Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Ruangwa
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametangaza mbele ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) pamoja na wanachama wa Chama hicho Mkoa wa Lindi kwamba jina lake litakuwepo kwenye Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2025.
Ametoa kauli hiyo mbele ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja wana CCM wa mkoa huo waliohudhuria majumuisho ya ziara ya Shaka mkoani Lindi kwa siku nne.
“Nataka kuwaambia Shaka ni kiongozi mkubwa, ni bosi wangu, huyu ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu, ni Katibu wa Itikadi na Uenezi mimi ni mbunge tu, huyu Shaka ndio mjumbe wa Sekretarieti inayochuja majina ya wagombea na mimi jina langu linapita pale.
“Hakuna masikio marefu zaidi ya wewe. Katibu wangu wa Itikadi na Uenezi nakupenda sana, nakuheshimu sana na jina langu litakuja 2025 na likija niangalie," amesema Waziri Mkuu ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Ruangwa.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amekubali ombi la Shaka aliyemuomba kumsaidia kupeleka mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mandawa. Ofisi hiyo ambayo imejengwa kwa nguvu za wana CCM wakishirikiana na Mbunge wao (Majaliwa).
Shaka alipokuwa katika Kata ya Mandawa wilayani Ruangwa, aliombwa na wana CCM kuona namna ambavyo anaweza kusaidia ujenzi wa ofisi hiyo ambapo aliahidi kusaidia mifuko 50 ya saruji, hivyo Waziri Mkuu ameahidi kutoa mifuko hiyo kwani hayo ni maelekezo ya Katibu wa Itikadi na Uenezi na lazima ayatekeleze.
Aidha, Waziri Mkuu amekubaliana na maombi ya Shaka ya kumpeleka Dar es Salaam mmoja ya wasanii wa mkoa huo ambaye ana uwezo mkubwa wa kuimba na sauti yake haina tofauti na aliyekuwa muimbaji mashuhuri wa Bendi ya TOT inayomilikiwa na chama hicho, Kapteni John Komba ambaye kwa sasa ni marehemu.
Shaka akiwa Lindi Mjini alipata nafasi ya kumshuhudia msanii huyo akiimba kwa sauti mithili ya Komba, na hivyo alitangaza kumchukua msanii huyo ili ampeleke TOT kuungana na wasanii wengine kuendeleza bendi hiyo.
Hivyo Shaka alipokutana na Waziri Mkuu alitoa ombi la kumsafirisha msanii huyo ombi ambalo Waziri Mkuu amesema atalitekeleza na ataondoka naye kwa ndege maalumu kutoka Lindi kwenda Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...