Na Said Mwishehe, Michuzi Tv-Kasulu
SHIRIKA la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limesema pamoja na shughuli ya kulisha wakimbizi kwenye kambi ya Nyarugusu pia limekuwa na miradi ya kuisaidia Tanzania hasa katika wilaya zinazopokea wakimbizi za Kasulu Mji na Kasulu DC mkoani Kigoma.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa WFP Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma Michael Bisama alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari waliopo kwenye Wilaya hiyo kwa lengo la kuangalia namna programu ya KGP (Kigoma Pamoja) ilivyofanikiwa kuwasaidia wakulima waliopo kwenye wilaya hiyo wanaojihusisha na kilimo hasa cha mahindi na maharage mekundu.
“WFP kwa Kasulu tuna kazi mbili kubwa, kazi ya kwanza ni kuwalisha wakimbizi walioko kwenye kambi ya Nyalugusu ambapo kuna Wakongo na Warundi.Kila mwezi takribani tani 23000 za chakula zinatumika na tunalisha wakimbizi wote bila kuchagua.
“Kazi ya pili tuna miradi ya kusaida Tanzania hasa katika wilaya ambazo zimepokea wakimbizi, Kasulu Mji na Kasulu DC .Kupitia KGP tuliamua kujikita katika kusaidia wakulima waliopo wilayani Kasulu , tunafahamu Kasulu wanalima sana ila tatizo ukihitaji hata tani zaidi ya tano huipati kokote .
“Wakulima wapo lakini ulimaji wao ni mdogo sana na mazao yao hayakuwa na viwango, na pale WFP tulipohitaji kununua tulishndwa,”amesema Bisama na kuongeza hivyo WFP iliamua kusaidia wakulima wadogo wanaoanzia ekari mbili hadi ekari tano, na lengo lilikuwa ni kuwanyanyua ili nao wawe wakubwa na wauze mazao ya kwa WFP.
“WFP ambacho tulikifanya ni kushirikiana na Serikali ya Wilaya ili kupata vikundi vya wakulima wadogo, hivyo kama KGP tukaanza kuwafundisha uvunaji bora, jinsi ya kuhifadhi na tukaenda nao mpaka tulipoona wameanza kuelewa kuhusu uvunaji, ukaushauji na uhifadhi.
“Baadae likaja swali wakulima wakishavuna wanaweka wapi? Hivyo WFP tuliamua kuyafanyia matengenezo maghala ili wakulima wawe na sehemu ya kuhifadhi mazao yao.Kwa Kasulu tumeyafanyia matengenezo maghala makubwa matatu.
“Maghala hayo yanatumiwa na wakulima walioko karibu na kambi za wakimbizi. Hayo maghala tumeshirikiana na Halmashauri kuyachagua na yapo kwenye maeneo ambayo wakulima wanazalisha.Pia WFP tukanunua vifaa vyote vinavyohitajika kwenye maghala,”amesema Bisama.
Akifafanua zaidi kuhusu WFP inavyowasaidia wakulima wa Kasulu Mji na Kasulu DC, Bisama amesema kupitia program ya KGP wakulima wa maharage na mahindi wamepata elimu ya namna bora kutunza mazao yao ili kuhakikisha yanakuwa kwenye viwango vinavyokubalika.Aidha amesema wakulima wengi walikuwa wanalima lakini hawakuwa ‘organize’, kuliwa na vikundi vingi na kila kimoja kilikuwa kinafanya kivyake.
“Hivyo WFP tuliamua kusaidiia vikundi ambavyo havikuwa vikisaidiwa.Tulichukua vikundi vichache tukavijingea uwezo na kisha wakajiunga kwenye AMCOS na kila kikundi kina wakulima kuanzia 37 na kuendelea”.
Kuhusu upatikanaji wa mazao Bisama amesema hapo awali kabla ya mradi ilikuwa ngumu kujua wakulima wanazalisha tani ngapi, hivyo kwa sasa kupitia program zilizopo wamesaidia wakulima kujua wanazalisha tani ngapi na wanajua ziko wapi? “Huko nyuma ilikuwa hata ukihitaji tani tano ya aina fulani ya mazao ilikuwa ngumu kuambiwa ziko wapi.Ukitaka ? Baada ya mradi huo kuja leo ukitaka mahindi unaambiwa nenda mahali fulani.
Kutokana na hali hiyo halmashauri wakaja na soko la wakulima hata wale ambao hawako kwenye mradi na nao mazao yao yananunuliwa.“WFP tunaamini kazi ya KGP sio kuwaaanda wakulima wawe wanauza mazao yao WFP peke yake , hapana kwa kuwa wamekuwa wakiwanganisha wakulima na wanunuzi wanawaunganisha na wanunuzi mbalimbali.Mkulima yuko huru kuuza mazao yake mahali kikote,”amesema.
Kupitia WFP, amesema mbali ya wakulima kupata soko la uhakika kuuza mazao yao lakini hata bei imeongezeka akitolea mfano msimu uliopita WFP imenunua kilo moja ya maharage Sh.1950 wakati wengine wananunua kilo moja Sh.1200 au Sh.1300.“WFP tumesaidia kuongeza thamani ya mazao ya wakulima.”
Akifafanua kuhusu matokeo chanya yaliyopatikana, amesema huko nyuma wakulima walikuwa wanauza mazao hovyo bila ubora na walikuwa wanakosa soko kwasababu ubora haukuwa mzuri, lakini baada ya mradi huo wamekuwa na soko la uhakika na wakati huo huo mazao yao yakiwa kwenye ubora unaotakiwa.Aidha amesema katka kuhifadhi mazao hawatumii tena dawa na badala yake wamekuwa wakitumia mifuko maalum ya kuhifadhi mazao ambayo hayaingii wadudu.
“Kwa hiyo watu wanahifadhi mazao yao hadi pale bei inapopanda.Zamani walikuwa wanauza kwa hasara kuogopa mazao yasiharibike”.Pia amesema WFP wamesadia kupeleka teknolojia ya kupukuchua mahindi, zamani walikuwa wanaweka kwenye magunia na kupiga mahindi lakini sasa hivi wanatumia mashine za kupukuchua mahindi ambayo imesaidia pia kupunguza muda.
Wakati huo huo amesema WFP wanaendelea kuwajengea uwezo wakulima ili wazalishe zaidi na pamoja na hayo hawajawabana wasiwauze watu wengine.“Maana leo WFP wapo na kesho wanaweza wasiwepo, Tunachotaka hata tukiondoka wakulima wawe na uwezo wa kuuzia watu wengine,”amesema Bisama na kusisitiza ndio maana mbali ya wao kununua mazao wamekuwa wakiwaunganisha wakulima na masoko.Kwa upandwa wakulima katika maeneo mbalimbali ya mradi wametumia nafasi hiyo kueleza kuwa kwa sasa wanalima kilimo chenye tija na wananufika nacho baada ya kupata mafunzo yaliyotolewa na WFP kwa kushirikiana na wadau wengine.
Wamesema wanajua jinsi gani wanatakiwa kuvuna, kutunza na kuuza mazao yao.
Wakati huo huo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma Dk.Sudi Kundelya amesema kupitia WFP wamekuwa wanufaika wakubwa sana wa miradi ya KGP.“WFP wamekuwa wakitusaidia kuendeleza wakulima na wafugaji wadogo wadogo,na tumepata mafanikio makubwa kutokana na miradi yao ambayo inaendelea , japo sasa hivi miradi ya KGP inakaribia mwishoni lakini tunajivunia mafanikio makubwa.Wamesaidia kuwajengea uwezo wakulima wetu.
“Kuna mabadiliko makubwa kwa wakulima wetu ukilinganisha na hapo awali hasa katika uvunaji na kutunza mazao yao baada ya kuvuna.Kwa bahati nzuri program hii ilihusisha maofisa ugani wetu hivyo tutaendelea kuwasaidia wakulima wetu,”amesema.

Wakulima wa mahindi wakimwaga mahindi yao kwenye turubai kabla ya kwenda kuyapukuchukua na kuyahifadhi

.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...