MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema kuwa kinachohitajika sasa ni mageuzi ya kweli, na siyo viraka vya mabadiliko kwa baadhi vipengele, katika Sekta ya Elimu Nchini.

 
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo, akiwasilisha maoni yake mbele ya Kikosi-Kazi cha Kuratibu Mageuzi ya Elimu Zanzibar,  kilichofika Ofisini kwake Migombani,  Jijini hapa.
 
Amesema suala la mageuzi katika Sekta ya Elimu ni la umuhimu wa pekee ili kuisogeza na kuivusha Nchi katika kuyafikia maendeleo ya kweli, ambapo dhamira hiyo itafikiwa kwa kutekeleza mabadiliko ya ujumla yatakayogusa wadau wote na wala siyo mapendekezo ya kupita.
 
Mheshimiwa Othman ameeleza kuwa, kuja kwa Kikosi-Kazi hicho sasa, ni mwangaza mpya wa kuelekea mageuzi ya kweli ya Sekta ya Elimu hapa Visiwani, na zaidi pale ambapo kimeonyesha dalili za kuwahusisha wadau wote, na kuwapa nafasi kupendekeza mabadiliko wanayoyahitaji.
 
“Mmeanza zoezi hili katika msingi mzuri, ambao moja kwa moja unaashiria mnakoelekea ni dira ya mageuzi ya kweli na wala siyo mabadiliko binafsi yanayohitajiwa na Wizara ya Elimu pekee”, ameeleza Mheshimiwa Othman.
 
Ametaja miongoni mwa maeneo yanayoguswa na changamoto nyingi katika Sekta ya Elimu hapa Nchini kuwa ni pamoja na Sera, hadhi na viwango vya ubora, na hasa ikizingatiwa kwamba hapakuwa na uwekezaji wa kutosha hapo kabla, uliolenga kuleta mageuzi ya kweli yaliyohusisha matakwa ya wadau wote, hali iliyoonekana kama ajenda ya kisiasa.
 
Mheshimiwa Othman ameongeza kwa kusema, “la muhimu ni kuanza kwa kuangaza pale ‘exactly’ tulipo na kujua tunapotaka kwenda, na lililo bora zaidi ni kuwahusisha kila wadau ili kukidhi mageuzi ya kweli katika sekta ya elimu hapa nchini”.
 
Akiwasilisha maoni yake kwa zaidi ya Dakika 90, Mheshimiwa Othman amegusia masuala ya tahmini, vigezo muhimu vya kitaaluma, uwezo wa wanafunzi na walimu, ubora wa wahitimu, mbinu za ufundishaji, hadhi na viwango vya taasisi za elimu ya juu, thamani na maslahi ya mwalimu na bajeti, mambo ambayo amesema Kikosi-Kazi hicho kinahitaji kuyazingatia kwa umakini, ili kufanikisha mageuzi yenye ufanisi katika Sekta ya Elimu.
 
Aidha, ametoa wito kwa Kikosi-Kazi kuzingatia mageuzi yaendayo sambamba na mabadiliko ya sasa duniani yanayojali ubora, viwango, ujuzi na ubunifu, huku akitilia-mkazo suala la umakini, nia ya dhati na uwajibikaji katika kutekeleza dhamira hiyo akisema, “hatuwezi kwenda na mazowea, iwapo tunahitaji kuleta mageuzi ya kweli katika sekta ya elimu na kwaajili ya maendeleo”.
 
Katika salamu zake, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mheshimiwa Ali Abdulghulam Hussein, amesema kuwa Kikosi-Kazi hicho kilichoteuliwa na kinachosimamiwa na Wizara yake ni hatua muhimu katika kuikuza na kuijenga Sekta hiyo ya Kijamii, na kwaajili ya maendeleo ya Taifa.
 
Naye, Mwenyekiti wa Kikosi-Kazi hicho, Profesa Idris Ahmad Rai, amefahamisha kuwa ‘Timu yake’ imekamilisha duru ya awali ya kuwafikia wadau wa elimu kwa upande wa kisiwa cha Unguja, na sasa inajiandaa kuelekea kisiwani Pemba kwaajili ya kukusanya maoni zaidi.
 
Kikosi-Kazi hicho, kinaundwa na wasomi na wanataaluma mbalimbali, wakiwemo Mawaziri Wastaafu na wabobezi kutoka Tasisi za Elimu ya Juu, Tanzania Bara na Zanzibar.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...