Mratibu wa Malaria Mkoa wa Singida, Dk.Abdallah Balla, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) mjini hapa jana wakati akitoa taarifa ya ugawaji wa vyandarua kwa wanafunzi wote mkoani hapa kuanzia darasa la kwanza hadi saba.
 Mratibu wa Kamati ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Singida, Happy Francis, akizungumza katika mkutano huo.
Mwenyekiti wa Kamati za Dini Mkoa wa Singida, Khamis Kisuke,  akizungumza.
Mchungaji wa Kanisa la Sabato Wilaya ya Manyoni,Mchungaji. Joel Ndegea, akizungumza kwenye mkutano huo.


 Na Dotto Mwaibale,  Singida

 WANAFUNZI wa shule zote za  msingi za Serikali na zisizo za Serikali katika Mkoa wa Singida, watagawiwa vyandarua  kuanzia Julai mwaka huu ikiwa ni utekelezaji wa afua zakupambana na ugonjwa wa malaria nchini.

Mratibu wa Malaria Mkoa wa Singida, Dk.Abdallah Balla, alisema hayo wakati  akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa na kwamba vyandarua hivyo vitagawiwa kwa wanafunzi wa kuanzia darasa la kwanza hadi saba.

Dk.Balla alisema zoezi la kugawa vyandarua hivyo ambavyo vitakuwa takribani 200,000  litaanza mara baada ya Bohari ya Dawa (MSD) kuvitoa na kuanza  kuvipeleka mashuleni.

Dk.Balla alisema vyandarua hivyo vitagawiwa bila kujali wapo wangapi kwenye kaya kwani lengo la serikali ni kutaka kuifanya Tanzania iwe huru kwa ugonjwa wa malaria ifikapo 2030.

Aliongeza katika kuhakikisha zoezi la kugawa vyandarua hivyo linafanikiwa, viongozi wa dini wamepewa semina ili wasaidie kuwaelimisha wananchi kwenye nyumba za ibada  umuhimu wa vyandarua hivyo.

Aliwataka wananchi waendelee kutunza mazingira kwa kuondoa maeneo ambayo maji yanaweza kutuwama kwani ndiyo yanakuwa chanzo cha mazalia ya mbu.

Naye Mchungaji wa Kanisa la Waadiventisti Wasabato Wilaya ya Manyoni, Joel Ndegea, alisema wananchi watambue kuwa serikali imetumia fedha nyingi kununua vyandarua hivyo wahakikishe wanavitumia kupambana na malaria na sio kwenda kuvitumia kuvulia samaki au kufugia kuku.

Kwa upande wake Mratibu wa Kamati ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Singida, Happy Francis, alisema vyandarua hivyo vimekuja katika muda mwafaka hivyo wanafunzi watakapogawiwa wazazi wahakikishe wanavitumia kwa malengo yanayosudiwa na si vinginevyo.

Naye Mwenyekiti wa Kamati za Dini Mkoa wa Singida, Khamis Kisuke, aliipongeza serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wa kutoa vyandarua hivyo na kuahidi kuwa watahakikisha wanawahamasisha wananchi ili wavitumie kwa lengo la kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...