Na Mwandishi Wetu, Mbeya
MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko Bw. Bernard Konga amesema kuwa utaratibu wa kutumia kadi ya bima ya afya ni utaratibu mzuri ambao umethibitika Kitaifa na Kimataifa katika kujihakikishia upatikanaji wa huduma za matibabu zinapohitajika.

Hayo ameyasema katika Maonesho ya Nane Nane yanayofanyika katika viwanja vya John Mwakangale mkoani Mbeya wakati akizungumza na wananchi waliotembelea banda la Mfuko.

"Utaratibu wa wananchi kuwa katika utaratibu wa bima ya Afya ndio utaratibu wa kisasa zaidi ambao umethibitika hivyo ni wakati muafaka kwa wananchi kujiunga na huduma zetu ili kujihakikishia huduma wakati wowote" alisema Bw. Konga.

Alisema kuwa Mfuko umekuwa ukishiriki katika maonesho yote ya Kitaifa kwa lengo la kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kujiunga na huduma za Mfuko kwa kuwa ndio suluhisho pekee katika kupata huduma za matibabu.

“Katika maonesho haya pia tumefanikiwa kutoa huduma ya upimaji afya ambayo kwetu tunaichukulia kama kinga, mwananchi anapojua hali ya afya yake inamsaidia zaidi kujikinga na kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza hivyo niwaombe sana wananchi kutumia fursa hizi zinapojitokeza,” alisema Bw.Konga.

Alieleza kuwa Mfuko umekuwa na mafanikio makubwa hususan katika kupaunua wigo wa wanachama wake ambapo kwa sasa kila mwananchi anayo fursa ya kujiunga na huduma zake tofauti na hapo awali ambapo Watumishi wa Umma tu ndio walikuwa na fursa hiyo.

Akizungumzia suala la Bima ya Afya kwa wote, alisema kuwa suala hilo ni mkombozi mkubwa kwa watanzania na kutokana na umuhimu huo Rais Samia Suluhu Hassan amelipa kipaumbele ili liweze kurahisisha upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wananchi.

“Bima ya Afya kwa wote itasaidia kwa kiwango kikubwa kuimarisha huduma za matibabu nchini na mfano mzuri tunauona sasa ambapo zaidi ya asilimia 75 ya mapato ya vituo yanatokana na bima ya afya hivyo wananchi wengi zaidi wakijiunga huduma zitakuwa bora zaidi na kila mwananchi atapata huduma bora zaidi,” alisema Bw. Konga.

Naye Shehe wa Mkoa wa Mbeya Bw. Usafiri Mjalambaha amewataka wananchi kuwa na maandalizi ya kupambana na magonjwa kwa kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ili maradhi yanapojitokeza waweze kupata huduma za matibabu bila kikwazo cha fedha.

“Wananchi ni wakati mzuri sasa wa kujiandaa kwa kuwa na kadi ya NHIF kwani sote tunajua maradhi huja bila taarifa na yanapokuja yanahitaji fedha nyingi ya kuyatibia hivyo ni vyema yakakukuta na kadi ya bima ya afya ambayo itakutibu bila kulazimika kutafuta fedha zingine au kuuza mali za familia,” alisema Shehe wa Mkoa.

Alitumia nafasi hiyo pia kuwaomba Waislamu wote nchini kutumia fursa hii kwani haina madhara yoyote katika dini ya kiislam bali ina faida kubwa ya kujikinga au kuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu wakati wowote.

“Huduma za NHIF zina manufaa makubwa sana hivyo niahidi tu kuwa nitakuwa balozi mzuri wa kutoa elimu hii ambayo nimeipata hapa ili kila mwananchi aone faida zake na achukue hatua ya kujiunga,” alisisitiza.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Bernard Konga akiwahudumia wananchi katika maonesho ya Kilimo Kitaifa 2022  Nane Nane yanayoendelea viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.


Wananchi wakipata huduma kwenye Banda la NHIF katika maonesho ya Kilimo Kitaifa 2022 Nane Nane yanayoendelea viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...