
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Jenista Mhagama Mhagama akizungumza wakati wa akifungua rasmi Programu ya Mafunzo ya Uongozi kwa Viongozi Wanawake katika utumishi wa umma yaliyoandaliwa na taasisi hiyo.Programu hiyo imeaandaliwa na Taasisi ya UONGOZI kwa kushirikiana na Serikali ya Finland..jpeg)
.jpeg)
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Jenista Mhagama Mhagama(kulia) akiwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Dk.Kadari Singo(katikati) na Mbunge wa Jimbo la Urambo Marigareth Sitta (kushoto) wakifuatilia hotuba ya Mwakilishi Mkazi UN Women Tanzania Hodan Addou(hayuko pichani).

Baadhi ya washiriki wakifuatilia kwa maelezo yaliyokuwa yakitolewa kuhusu umuhimu wa mafunzo hayo ya uongozi kwa wanawake viongozi Tanzania.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI Kadari Singo akisisitiza jambo wakati wa ufunguzi wa program hiyo.
.jpeg)
Mwakilishi Mkazi UN Women Tanzania Hodan Addou akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya muda mfupi ya uongozi kwa viongozi wanawake Tanzania.

Balozi wa Finland nchini Tanzania Riitta Swan akielezea hatua ambazo zinazuchukuliwa na nchi yake katika kusaidia kufanikisha program hiyo ya uongozi kwa viongozi wanawake .Filanda imekuwa mdau mkubwa wa Taasisi ya UONGOZI katika kufanikisha masuala mbalimbali yanayohusu utoaji mafunzo kwa viongozi.
Na Said Mwishehe, Michuzi TV
WAZIRI,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Jenista Mhagama amesema kwa miaka mingi ya nyuma uwakilishi wa wanawake katika nafasi za uongozi na ngazi za maamuzi ulikuwa hauridhishi ila kutokana na jitihada za dhati za Serikali hali inaimarika kila kukicha.
Amesema wanawake viongozi wanaongezeka katika ngazi mbalimbali za maamuzi huku akieleza anaona faraja Taasisi ya Uongozi yenye jukumu la kukuza uelewa na ujuzi wa masuala ya uongozi imeona umuhimu wa kuwajengea uwezo viongozi wanawake.
Waziri Mhagama ameyasema hayo leo Juni 20,2022 wakati akifungua rasmi Programu ya Mafunzo ya Uongozi kwa Viongozi Wanawake katika utumishi wa umma yaliyoandaliwa na taasisi hiyo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, amesema ni muhimu kutolewa kwa mafunzo hayo kwani yanaunga mkono jitihada za dhati za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kufikia taifa lenye usawa wa kijinsia katika mambo mbalimbali ikiwepo suala la uongozi.
“Niwapongeze sana Taasisi ya UONGOZI kwa kuandaa programu hii muhimu kwetu na kwa taifa. Idadi ya wanawake katika nafasi za uongozi imekuwa ikiongezeka duniani kote kwa miaka mingi. Ongezeko hilo linahusishwa na mipango ya kitaifa na kimataifa inayosisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa wanawake katika uongozi.
“Na maamuzi katika mashirika ya umma, binafsi na ya kiraia (CSOs). Mipango hiyo inatetea usawa wa kijinsia katika nafasi ya uongozi na hivyo kukuza ushirikishwaji wa wanawake katika uongozi na kufanya maamuzi,”amesema.
Ameongeza kwa hiyo uwakilishi na mchango wa wanawake katika kutatua changamoto za maendeleo umeshuhudiwa kwa uzito duniani katika miongo michache iliyopita.
Amesema ripoti ya Wanawake kwenye siasa iliyochapishwa na Umoja wa Mataifa (UN) na Chama cha Mabunge Duniani (IPU) Januari 2021, imebaini kuongezeka kwa nafasi za uongozi kiutendaji, Serikali na bungeni ambazo zinashikiliwa na wanawake katika nchi mbalimbali duniani.
“Hadi Januari 1 mwaka huu, marais waliochaguliwa ni 9 kati ya 152 (sawa na asilimia 5.9), ilihali wakuu wa nchi wanawake ni katika nchi 13 kati ya 193 (sawa na asilimia 6.7). Ulaya inaongoza kwa kuwa na wanawake wengi zaidi wanaoongoza nchi.
Amesema kwa upande wa Afrika, japokua nchi nyingi hazijafikia asilimia 50 au zaidi, bado zimeongeza idadi ya wanawake mawaziri. Mathalani, Namibia imeshuhudia ongezeko kubwa kutoka asilimia 15 hadi 39 ya mawaziri wanawake.
Amesema Tanzania, idadi ya wanawake katika nafasi za juu za uongozi bado ni ndogo. Takwimu zinaonesha kuna asilimia 26 ya wanawake viongozi ukilinganisha na viongozi wanaume ambao wapo kwa asilimia 74.
Pamoja na hayo amesema bado kuna kazi kubwa ya kuwawezesha wanawake katika sekta mbalimbali ili kufikia taifa lenye usawa wa kijinsia katika Uongozi.Changamoto ya kuwa na ufinyu wa wanawake katika uongozi haionekani tu katika sekta ya umma bali pia inajitokeza katika sekta binafsi na asasi za kiraia,”amesema.
Hata hivyo, maendeleo ya kitamaduni pamoja na mageuzi yanayoendelea katika mifumo ya elimu yanatoa nafasi ya kuboresha. Uwakilishi mkubwa wa wanawake katika ngazi za chini unaweza kubadilishwa kuwa fursa ikiwa programu mahususi na maalum kama hii ya kuwajengea uwezo viongozi zitakuwa endelevu kwa viongozi wote wanawake.
“Mipango kama hii ina uwezekano wa kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi za juu za kufanya maamuzi nchini. Naipongeza sana Taasisi ya UONGOZI kwa kuliona hili na kuchukua hatua ya kuwezesha kundi hili maalumu na muhimu katika jamii na taifa.
Licha ya kuwa na mila, desturi na taratibu zinazokwamisha juhudi za Serikali za kuwawezesha wanawake kujikita kwenye nafasi za uongozi.“Zipo sababu nyingine nyingine zinazowakwamisha wanawake kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi.
“Mara kwa mara, tumeona viongozi wanawake wenye uthubutu wakiitwa majina tofauti kama ‘Jike Dume’, ‘Mwanamke wa Chuma’ (Iron lady). Kubambikiana majina haya wakati mwingine huwa ni kero na labda huwafanya wanawake kuwa dhaifu.Pia udhalilishaji wa kijinsia vyuoni, makazini na hata kwenye mitandao ya kijamii (social media).
“Mifumo isiyotambua na kutoa nafasi ya kukidhi mahitaji ya lazima ya jinsia ya kike; mfano mafao ya mama wajawazito na wanaonyonyesha makazini, bado ni changamoto kwa ustawi wa viongozi wanawake,”amesema Waziri Mhagama.
Aidha Serikali itaendelea kuandaa sera na miongozo yenye kutoa kipaumbele kwa watoto wa kike kupata elimu ya msingi, sekondari, shule za ufundi na vyuo vikuu na hata katika ajira.Hata hivyo bado kuna changamoto ya ufinyu wa watoto wa kike na wanawake kutumia fursa hizi kikamilifu zinazotolewa na serikali.
Awali kabla ya kumkaribisha Waziri Mhagama ,Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI Dk.Kadari Singo amesema program hiyo ambayo imezinduliwa leo inalenga kuwaanda viongozi wanawake chipukizi na kwa sasa wameanza na viongozi 50 na itafanyika kwa siku nne.Amefafanua kwa mujibu wa ratiba programu hiyo itafanyika kwa miaka minne na hivyo makadirio viongozi ya wanawake viongozi watakaonufaika na program hizo watafikia 200.
“Shida haya madarasa wapo ambao wanachukulia Serious na wengine hawako serious , unafundisha wengine wanacheza simu, wengine wanatoroka toroka, hivyo sisi tutawajenga walio tayari na siku moja huenda wakaingia kwenye kapo la Mama(Rais) kutokana na kuiva katika uongozi.
“Kwa kuepuka utoro ndio maana program hii inayoanza leo tumeamua wote ambao tutakuwa nao tumewatafutia eneo moja la kukaa na watafundishwa mambo mbalimbali ya uongozi,’amesema Singo na kuongeza fedha zinazotumika kwenye program hiyo zinatolewa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na nchi ya Finland.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...