Stanley Mbaga Afisa Udahili akiwapa vipeperushi Wanafunzi wa Shule ya sekondari Nyasa lake shore ya Kyela walipotembelea maonesho ya 29 ya Sikukuu ya Wakulima (Nane Nane) yanayofanyika mkoani Mbeya katika viwanja vya John Mwakangale.
Rufina Khumbe mhadhiri Msaidizi Ustawi wa Jamii na Mratibu wa Kituo cha Elimu, Ushauri na Msaada wa Kisaikolojia akizungumza na wananchi wa katika maonesho ya 29 ya Sikukuu ya Wakulima (Nane Nane) yanayofanyika mkoani Mbeya katika viwanja vya John Mwakangale.
Itika ngwakwa mhadhiri msaidizi Ustawi wa jamii akizungumza na mwananchi alipotembele katika maonesho ya 29 ya Sikukuu ya Wakulima (Nane Nane) yanayofanyika mkoani Mbeya katika viwanja vya John Mwakangale
Stanley Mbaga Afisa Udahili akiongea na Wanafunzi wa Shule ya sekondari Nyasa lake shore ya Kyela Mbeya katika maonesho ya 29 ya Sikukuu ya Wakulima (Nane Nane) yanayofanyika mkoani Mbeya katika viwanja vya John Mwakangale.

Na Mwandishi Wetu
TAASISI ya Ustawi wa Jamii (ISW) iliyoko chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imeeleza umuhimu wa wakulima na jamii kwa ujumla kupata elimu ya kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi.

Akieleza hayo katika maonesho ya 29 ya Sikukuu ya Wakulima (Nane Nane) yanayofanyika mkoani Mbeya katika viwanja vya John Mwakangale, Mhadhiri na mratibu wa kituo cha Elimu, Ushauri na Msaada wa Kisaikolojia katika Taasisi hiyo, Rufina Khumbe, amesema wanatoa ushauri kwa wakulima kujiandaa na matokeo chanya au hasi kulingana na mabadiliko ya tabia nchi yanayoweza kuleta majanga.

“Wanaweza kutokea wadudu au mvua zisizotosheleza, kwa hiyo sisi tunatoa elimu na ushauri wapi watapata msaada endapo matatizo kama hayo yatajitokeza na tunawaelekeza namna ya kukubaliana na kuendana na matukio kama hayo.

Kwa upande mwingine unakuta mtu alichukua mkopo lakini anashindwa kufanya marejesho kama inavyotakiwa sasa akishindwa kumudu hali hiyo anaweza kuchukua maamuzi magumu asipopata mtu wa kuzungumza naye. Kwa hiyo ni jukumu letu kutoa elimu na ushauri ili jamii iweze kujikinga na au kukabiliana na matatizo yanayoweza kujitokeza”.

Aidha mhadhiri huyo ameeleza umuhimu wa kuwa na jamii shirikishi ambayo ina uwezo wa kupunguza changamoto zilizopo na kupunguza matatizo ya saikolojia na msongo wa mawazo.

“Jamii iboreshe mawasiliano kwa maana ya kuzungumza na kuibua changamoto baina yao katika jamii husika na kuona namna ya kuzitatua. Mahusiano ni muhimu sana katika ngazi ya familia. Kama wanafamilia hawataweza kuzigeuza changamoto na rasilimali walizonazo kuwa fursa ni dhahiri kwamba migogozo itajitokeza katika familia husika“ amesema Bi. Rufina na kuongeza:

"Shida kubwa ni familia kutokuwa na mawasiliano au kuzungumza. Mfano katika suala la uchumi ambapo wana ndoa wanaweza kukaa chini na kuzungumza na kuweka bayana kipato chao ambapo familia ingeweza kuona namna sahihi ya kutumia kipato kinachopatikana kwa ajili ya kujikimu kimaisha na kusonga mbele".

Wakati huo huo, Itika Ngwaka, Mhadhiri Msaidizi ambaye anafundisha masuala ya ustawi wa jamii amesema wameshiriki katika maonesho hayo kwasababu Wizara ina mpango wa kuboresha maisha ya Watanzania hususan kwenye eneo la kilimo (kilimo na ufugaji) na kufikia ajenda ya kukuza kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.

“Kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na maafisa ustawi wa jamii katika maeneo ya shughuli za kilimo kuisaidia jamii kuwa na familia zenye utulivu, kuepuka migogoro na kuwa na utulivu wa afya ya akili ili kuwawezesha kujikita katika kilimo hai na kujiandaa kisaikolojia kuweza kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na majanga yanayoweza kujitokeza kama ukame, wadudu waharibifu, na mafuriko. Sambamba na hilo ni kuiwezesha jamii kutambua wadau wa kilimo na fursa zilizopo ili ijikite kwenye kilimo hai na kufikia malengo.

Kwa muktadha huo pia tunahitaji watoto wa wakulima kujiunga na masomo ya elimu ya juu ili wakirudi katika kaya zao waweze kuboresha na kuendeleza shughuli za kilimo”.

Ametolea mfano wa kozi ya Menejimenti ya Rasilimali Watu ambapo mtoto mmoja akiwa mtaalamu kwenye eneo hilo anaweza kushauri namna ambavyo wanaweza kutumia rasilimali watu na vitu walivyo navyo kuboresha maisha yao ya kila siku".

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...