Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha TLP, Augustino Mrema.

 

Na Thobias Mwanakatwe

MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha TLP, Augustino Mrema, amesema uteuzi na mabadiliko ya wakuu wa mikoa uliofanya na Rais  Samia Suluhu Hassan iwe chachu kwa walioteuliwa kufanya kazi kwa bidii kumsaidia Rais katika kuleta maendeleo makubwa ya kiuchumi nchini.

Akizungumza jana kwa simu akiwa jijini Dar es Salaam, alisema Rais anapofanya mabadiliko ya viongozi dhamira yake kuu ni kutaka kuona wasaidizi wake wanamsaidia katika kuleta maendeleo kwa wananchi.

Mrema ambaye ni mwanasiasa mkongwe ambaye amewahi kushika nyadhifa kadhaa ikiwano ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alisema Rais tuliyenaye anapenda kuona wasaidizi wake wanaleta mabadiliko ya kimaendeleo katika maeneo aliyowateua.

"Viongozi waliobahatika kuteuliwa cha msingi wakishaanza kutekeleza majukumu yao wachape kazi kuwaletea maendeleo wananchi maana dhamira ya Rais ni kuiona Tanzania inakuwa nchi yenye watu wake wenye maendeleo makubwa," alisema Mrema.

Mrema aliongeza kuwa mara nyingi watu wanapoteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi wanafurahia badala ya kwenda kufurahia wanapokuwa wamesaidia kuleta mabadiliko ya maendeleo kwenye eneo walilopangiwa.

Alisema walioachwa katika uteuzi huu hawana sababu ya kujisikia wanyonge kwani mchango wao walioutoa wakiwa viongozi unatambulika kwani uongozi ni kupokezana vijiti.

"Mimi nilikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani leo hii si niko benchi nafasi ameishika mwingine, na kwenye hizi kazi ukifanya vizuri utakumbukwa daima kwa uwajibikaji uliotukuka na heshima utakuwa nayo mbele ya jamii kama ilivyo kwangu mimi," alisema Mrema.

Mrema alisema moja ya majukumu ya Mkuu wa mkoa ni pamoja na kuhakikisha Mkoa  unakuwa na makusanyo ya mapato na kuzuia rushwa na upotevu wa mapato kwenye halmashauri zilizopo kwenye mkoa husika.

Aliongeza kuwa katika siku za karibu tumekuwa tukishuhudia katika ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) halmashauri nyingi zikikumbwa na kashfa ya ubadhirifu wa mapato na wakuu wa mikoa wapo lakini hawachukui hatua kwa watendaji wao wa chini.

Mrema alisema sio jambo lenye afya kiongozi wa kitaifa anapofanya ziara katika mikoa  na kuibua suala la ubadhirifu wa mapato wakati viongozi wa mikoa wapo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...