopo Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma.
Naibu
Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende (wa tatu kulia) akipata
maelezo kutoka kwa mwakilishi wa TBA, Msanifu Majengo Weja Ng’olo na
Mwakilishi wa SUMA JKT, Jacob Gati (wa kwanza kushoto) wakati wa
makabidhiano ya eneo la ujenzi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali
kwenye Mji wa Serikali Mtumba Dodoma.
Naibu
Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende (wa pili kulia)
akishuhudia wawakilishi wa TBA wakiwaonesha mipaka wawakilishi wa
Kampuni ya Ujenzi ya SUMA JKT. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Utawala
na Rasilimali Watu Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Bw. James Kibamba
na kulia ni Mkurugenzi wa Mipango, Dkt. Abdul Mussa.
Naibu
Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende (wa tano kulia) akiwa
kwenye picha ya pamoja na wawakilishi wa Kampuni ya Ujenzi ya SUMA JKT
na TBA na watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wakati wa
makabidhiano ya eneo kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi Mji wa Serikali
Mtumba, Dodoma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...