Rais Dkt Hussein Mwinyi amezindua tawi jipya la Benki ya CRDB na
kukabidhi pikipiki na boti za uvuvi na kilimo Ili kuwashirikisha
wananchi wengi kuujenga uchumi wa visiwa hivi.
Rais alikabidhi
jumla ya pikipiki 272 na boti 94 zitakazosaidia kuimarisha shughuli za
vijana na wanawake ambazo ni mkopo uliotolewa na Benki ya CRDB.
"Tuliahidi
sasa tunatekeleza. Mtakumbuka siku chache baada ya kuapishwa kuingia
madarakani niliziomba taasisi za fedha kushirikiana na Serikali
kufanikisha utekelezaji wa ahadi nilizozitoa kipindi cha kampeni za
uchaguzi mkuu. Benki ya CRDB imekuwa mstari wa mbele katika hili na leo
tumeanza na vijana pamoja na, wavuvi na wakulima wa mwani," amesema Rais
Mwinyi.
Dkt Mwinyi alizindua mikopo hiyo kwenye ufunguzi wa tawi la Benki ya
CRDB lililopo katika Mtaa wa Sunda, Barabara ya Mtemani akiwahimiza
wananchi kuzitumia huduma zake kufanikisha shughuli zao za kiuchumi.
"Tawi
hili linatoa huduma za benki kwa masharti ya Kiislam na yale ya
kawaida. Serikali kwa kushirikiana na wadau imedhamiria kuwawezesha
wananchi kiuchumi ndio maana inasogeza huduma zikiwamo za kifedha jirani
yenu. Kila mmoja aangalie fursa zilizopo kukuza uchumi wake,"
amesisitiza Rais huyo.
Alipozindua kampeni zake, Septemba 12
mwaka 2020 kwenye Uwanja wa Demokrasia uliopo Kibandamaiti Mjini Unguja,
Dkt Mwinyi aliahidi mambo kadhaa atakayoyafanya endapo atachaguliwa
kuiongoza SMZ ikiwamo kuimarisha uchumi wa bluu, kilimo na kuwawezesha
wananchi kwa mitaji.
Kati ya pikipiki 272 zilizokabidhiwa Jana, 222 zilitolewa kwa vijana wa
Mkoa wa Pemba Kaskazini na 50 kwa Pemba Kusini huku mkoa ukipata nusu ya
boti 94 zilizokuwapo ambazo 32 ni kwa ajili ya kilimo cha mwani, na 15
kwa ajili ya uvuvi.
Vilevile, Rais alikabidhi hundi za mkopo kwa
vikundi vitatu zenye thamani ya Sh273.8 milioni. Mikopo hiyo ilitolewa
kwa Chama cha Ushirika Shirikani (Sh210.8 milioni), Chama cha Ushirika
Umoja ni Nguvu (Sh58.8 milioni) na Chama cha Ushirika Mategemeo
kilichopokea Sh5 milioni.
Mapema Februari, SMZ iliingia
makubaliano na Benki ya CRDB kuwakopesha wananchi bila riba ikiikabidhi
benki hiyo Sh60 bilioni zitakazokuwa zikitolewa kila mwaka kwa kipindi
cha miaka mitano mfululizo.
Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB,
Abdulmajid Nsekela amesema kuanzia Januari mpaka Juni, wamekopesha
Sh23.5 bilioni kwenye matawi matatu yaliyokuwapo na anaamini wananchi
wa Wete sasa wanayo fursa ya kulitumia tawi hilo linalofanya jumla kuwa
manne visiwani hapa.
"Wananchi wanaweza kupata huduma zetu pia
kupitia makala 280, tulionao Unguja na Pemba. Mheshimiwa Rais ulitupa
changamoto ya kusogeza huduma kwa wananchi na leo tumefika Wete,"
amesema Nsekela.
Mkurugenzi huyo alisema wataendelea kushirikiana
na Serikali kufanikisha miradi ya maendeleo ukiwamo utekelezaji wa
program ya inuka na uchumi wa buluu inayolenga kuwawezesha wananchi
kunufaika na fursa zilizopo baharini.
Kwenye Sh60 bilioni
zilizotolewa na Serikali, Nsekela alisema tayari jumla ya Sh6.7 bilioni
zimekopeshwa kwa vikundi 607 vikiwamo 58 vya wilayani Wete. Vikundi
hivyo vyote, vina wanachama 11,806 wakijumuisha 689 wa Wete waliopokea Sh529.6 milioni.
Akizungumzia
umuhimu wa sekta binafsi katika kujenga uchumi, Waziri wa Fedha na
Mipango wa SMZ, Dkt Saada Mkuya alisema taasisi za fedha zinachangia
asilimia 3.4 kwenye pato la Taifa kwa mwaka.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela wakikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa Tawi la Benki ya CRDB lililopo Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Zanzibar leo Julai 25, 2022. Kushoto ni Mke wa Rais Mwinyi, Mama Mariam Mwinyi na kulia ni Waziri wa Fedha na Mipango wa Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya. Picha zote na Othman Michuzi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali
Mwinyi, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid
Nsekela wakifungua sehemu yenye jiwe la msingi wakati ufunguzi rasmi wa Tawi la Benki ya CRDB
lililopo Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Zanzibar leo Julai 25, 2022.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali
Mwinyi, akipata maelezo kutoka kwa Meneja wa Tawi la Wete, Dkt. Juma Sahimu, pindi alipotembelea tawi hilo wakati ufunguzi rasmi wa Tawi la Benki ya CRDB lililopo Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Zanzibar leo Julai 25, 2022.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali
Mwinyi, akihutubia muda mfupi baada ya kulifungua rasmi wa Tawi la Benki ya CRDB
lililopo Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Zanzibar leo Julai 25, 2022.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid
Nsekela, akizungumza ufunguzi rasmi wa Tawi la Benki ya CRDB lililopo Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Zanzibar leo Julai 25, 2022.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali
Mwinyi, akisalimiana na viongozi wa Benki ya CRDB, wakati alipowasili kwa ufunguzi rasmi wa Tawi la Benki ya CRDB lililopo Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Zanzibar leo Julai 25, 2022.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali
Mwinyi, akimkabidhi Mwenyekiti wa Waendesha Piki Piki Mkoa wa Kaskazini
Pemba (PENBRO), Mussa Haji Moja ya Pikipiki 272 zilizotolewa na Benki ya
CRDB kupitia katika Programu ya Inuka na Uchumi wa Buluu katika
ufunguzi wa tawi la benki hiyo lililopo Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba,
Zanzibar leo Julai 25, 2022. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya
CRDB, Abdulmajid Nsekela.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...