.jpeg)
* Bilioni 570 kunufaisha wanafunzi kupitia mikopo ya Elimu ya juu
* Serikali kutoa ufadhili kwa wanafunzi vinara masomo ya sayansi
SERIKALI ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kutekeleza kwa dhati uboreshaji wa sekta ya elimu na kuwekeza katika sekta ya hiyo ili kutoa wasomi wenye ujuzi wa kutoa matokeo bora kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Hayo yameelezwa leo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda wakati wa kikao maalum cha kueleza mwelekeo wa sekta ya elimu kwa mwaka wa fedha 2022/ 2023, vipaumbele na maeneo ya kimakakati katika utekelezaji na uboreshaji wa sekta ya elimu nchini kilichoikutanisha Wizara hiyo wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari.
Prof. Mkenda amesema, dhamira ya Serikali ni kuwa na elimu inayoandaa vijana watanzania vyema hasa katika ujuzi na katika kufanikisha hilo mambo muhimu yanayofanyiwa kazi kwa sasa ni pamoja na mapitio ya Sera ya Elimu na mafunzo ya mwaka 2014 pamoja na Sera ya Sayansi na Teknolojia ambapo Serikali imefungua milango kwa wadau na wanachi kutoa maoni kuhusu maboresho hayo.
Amesema, ubora na upatikaji wa elimu ni mambo muhimu ambayo Serikali imeweka dhamira ya dhati kwa kuweka mikakati na utekelezaji katika kuhakikisha elimu inayotolewa inakuwa bora na yenye viwango katika ujuzi kwa kuwapa wanafunzi maarifa faafu.
Akieleza hali ya upatikanaji wa elimu nchini Prof. Mkenda amesema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 Wizara imetengewa shilingi trilioni 1.49 na katika kuboresha elimu ya juu shilingi bilioni 570 zimetengwa kwa ajili ya mkopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na tayari dirisha la uombaji limefunguliwa na kuwataka wahitaji kufuata taratibu ili kunufaika na mkopo huo.
Vilevile amesema, tayari Benki ya NMB imetenga kiasi cha shilingi bilioni 200 kwa kuanzia mwaka wa fedha 2022/23 kwa ajili ya kuanza kutoa mikopo ya elimu ya ufundi na fedha hizo zitatolewa kwa utaratibu maalumu wa kibenki na kwa mujibu wa makubaliano rasmi kati ya Wizara na NMB ambapo itatolewa kwa riba nafuu ya asilimia 9 ili wanafunzi waweze kuendelea na masomo.
Aidha amesema, Serikali ya awamu ya sita katika kuboresha sekta ya Elimu nchini shilingi bilioni tatu zimetengwa kwa ajili ya ufadhili ‘Samia Schlarship’ kwa wanafunzi wa waliofaulu masomo ya sayansi vizuri zaidi katika mitihani yao kupitia Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA,) na kuendelea na masomo ya sayansi katika ngazi ya Elimu ya juu kwa kada za Sayansi, uhandisi na elimu tiba na Serikali itawasomesha bure katika vyuo vikuu mbalimbali nchini na itazidi kuongeza fedha ili kutoa fursa kwa vijana wengi watakaosoma masomo ya sayansi ndani na nje ya nchi.
Kuhusiana na elimu bila malipo Waziri Mkenda amesema baada ya Serikali kutangaza kuwa elimu ya darasa la kwanza hadi kidato cha sita kuwa bure bado wanapitia waraka wa michango shuleni na kusisitiza kuwa michango iwe hiari kama Serikali ilivyoelekeza.
Waziri Mkenda amesema, katika kuhakikisha ubora wa Elimu Aprili4, 2021 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akihutubia Bunge alielekeza mapitio ya sera na mitaala ili kuboresha elimu na upatikanaji wake wenye kuakisi ujuzi bora kwa wanafunzi.
Amesema, miongoni mwa mambo yanayoendelea ni pamoja na mapitio ya sera ya elimu ambapo kuna sera mbili zinazofanyiwa mapitio ikiwemo Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 pamoja na Sera ya Sayansi ya Sayansi na Teknolojia na kueleza kuwa Sheria ya elimu ni lazima iende sambamba na Sera na suala la mitaala lazima pia liendane na Sera.
Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF,) Bakari Machumu akizungumza katika kikao hicho na kueleza kuwa wanahabari wataendelea kuelimisha kutokana na umuhimu wa sekta ya Elimu katika maendeleo ya kijamii, uchumi na siasa, Leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH,) Dkt. Amos Nungu akizungumza katika kikao hicho na kueleza kuwa Serikali inafanya mambo mengi ambayo bila vyombo vya habari wananchi hawawezi kusikia jitihada hizo na kuahidi kukutana na waandishi wa habari mapema mwezi Agosti.
Baadhi ya Wahariri na viongozi wa Wizara wakifuatilia kikao hicho.
Mjadala ukiendelea.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...