Mtendaji Mkuu wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Dtk. Edwin Mhede amesema jukumu la kuwasaidia watu wenye uhitaji ni wajibu wa kisheria kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 11(i) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 pamoja na marekebisho yake, na ndiyo maana Wakala wa DART ukaweka kitengo maalumu cha kuratibu namna ya kuwahudumia abiria wenye uhitaji.

Dkt. Mhede amesema hayo wakati wa kufungua kikao kilichoandaliwa na Wakala wa DART na kuwashirikisha  Wadau kutoka Makundi Maalumu wakimemo Wazee, Walemavu, Wanafunzi, Wajawazito na Wagonjwa kwa lengo la kuboresha huduma zitolewazo katika Mfumo wa Mabasi Yaendayo Haraka.

“mtu ana haki ya kusaidiwa katika hali ya uzee, pili katika hali ya ugonjwa na au katika hali nyingine yoyote ya kutokujiwezahii ni kwa mujibu wa sheria mama yetu” alisema Dkt Mhede Juni 02, 2022 katika Ukumbi wa TAMISEMI Magogoni mkoani Dar es salaam.

Aidha Dkt. Mhede alisema vikao vya aina hiyo ni lazima kufanyika muda wote ili kuona endapo huduma itolewayo na Wakala wa DART kama inakidhi mahitaji ya wateja wake au inakabiliwa na changamoto zinazohitaji kutatuliwa.

“Hiki ni kikao muhimu sana kwani katika mradi wetu ni lazima mara zote tuwe vikao na wadau ili kujikumbusha kama tunaenenda  sawa sawa au kuna mahala hatuendi sawasawa” alisema Dkt. Mhede.

Vilevile Dkt. Mhede amesisitiza matumizi ya lugha nzuri kwa kuwasihi wadau hao kutumia lugha yenye staha na heshima pale wanapohudumiwa na Watumishi wa DART kule katika vituo vya mabasi yaendayo haraka kwani na wao ni binadamu na kwamba wanaumia endapo wataongeleshwa katika lugha isiyokuwa nzuri.

Pia amewataka Watumishi wa DART kuzingatia lugha ya biashara muda wote ikiwemo kutabasamu kama lugha ya biashara isiyotoa maneno.

  ”Jamani lugha ni biashara, lugha ndiyo huponya watu. Mtu hata akikosa huduma aliyotaka kutoka kwako lakini kama umemjibu kwa lugha nzuri huku ukitabasamu ataondoka akiwa amefarijika na kuona kwamba ulikuwa na dhamira ya kumuhudumia” alisema Dkt. Mhede.

Kwa upande wake mmoja wa wadau hao ameonyesha kufurahia huduma ya Mabasi Yaendayo Haraka mbali ya kuwepo kwa changamoto ndogo ambazo anaamini Wakala wa DART utazifanyia kazi ili kuziondosha kabisa.

“Wakati huduma inaanza tulikuwa tunatangaziwa vituo  na mfumo mliouweka katika mabasi yenu lakini siku hizi hatusikii mabasi yakitanganza vituo tena. Hii ilikuwa inawasaidia wenzetu wasioona kwani walikuwa hawalazimiki kumuuliza mtu hapa ni wapi?” alisema Mwl. Hanifa Mbata ambaye ni mweka hazina wa Chama wa Wagonjwa wa Akili (TAMH).

Naye Wakili Gideon Mandesi kutoka Chama cha Wasioona, alisisitiza utungwaji wa kanuni za maadili katika kuwahudumia watu wenye mahitaji maalumu na kutaka huduma zitolewazo na Wakala wa DART ziwe na muendelezo.

Katika kikao hicho cha siku moja Wajumbe wa kikao husika watajadili changamoto za utoaji huduma na kuweka mikakati ya pamoja ili kukabiliana na changamoto zilizojitokeza katika mfumo wa mabasi yaendayo haraka.Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Dr. Edwin Mhede akisisitiza jambo wakati akifungua kikao kilichoandaliwa na Wakala wa DART na kuwashirikisha Wadau kutoka Makundi Maalum kilicholenga kuboresha huduma zitolewazo katika Mfumo wa DART. Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa TAMISEMI Magogoni tarehe 02 Juni 2022.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...