Na Said Mwishehe, Kibondo
SHIRIKA la Mpango wa Chakula Duniani(WFP) limesema limetumia Sh.bilioni 5.1 katika kusaidia maendeleo ya kilimo kwa wakulima wa Wilaya nne zilizopo kwenye mkoa huo.
Mkuu wa Ofisi Shirika la Mpango wa Chakula Duniani(WFP) Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma Said Johari amefafanua hatua kwa hatua namna wanavyotekeleza mradi huo na manufaa yaliyopatikana kwa wakulima tangu kuanza kwa mradi huo mwaka 2018 hadi mwaka huu wa 2022 wakati mradi unaelekea mwishoni.
“WFP Kibondo tunafanya kazi mbili, kwanza tunaangalia wakimbizi walioko Kambi ya Nduta ambako kuna wakimbizi 75000.Tunaangalia masuala yote ya chakula. Hilo ndilo jukumu letu kubwa .
“Pia ofisi ya Kibondo tunaangalia program ya Kigoma Pamoja ambayo tunaitekeleza kwa ushirikiano wa mashirika 16 kusaidia maendeleo ya Mkoa wa Kigoma,”amesema Johari.
Amefafanua WFP kwenye umoja huo wapo kwenye eneo la kilimo, wakiwa pamoja na FAO, ITC na UNCDF.Kwenye eneo la kilimo wanaangalia mnyonyoro wa thamani wa mazao matatu ya Mhogo, Mahindi na Maharage.
“Kwa hiyo kwenye kazi zile ambazo zinafanywa na theme ya kilimo ,FAO wao wanawezesha eneo la kanuni bora za kilimo, WFP tunaangalia upotevu wa mazao.
“ ITC wamejikita katika kuunganisha wakulima na masoko na UNCDF wanasaidia vikundi juuya fedha (financial inclusion). Kwa upande wa WFP tuna kazi kadhaa ambazo tumezifanya kwenye eneo hilo la kilimo husasan upotevu wa mazao,”amesema.
Ameongeza WFP kwa kushirikiana na halmashauri husika wamevitambua vikundi vya kufanya navyo kazi ambapo vipo 1,055.Pia wametoa mafunzo kwa wakulima kuhusu namna ya uhifadhi wa mazao na kuzuia upotevu wa mazao.
“Kwa ujumla tumefikia wakulima 24,316 tangu tulipoanza mradi mwaka 2018.Tumekarabati maghala matano ya kuhifadhi chakula na jumla ya fedha ambazo zimetumika ni Sh.milioni 137.
“Maghala mengi yalikuwa hayatumiki hivyo kwa suala zima la uhifadhi tuliona tukarabati maghala hayo.Pia tumetoa maturubai , vifaa vya kupimia unyevu wa mazao, tumetoa chaga za ambazo zinawekwa chini kabla ya kuweka chakula kutokana na mahitaji yao mbalimbali.
“Kwa ujumla vifaa ambavyo tumevitoa kwa wilaya zote tatu gharama yake ni Sh.milioni 137 na vifaa hivyo vimewekwa kwenye maghala, lakini tumewezesha mashine za kupuchukulia mahindi kwa halmashauri zote ambazo zina thamani ya Sh.milioni 84,”amesema.
Akifafanua zaidi kuhusu mradi huo amesema wamefanikiwa kuwaunganisha wakulima na wafanyabiashara mbalimbali kama sehemu ya kutafuta masoko,wamewaunganisha wakulima na wanaotengeneza vifaa.
“Kwasababu WFP hatawakuwepo kwenye kipindi chote, hivyo wameona ni vema wakawaunganisha na watengeneza vifaa hivyo vya kuhifadhia mazao. kuna wasambazaji 20 wanaotumika kuagiza mifuko kutoka kwa watengenezaji.
“WFP tumewezesha uanzishaji wa vyama vya ushirika 15 vya AMCOS katika halmashauri zote nne ambao ndio wanafanya uratibu katika masuala yote ya ukusanyaji wa mazao kwaajili ya soko la pamoja,”amesema .
Pia amesema katika kuwawezesha wakulima WFP sio soko la moja kwa moja lakini kutokana na uhitaji wa chakula nao walinunua mazao katika msimu wa 2019/2020.“Tulinunua maharage tani 366 ambapo wakulima walilipwa Sh.milioni 751.Tulinunua kilo moja ya kwa Sh.2,050.Msimu wa mwaka 2020/2021 tulinunua tani 1315 za maharage.Hivyo wakulima walipata Sh. bilioni Sh.2.5.
“Tulinunua kwa bei ya juu ukilinganisha na bei ya soko kwa wakati huo.Matokeo ya kazi ambazo tumezifanya katika mradi huo jukumu letu kubwa lilikuwa kuzuia upotevu wa mazao shambani yanapovunwa na wakati wa uhifadhi.
“Wakati tunaanza mradi upotevu ulikuwa asilimia 28 lakini hivi sasa upotevu umepungua ni asilimia 12.Aidha katika kufanya kazi kuna aina mbili tunazotumia,"amesema.
Amefanunua kuwa moja wanafanya kazi kwa kushirikisha kwa mashirika mengine yanayofanya kazi na WFP,hivyo walianza na Faida Mali na sasa wako na BRiTEN na kupitia washirika hao wametumia kiasi cha Sh.bilioni 4.
“Kazi ambazo zilifanywa moja kwa moja na WFP tumetumia Sh.milioni 596 lakini kwa kazi zote ambazo tumezifanya katika mradi huu ni zimetumika Sh.bilioni 5.1.
Mkuu wa Shirika la Mpango wa Chakula Dunianiuniani (WFP) Said Johari akifafanua jambo kwa waandishi wa habari alipokuwa akielezea hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Shirika hilo katika kuleta maendeleo kwa wakulima mkoani Kigoma
Sehemu ya magunia ya mazao ya maharage yakiwa yamehifadhiwa katika moja ya ghala kati ya matano yaliyokarabatiwa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) mkoani Kigoma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...