Na Mwandishi Wetu, Michuzi Tv
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa kilimo nchini Tanzania (TARI) Dkt. Geoffrey Mkamilo amefanya ziara katika wilaya ya Buhigwe Mkoani Kigoma na kushauri kuchukuliwa kwa hatua za kukabiliana na migomba iliyoathirika na ugonjwa wa zao la migomba ambao unaosadikika kutokea nchini Kongo, Burundi na Rwanda unaojulikana kama Banana Bunchy Top Virus (BBTV) na kuahidi kutoa ushirikiano katika kukabiliana na ugonjwa huo nchini.
Dkt. Mkamilo ambaye katika ziara hiyo ameambatana na jopo la watafiti na wataalam wa zao la migomba kutoka TARI, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe Dkt.Themistocles Kamugisha pamoja na Afisa Kilimo wa Wilaya (DAICO)
Ndugu Weisy Wikedzi ameeleza kuwa baada ya kupata taarifa za uwepo wa ugonjwa huo, alituma wataalamu kutoka TARI ambao walichukua sampuli na kuzipeleka kupimwa maabara ambapo zilitoa matokeo chanya kuashiria uwepo wa ugonjwa huo wa Banana Bunchy Top Virus.
Ugonjwa huo ambao umeathiri sehemu kubwa ya mashamba ya migomba Wilayani Buhigwe na katika maeneo mengine mkoani Kigoma unaelezwa kusambazwa na wadudu mafuta (Aphids) pamoja na matumizi ya mbegu ambazo zimebeba vimelea vya ugonjwa huo.
Akielezea mikakati iliyoandaliwa na TARI kukabiliana na ugonjwa huo, MkurugenziMkuu wa TARI Dkt. Mkamilo ameeleza kuwa hatua ya kwanza ni kutoa elimu kwa Maafisa Kilimo kuhusiana na ugonjwa huo,dalili na athari zake pamoja na kuwaeleza hatua za kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na matumizi sahihi ya mbegu bora za migomba zinazostahimili magonjwa.
Dkt. Mkamilo katika ziara hiyo amegawa miche 220 ya aina tano za mbegu za migomba za TARIBan1, TARIBan2, TARIBan3 TARIBan4 na Fhia23 ambazozinavumilia magonjwa (Desease resistant variety) kutoka Kituo cha TARI Maruku kwa Halmashuri ya Buhigwe ili wazalishe miche zaidi ( seed multiplication) kama hatua ya kukabiliana na ugonjwa huo.
Aidha, Dkt. Mkamilo amewashauri Maafisa Kilimo na Wakulima katika Halmashauri hiyo kuondoa migomba iliyoathirika na ugonjwa huo, kuiteketeza na kuacha shamba bila kupanda mazao kwa kipindi cha miezi minne hadi sita ili kutokomeza vimelea vyugonjwa kabla ya kupanda tena migomba.
Akipokea miche hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Buhigwe DktThemistocles Kamugisha ameushukuru Uongozi wa TARI kwa hatua hizo za kubaini uwepo wa ugonjwa huo katika Halmashauri ya Buhigwe, kutoa elimu kwa Maafisa ugani na wakulima kuhusiana na ugonjwa huo pamoja na hatua ya kuwagaia miche ya migomba inayostahmili magonjwa ili wakazalishe mbegu zaidi.
Kwa mujibu wa mtafiti wa zao la migomba kutoka Kituo cha TARI Maruku Alexander Fayu, migomba iliyoathirika na ugonjwa huo wa Banana Bunchy Top Virus (BBTV) huonyesha dalili za kudumaa, majani yake husinyaa, kukakamaa na hubadilika kuwa ya njano na mgomba ulioathirika hautoi mkungu.
Mkurugenzi
Mkuu wa Taasisi ya Utafiti nchini Tanzania (TARI) Dr. Geoffrey Mkamilo
akikabidhi miche ya migomba kwa Afisa kilimo wa wilaya ya Buhigwe
(DAICO) ndugu Weisy Wikedzi
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...