* Wananchi Tabora wachangamkia vyeti vya kuzaliwa vya watoto

KABIDHI Wasii Mkuu Bi. Angela Anatory ametembelea na kukagua vituo vya tiba vinavyotoa huduma ya mama na mtoto na Ofisi za Watendaji Kata ambapo zoezi la usajili na kuwapatia vyeti vya kuzaliwa  linafanyika, pia amezungumza na Wananchi waliofika kupatiwa huduma katika vituo hivyo hii leo Mkoani Tabora.

Bi. Anatory amesema kuwa  amebaini changamoto mbalimbali zilizojitokeza wakati zoezi hilo likiendelea hasa kwa baadhi ya Wazazi kutokuwa na kumbukumbu wa nyaraka muhimu zinazoonesha tarehe na mwaka wa kuzaliwa mtoto pamoja na majina sahihi ya wazazi wote wawili wa mtoto jambo ambalo limechangia kwa baadhi ya Wananchi kuchelewa kupatiwa huduma hiyo.

‘’Ndugu wananchi msiwe na wasiwasi mpango huu ni endelevu na kila mtoto mwenye sifa atasajiliwa na kupatiwa cheti chake cha kuzaliwa, na sisi viongozi wenu tuliopewa zamana ya kusimamia hilo tunapita na kukagua ili changamoto zinazojitokeza tuweze kuzitatua kwa wakati.’’Alisema Bi. Anatory.

Kwa upande wake Muuguzi ambaye pia ni msajili msaidizi katika Zahanati ya Ng’ambo Bw.Verus Samson amesema wameweka utaratibu wa kuwapatia namba wananchi ili kupunguza msongamano kutokana na mwitikio kuwa mkubwa hivyo kuwapa nafasi wananchi kuendelea na shughuli zao za kila siku badala ya kukaa foleni muda mrefu.

‘’Tumeweka utaratibu wa kutoa namba, kwa kila siku tunatoa namba mia moja wengine tunawaambia warudi kesho ambao hao ndiyo tunaanza nao asubuhi na mapema na huu utaratibu umetusaidia kupunguza foleni na msongamano’’.Alisema Bw. Samson.

Wakati huo huo baadhi ya wanachi wameeleza na kuipongeza Serikali kwa kuwaletea huduma karibu na makazi yao kwani hapo awali walishindwa kufuatilia vyeti hivyo katika Makao Makuu ya Wilaya ambapo usajili unafanyika.

Bi. Elizabeth Daniel kutoka Zahanati ya Ng’ambo mara baada ya kukabidhiwa cheti cha mtoto wake John Paul amesema cheti hicho kitamsaidia mtoto wake akifikisha umri wa kuanza shule na kwa sasa wanataka kumkatia bima ya afya hivyo kinahitajika kwa haraka ili mwanawe apatiwe matibabu.

Kwa upande wake Bw.Hamadi Paulo ambaye alifika katika ofisi ya Kata Ng’ambo kumsajili mtoto wake Paul Hamadi na kusema kuwa cheti hicho atakitunza hadi ukubwani kwake kwani alishuhudia baadhi ya wananchi waliokosa ajira katika mradi wa Reli ya SGR kwa kukosa vyeti vya kuzaliwa hivyo amejifunza umuhimu wa nyaraka hiyo kwa mtoto kutimiza ndoto yake hapo baadaye.

Mpango wa usajili na kuwapatia vyeti vya kuzaliwa watoto wa umri chini ya miaka mitano ulizinduliwa rasmi Juni 3, 2022 Mkoani Tabora na zoezi linaendelea ambapo mpaka sasa watoto wapatao 9,108 wamesajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa bure katika vituo vya tiba vinavyotoa huduma ya mama na mtoto na ofisi za watendaji Kata na usajili bado unaendelea na taarifa zinapokelewa kutoka vituoni kielekroniki hadi katika kanzi data ya RITA Makao Makuu Jijini Dar es salaam..





 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...