Balozi Agnes Kayola akizungumza wakati akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari juu ya mtangamano wa kikanda wa  Nchi wanachama za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC,) na fursa zinazopatikana  na kuwataka waandishi wa habari kueleza fursa zinazopatikana kupitia umoja huo ili wananchi wapate kunufaika, leo mjini Bagamoyo.

Balozi Mstaafu Dkt. Omar Maundi akizungumza wakati wa mafunzo hayo na kueleza kuwa umoja huo ni muhimu hasa katika masuala ya biashara ambayo ni huru wa nchi wanachama na kuwataka watanzania kutumia fursa hiyo ya kibiashara, Leo mjini Bagamoyo.

 

 SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema kuwa, itaendelea kushirikiana na makundi mbalimbali katika jamii vikiwemo vyombo vya habari ili kuhakikisha wanayafahamu malengo na mikakati ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) waweze kuibua fursa mbalimbali zilizopo katika nchi wanachama kwa lengo la kuwashirikisha Watanzania waweze kuzitumia kujiendeleza kiuchumi.

Hayo yameelezwa leo Julai 25, 2022 na Balozi Agnes Kayola wakati akimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine katika ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili kwa wanahabari mjini Bagamoyo mkoani Pwani yanayoratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ).
 

Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uelewa wanahabari kuhusu Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC,) na fursa zinazopatikana ili waweze kushiriki kikamilifu kutoa taarifa chanya ambazo zitakuwa na hamasa kwa Watanzania ili waweze kuzitambua fursa zilizopo katika jumuiya hiyo.

"Tanzania ni miongoni mwa nchi waanzishi wa SADC ambayo ina umri wa miaka 40. Waandishi wa habari mna mchango mkubwa kuhakikisha kundi la vijana linafahamu ipasavyo umuhimu wa SADC ili waweze kushiriki na kuzitumia fursa zilizopo katika jumuiya hii ya kikanda kwa manufaa,"amesema Balozi Kayola.

Amesema, licha ya fursa nyingi zilizopo katika nchi wanachama wa jumuiya hiyo, pia Tanzania inazo huduma nyingi ambazo zikitumika ipasavyo zitaweza kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa jamii na Taifa kwa ujumla.

"Pia kutokana na fursa zinazopatikana tutaendelea kutumia lugha yetu ya Kiswahili kama bidhaa, hivyo jukumu kubwa ambalo mnapaswa kulifahamu ni kuhakikisha mnakitumia Kiswahili ipasavyo katika kutoa taarifa zenu,"amesema.

Amefafanua kuwa, malengo ya SADC kama ilivyoelezwa katika Kifungu cha 5 cha Mkataba wa SADC (1992) ni kufikia maendeleo ya kiuchumi, amani na usalama, na ukuaji, kupunguza umaskini, kuimarisha kiwango na ubora wa maisha ya watu wa Kusini mwa Afrika.

Sambamba na kusaidia watu wasiojiweza kijamii kupitia Ushirikiano wa Kikanda. "Malengo haya yanapaswa kufikiwa kwa kuongezeka kwa Mtangamano wa Kikanda, unaojengwa kwa misingi ya kidemokrasia, na maendeleo yenye usawa na endelevu,"amesema.

Akieleza mikakati ya Wizara hiyo Balozi Kayola amesema kuwa, kupitia SADC wana mikakati mbalimbali ikiwemo kuwaenzi viongozi waanzilishi akiwemo Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

"Kwa kuzingatia hilo sanamu ya Mwalimu Nyerere itajengwa kwenye jengo la amani na usalama huko Addis Sababa nchini Ethiopia, mkakati huo unaendelea na itazinduliwamwaka 2023."Amesema.

Pia amesema, jukumu lingine walilonalo ni kuhamasisha jamii ya Watanzania waaweze kufahamu kuhusu majukumu, malengo na fursa zinazopatikana kwenye jumuiya ya SADC.

"Lengo lingine ni kuhamasisha umoja na ushirikiano katika nchi wanachama, kwa kulizingatia hilo Mheshimiwa Dkt.Jakaya Kikwete,Rais mstaafu waa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Jopo la Wazee wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), linaloshughulikia migogoro katika nchi wanachama wa jumuiya,"amesema Balozi Kayola.

Amesema, lengo lingine ni kutoa elimu kuhusu mtangamano wa jumuiya hiyo na ushiriki wa sekta ya habari katika kuhakikisha wanashiriki kikamilifu kufikisha taarifa chanya.

Awali Balozi Mindi Kasiga kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alieleza kuwa GIZ kwa kushirikiana na Wizara wameandaa na kutoa mafunzo hayo kwa kundi la wanahabari kwa manufaa ya Umma wa watanzania ambao watashirikishwa fursa zenye manufaa ya kiuchumi za SADC.

Balozi Mindi Kasiga akizungumza wakati wa mafunzo hayo na kueleza kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwajengea wanahabari uwezo ili watanzania waweze kunufaika na fursa kupitia SADC umoja ambao umejizatiti kuleta maaendeleo kwa wananchi, kujenga uchumi wa nchi pamoja na kuimarisha amani na usalama, Leo mjini Bagamoyo.


Mwezeshaji wa kikanda kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC,) kutoka Zambia Chibamba Kanyama akitoa mada katika mafunzo hayo na kuwahimiza wanahabari kuendelea kutumia vyema kalamu zao kuonesha fursa ili watanzania waweze kunufaika, Leo mjini Bagamoyo.






 Matukio katika picha wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika leo mjini Bagamoyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...