Benki
ya NMB ilikabidhi hundi yenye thamani ya 20m/- kwa Chuo cha Taifa cha
Utalii (NCT) ikiwa ni sehemu ya dhamira yake ya kusaidia kukuza uwezo wa
sekta ya utalii hapa nchini .
Msaada huo wa benki hiyo unaunga
mkono mkakati wa NCT unaolenga kuongeza ufanisi katika mnyororo wa
thamani wa sekta ya utalii kwa lengo la kuboresha huduma wa sekta hiyo.
Akizungumza
wakati wa hafla ya makabidhiano hayo iliyofanyika jijini Dar es Salaam,
Afisa Mkuu Rasilimali Watu wa Benki ya NMB, Emmanuel Akonaay alisema
benki hiyo imejipanga kuendelea kusaidia maendeleo ya Sekta ya Utalii na
imejidhatiti katika kutoa suluhisho la huduma za kifedha kwa kuwa na
mifumo bora zaidi ya ubadilishaji wa fedha na pia kuimarisha biashara ya
kadi ambayo itawezesha watalii kutohangaika wanapofanya manunuzi na
malipo mbalimbali.
Aidha, Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.
Pindi Chana wakati wa hafla hiyo aliishukuru benki hiyo na kubainisha
kuwa Serikali inalenga watalii Milioni tano ifikapo mwaka 2025 hivyo
msaada huo umekuja wakati muafaka huku Sekta hiyo inatoa fursa nyingi
katika sekta ya benki na fedha.
Lakini pia, Afisa Mtendaji Mkuu
wa NCT Dk.Shogo Mlozi alibainisha kuwa mpango wa mafunzo ya kimkakati
unalenga washiriki zaidi ya 5000 wakiwemo maofisa 700 wa uhamiaji na
wengine walioko kwenye mnyororo wa thamani wa Sekta ya Utalii kutoka
Mikoa inayojumuisha Dar es Salaam, Zanzibar, Arusha, Mwanza, Kilimanjaro
na Mara.
Afisa Mkuu wa Rasilimali Watu Benki ya NMB, Emmanuel Akonaay
(kushoto), akikambidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni 20 Waziri wa
Maliasili na Utalii, Mhe.Dkt. Pindi Chana (wa pili kushoto), kwa ajili
ya ufadhili wa mafunzo kwa wadau wa mnyororo wa thamani kwenye sekta ya
utalii. Kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utalii Tanzania (NCT),
Dk. Shogo Mlozi na wa pili kulia ni Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk.
Anna Makakala.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...