
TANZANIA imeungana na Mataifa mengine Barani Afrika kuadhimisha siku ya Usajili wa matukio muhimu ya Binadamu na Takwimu, ambayo ni Vizazi,Vifo na sababu zake, ndoa, talaka na watoto wa kuasili.
Ikiwa ni maadhimisho ya tano kufanyika Kwa upande wa Tanzania kiwango Cha Usajili kimepanda kupitia mpango wa Usajili na kuwapatia vyeti vya kuzaliwa Watoto wa Umri chini ya Miaka Mitano ambapo hadi sasa unatekelezwa katika Mikoa 23 na kuonesha mafanikio ya zaidi ya watoto Milioni 7.7 wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa bila ya malipo ya ada na hivyo kuongeza asilimia ya watoto waliosajiliwa nchini kufika 65 kutoka asilimia 13 ya mwaka 2012.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro wakati wa maadhimisho hayo yaliyofanyika leo tarehe 10 Agasti,2022 katika Kata ya Gongolamboto jijini Dar es Salaam na kwenda sambamba na kauli mbiu ya "Kuimarisha Uratibu, Uongozi, Uwajibikaji wa Kitaifa na mifumo jumuishi ya Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu na Takwimu: Nyenzo Muhimu katika Kumhesabu kila Mmoja."
Mhe. Dkt Ndumbaro amesema, Wizara yake kupitia Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA,) wanaendelea kutekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha ifikapo 2025 watoto wote walio na umri wa chini ya miaka 5 wanasajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa huku akiielekeza RITA kukamilisha asilimia 35 iliyobaki ndani ya mwaka mmoja ili kila mtoto aliyechini ya umri wa miaka 5 anapata cheti cha kuzaliwa na ifikapo 2030 watoto wote wawe na vyeti vya kuzaliwa.
Ameongeza kuwa, kufikia Januari mwaka ujao watoto wote watasajiliwa pindi wanapozaliwa na kutilia mkazo mkakati wa watoto wanaoanza shule kuwa na vyeti vya kuzaliwa na wasio navyo kupata Usajili pindi wanapoanza masomo yao, pia litawajumuisha wanafunzi wa Sekondari na vyuo ambao usajili wa Taasisi zao za elimu utakwenda sambamba na vyeti vya kuzaliwa.
Hata hivyo amewataka viongozi wa Serikali ya mitaa na Kata kufuatilia na kuhamasisha zoezi la usajili ili kujua matukio katika maeneo yao yanaongezeka kwa namna gani na wazazi na walezi kuwapa haki hiyo ya msingi watoto wao.
Pia ameipongeza RITA kwa kushirikiana na wadau mbali kwa kasi ya usajili na utoaji vyeti vya kuzaliwa kwa wananchi kupitia programu bunifu za Usajili zinazoendelea nchi nzima na kusisitiza hivi Sasa RITA ipo Kidigitali hivyo Wananchi wachangamkie kupata huduma kisasa zaidi.
Kwa upande wake Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA Bi. Angela Anatory amesema maadhimisho hayo ya tano ya siku ya Usajili wa Matukio muhimu ya Binadamu na Takwimu Barani Afrika imelenga kujenga ufahamu kwa wananchi juu ya kumbukumbu muhimu pamoja na matukio muhimu ya vizazi, vifo, talaka, ndoa pamoja na kuasili watoto.
Amesema, RITA ikiwa taasisi pekee inayosimamia matukio ya Usajili wamekuwa wanatekeleza usajili wa matukio hayo pamoja na kubuni programu za maboresho ya kuongeza kasi na kupanua wigo wa utoaji huduma.
Bi. Angela amesema katika mpango wa Usajili na utoaji vyeti vya kuzaliwa bila malipo kwa watoto walio chini ya miaka mitano Wakala hiyo inaendelea kutoa huduma hiyo kwa kusogeza huduma hiyo karibu na makazi ya wananchi kupitia ofisi za watendaji wa Kata na vituo vya tiba vya afya ya Mama na mtoto.
" Kwa mwaka mmoja tangu kuadhimishwa kwa siku hii tumeweza kufikia Mikoa 3 ya ziada ya Katavi, Rukwa na Tabora na jumla ya watoto laki nne na sitini wamesajiliwa na kupatiwa vyeti." Amesema na hapa katika Viwanja hivi tunasajili na tayari tumeshatoa vyeti vya kuzaliwa Kwa Wananchi zaidi ya 600".Alisema Bi.Anatory.
Aidha amesema, mpango huo utaendelea katika mikoa ya Kagera na Kigoma pamoja na kutatua changamoto zilizopata huduma katika mikoa ya awali.
Bi. Angela amesema, mpango wa wa kusajili watoto wa miaka 5 hadi 17 walio shuleni unaendelea kwa kushirikiana na Halmashauri.
"Kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu kufanyika kwa maadhimisho haya Wilaya 7 zimefikiwa na wanafunzi laki moja na nusu wamesajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa na kufanya idadi za Wilaya 28 kufikiwa na wanafunzi laki tano, sitini na nne elfu na mia moja na sabini na moja kusajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa." Amesema.
Amesema Wakala itaendelea kuboresha mifumo ya TEHAMA ili kurahisisha utoaji wa huduma ikiwemo kuweka mfumo wa Ndoa utakaowawezesha kutoa leseni kwa wafungisha ndoa pamoja na kupata takwimu za kitengo hicho
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi mkaazi wa UNICE Bw. Ousmane Niang ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuwafikia watoto kuwasajili na kuwapa vyeti katika mikoa 23 ya Tanzania na ni mfano mkubwa wa kuigwa kwa nchi nyingine Afrika.
Amesema wataendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania na wadau mbalimbali katika kuhakikisha watoto wote wanasajiliwa na kupewa vyeti pamoja na kuchukua kumbukumbu ya matukio yote muhimu ikiwemo vizazi, na vifo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Serikali ya Canada Bi. Helen Fytche amesema kila mwananchi ana haki ya kusajiliwa na kupata cheti cha kuzaliwa na hivyo Serikali yake itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma hiyo.
Naye mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani (UNFPA ,) Ramadhan Hangwa amesema wamekuwa wakiboresha mifumo ya kupata cheti cha kuzaliwa kutoka miezi miwili hadi saa 24 na Zanzibar inatekeleza hilo.
Amesema, wadau waende sambamba na uboreshaji wa Usajili na ukusanyaji wa matukio ya binadamu ili kwenda sambamba na kasi ya maendeleo ulimwenguni.
Kwa upande wake Mbunge wa Ukonga Mhe. Jerry Slaa amesema suala la mirathi liangaliwe ili kuokoa familia hasa akina Mama na watoto na kuwataka wananchi wa Ukonga kujitokeza kwa wingi siku ya Agosti 23 ili wahesabiwe kwa maendeleo endelevu.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na wadau mbalimbali zikiwemo Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma TAMISEMI wadau wa Maendeleo Shirika la kuhudumia Watoto Duniani UNICEF, Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani (UNFPA ,) Shirika la Maendeleo la Canada, Ubalozi wa Italia, Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA), Ofisi ya Taifa ya Takwimu( NBS), Kampuni ya mawasiliano ya Tigo Tanzania na Wizara mbalimbali ambao wamewataka wananchi kushiriki katika zoezi la Sensa litakalofanyika Agosti 23 mwaka huu kwa kujitokeza kuhesabiwa ili Serikali iweze kupanga mipango yake ya maendeleo.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Ludigija Ngw'ilabuzu akizungumza wakati wa maadhimisho hayo na kuwataka wananchi kushiriki katika zoezi la Sensa litakalofanyika Agosti 23 mwaka
huu kwa kujitokeza kuhesabiwa ili Serikali iweze kupanga mipango yake
ya maendeleo.
Naibu Mkurugenzi mkaazi wa UNICE Bw. Ousmane Niang akizungumza wakati wa maadhimsho hayo ambapo ameipongeza Serikali
ya Tanzania kwa kuwafikia watoto kuwasajili na kuwapa vyeti katika mikoa
23 ya Tanzania na ni mfano mkubwa wa kuigwa kwa nchi nyingine Afrika.
Baadhi ya wadau wakitoa salamu katika maadhimisho hayo.

Wananchi wakipata huduma ya usajili na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa.
Matukio mbalimbali wakati wa hafla hiyo.(Picha na Emmanuel Massaka wa Michuzi Tv.)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...