Vodacom Tanzania Plc imeanza kutoa mgao wa Shilingi 3.3 bilioni kwa watumiaji wake zaidi ya 7.7 milioni, ikiwa ni sehemu ya faida iliyopatikana kwenye akaunti za M-Pesa. Malipo haya yanategemewa kukamilika tarehe 17 Juni, ambapo wateja wote watakuwa wameshapokea mgao wao na kufanya idadi itakayotolewa kwa ujumla kufikia Shilingi 174 bilioni tangu kampuni hiyo ianze kugawa faida kwa wateja wake
Akifafanua kuhusu gawio hilo la M-Pesa, Mkurugenzi wa M-Pesa Epimack Mbeteni, alisema, “tuna furaha kubwa sana kuona kuwa huduma ya M-Pesa inaendelea kuwa msingi wa shughuli za kibiashara pamoja na maisha ya kila siku ya wananchi hapa nchini. Tuko katika mchakato wa kugawa Shilingi 3.3 bilioni kwa wateja wetu ambao wamekuwa wakitumia mfumo wetu kwa kipindi hiki, na malipo yanaingia moja kwa moja katika akaunti zao za M-Pesa.”
Faida italipwa kwa wateja, mawakala, wakala mkuu na wadau wengine wa kibiashara wa M-Pesa kulingana na matumizi yao ya huduma za M-Pesa. Gawio linategemea kiasi cha matumizi ya huduma katika kipindi hicho cha robo ya kwanza ya mwaka 2022 (Januari hadi Machi). Shughuli hizo ni pamoja na kuhamisha pesa, kulipa bili, manunuzi ya muda wa maongezi na mengine.
Wateja wanaweza kutuma neno “KIASI” kwenda namba 15300 ili kuona kiasi cha gawio watakalopokea. Mara baada ya kupokea mgao, wateja wa M-Pesa wanaweza kutumia gawio hilo kwa njia ya kutoa pesa taslimu, kununua vifurushi vya maongezi na data au kutumia kulipia bili au manunuzi ya bidhaa.
Bw. Mbeteni alimalizia kwa kusema, “Mfumo huu wa kipekee umekuwa na nafasi kubwa katika kujenga hali ya ushirikishwaji na upatikanaji wa huduma za kifedha nchini. Wanawake na vijana wameona unafuu na urahisi wa kutumia M-Pesa na wanatumia huduma nyingi ili kuboresha maisha yao. Pia mfumo umekuwa rasilmali muhimu katika kuwezesha biashara ndogondogo na kupambana na changamoto zilizosababishwa na mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO -19. Kwetu Vodacom Tanzania, dhamira yetu ni kuhakikisha kuwa mfumo huu tunauboresha ili kuendana na mahitaji ya wateja wetu.”
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...