*Ni kauli ya msisitizo iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam akiwaambia wavamizi wa ardhi, asema kinachofuata hapo ni mazungumzo tu
Na MWANDISHI WETU
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Amos Makala amesema mvamizi yeyote wa ardhi ambaye hana karatasi au hati miliki ya ardhi hana haki na kuwa kinachofuata baada ya hapo ni mazungumzo tu.
“Bila karatasi wala hati huna haki, kinachofuata baada ya hapo ni mazungumzo tu kwani mvamizi ni sawa na mhalifu,” alisema Mhe. Makala wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Mabwepande Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Mhe. Makala alisema mvamizi yeyote ni sawa na mhalifu na kwamba mbele ya Sheria makosa hayo ya uvamizi wa ardhi ni sawa na kosa la jinai hivyo mtu anapoelekezwa kuwa makosa yamefanyika na anatakiwa awe mwepesi wa kuunga mkono na kurekebisha makosa kwani wakiendelea na ubishi hautawasaidia.
“Nimekuja na watu wa NSSF lile eneo lao wanapima viwanja na nimewaambia wapime viwanja rafiki ili watu wa Mabwepande nao waweze kupata,” alisema.
Alisema wameanza kupima katika eneo la NSSF na baadaye wataenda katika eneo la DDC na eneo la Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ambayo yamevamiwa pamoja na taasisi nyingine zote ambazo zimevamiwa.
Mhe. Makala alizitaka taasisi zote ambazo zinamiliki maeneo katika Kata hiyo ya Mabwepande kutenga maeneo kwa ajili ya huduma mbalimbali za jamii kama ambavyo NSSF walishafanya kwa kutoa eneo kwa ajili ya kujenga shule.
Naye, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Mhe. Songoro Mnyonge aliupongeza Mfuko wa NSSF kwa kukubali kupanga upya eneo lao na pia kutoa eneo ambalo litajengwa Shule.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Godwi Gondwe alisema katika eneo la NSSF limeshapimwa na limeshawekwa alama jambo ambalo litaondosha uvamizi wa ardhi katika eneo hilo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...