Meneja wa Tarura wilaya ya Tunduru Mhandisi Silvanus Ngonyani wa pili kushoto,akiwatembeza baadhi ya Waandishi wa Habari wa vyombo mbalimbali katika barabara ya lami ambayo imekamilika na kuanza kutumika katika mji wa Tunduru.



Barabara ya lami ya Ushirika-Hospitali ya wilaya iliyojengwa na Tarura katika mji wa Tunduru ambayo inatajwa imebadilisha kabisa muonekana wa mji huo na kuongeza thamani ya ya ardhi ambapo watu kutoka nje ya Tunduru na mkoa wa Ruvuma, wameanza kufika kwa wingi kwa ajili ya kuwekeza na kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi kufuatia kuwepo kwa miundombinu rafiki ya barabara hizo.

***************************

Na Muhidin Amri,
Tunduru

BAADHI ya wananchi wilayani Tunduru,wameiomba Serikali kuwadhibiti madereva wanaozidisha uzito wa magari kwani tabia hiyo inachangia kwa kiwango kikubwa kuharibu barabara zinazojengwa kwa fedha nyingi za serikali.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana walisema,kama madereva wataepuka kuzidisha uzito itawezesha kulinda na kuzifanya barabara zinazoendelea kujengwa kudumu kwa muda mrefu bila kuhitaji matengenezo ya mara kwa mara.

Abdala Kalanje mkazi wa mtaa wa Majengo alisema,licha ya serikali kujitahidi kujenga na kuboresha miundombinu ya barabara kwa kutumia fedha nyingi za walipa kodi,kama madereva wasipotaka kufuata na kuzingatia sheria kwa kutozidisha uzito kwenye magari wanayoendesha kuna hatari barabara hizo zinaweza kuharibika kwa muda mfupi.

Kalanje,ameuomba wakala wa barabara mijini na vijijini(Tarura),kusimamia kikamilifu miradi ya ujenzi wa barabara za lami na changarawe inazojenga na kuwachukulia hatua kali madereva na watumiaji wengine wenye nia ovu ya kuharibu kwa makusudi miundombinu hiyo.

Hassan Hausi, ameipongeza Tarura kwa kujenga barabara za lami katika mitaa mbalimbali ya mji wa Tunduru,hata hivyo ameshauri kuongeza alama zinazoonyesha kiwango cha uzito wa magari yanayopaswa kupita kwenye barabara hizo ili kuzuia uharibifu.

Aidha, ameiomba Halmashauri ya wilaya Tunduru kushirikiana na Tarura katika suala zima la kutunza miundombinu ya barabara na serikali za mitaa kuanza kutumia sheria zake ndogo kwa kuwachukulia hatua watu wote watakaobainika kuharibu barabara hizo ikiwamo kutupa uchafu kwenye mitaro.

Amewataka wananchi wenzake kutunza miundombinu hiyo kwani serikali inatumia fedha nyingi kwa ajili ya kurahisisha na kuunganisha mawasiliano kati ya sehemu moja na nyingine.

Alisema,ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha anakuwa mlinzi wa miradi inayoendelea kujengwa ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kuharakisha maendeleo katika wilaya hiyo na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake meneja wa Tarura wilaya ya Tunduru Mhandisi Silvanus Ngonyani alisema,dhamira ya serikali ya awamu ya sita kuendelea kujenga barabara hizo kwa kiwango cha lami katika mji wa Tunduru ili kuchochea ukuaji wa shughuli za uchumi na biashara kwa wananchi.

Alisema,mji wa Tunduru tangu upate uhuru mwaka 1961 hadi 2021 ulikuwa na mtandao wa barabara za lami zenye urefu wa km 1.2 tu,lakini tangu serikali ya awamu ya sita ilipoingia madarakani imeweza kutenga jumla ya Sh.bilioni 1.6.

Alisema,fedha hizo zimetumika kujenga barabara za lami zenye urefu wa km 3.16 na hadi sasa km 2 zimekamilika na km 1.2 zinaendelea kuwekewa tabaka la lami, ambapo ujenzi wa barabara hizo umefikia asilimia 90 na wanategemea kukamilisha kazi zote mwezi Agosti mwaka huu.

Aidha alisema,ili kuuweka mji wa Tunduru katika hali ya usafi katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 serikali imetenga Sh.milioni 900 ambazo zitatumika kujenga barabara nyingine za lami km 1.5.

Alisema, ujenzi wa barabara za lami katika Halmashauri hiyo ni mpango endelevu na wanategemea katika kipindi cha miaka 9 ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan angalau kuwe na km 15 za barabara za lami na hatimaye serikali ione uwezekano wa kuupandisha hadhi mji wa Tunduru kuwa Manispaa.

Kwa mujibu wa Ngonyani,moja ya vigezo vinavyotumika kupandisha hadhi kwenye Halmashauri za wilaya,miji na manispaa au majiji ni kuwepo kwa barabara nyingi za lami.

Aidha alisema,ujenzi wa barabara hizo unakwenda sambamba na uwekezaji wa taa za barabarani ili kuwawezesha wananchi kufanya shughuli zao muda wote na hata kusaidia kupunguza ajali za barabarani.

Amewataka wananchi kuhakikisha wanatunza barabara hizo kwa kufanya usafi na kuepuka kutupa uchafu kwenye mitaro ili ziweze kudumu kwa muda mrefu na kuleta tija inayokusudiwa na Serikali yetu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...