Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
SERIKALI
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu
zimekamilisha majadiliano ya mkataba wa kuondoa utozaji Kodi Mara
Mbili na Kuzuia Ukwepaji wa Kodi ya Mapato kati ya nchi hizo mbili.
Nyaraka
za kufikiwa kwa majadiliano hayo zimetiwa Saini jijini Dar es Salaam na
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru,
Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu nchini Tanzania Mheshimiwa Khalifa
Abdulrahman Almarzooqi na Bw. Abdullah Ahmed Al Obaidali, ambaye ni
Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Fedha ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE)
anayeshughulikia Ushirikiano wa Kimataifa na Mashirika ya Fedha.
Bw.
Mafuru alieleza kuwa makubaliano hayo yatakayofuatiwa na utiaji Saini
mikataba yake muda si mrefu yanafuatia jitihada za Mheshimiwa Samia
Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizozifanya hivi
karibuni katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu ambapo aliagiza
kuondolewa kwa changamoto hiyo ili kukuza mahusiano ya kiuchumi,
kuimarisha ushirikiano katika masuala ya kodi na kuchochea mazingira
wezeshi ya uwekezaji.
“Ni
matumaini yetu kwamba baada ya mkataba huu kukamilika tutaona uwekezaji
mkubwa ukija baina ya nchi zetu hizi na hasa kutoka Uarabuni ambao wana
mitaji mikubwa lakini utozaji kodi mara mbili ulikuwa unawakwaza, hata
wawekezaji, wafanyabiashara wa Tanzania wataweza kufanya biashara bila
kuwa na mashaka ya kutozwa kodi mara mbili hivyo kuongeza ukuaji wa
uchumi wa nchi hizi mbili” alisema Bw. Mafuru.
Kwa
upande wake Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu nchini Tanzania
Mheshimiwa Khalifa Abdulrahman Almarzooqi alisema kuwa hatua iliyofikiwa
ya kuondoa utozaji kodi ya mapato mara mbili kati ya Tanzania na UAE
kutavutia wawekezaji wengi aidi kutoka katika nchi za Umoja wa Falme za
Kiarabu na kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi.
Alipongeza
jitihada zinazofanywa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kuboresha mazingira ya uwekezaji
nchini na kufanikisha jambo hilo la kuondoa utozaji wa kodi ya mapato
mara mbili na kwamba hatua hiyo itavutia mitaji na wawekezaji wengi
kutoka nchi za Kiarabu kuja kuwekeza Tanzania.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...