Kamisaa wa zoezi la Sensa na makazi ya watu ya mwaka 2022 ambaye pia ni Spika Mstaafu wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda akizungumza leo Agosti 3,2022 Kibaha mkoani Pwani.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge akizungumza leo Agosti 3, 2022 alipokuwa akizindua zoezi la Sensa lililofanyika Wilayani Kibaha katika Kongamano la Viongozi wa Dini la kuhamasisha sensa ya watu na makazi

Na Khadija Kalili, Kibaha
KAMISAA wa zoezi la Sensa na makazi ya watu ya mwaka 2022 ambaye pia ni Spika Mstaafu wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda amewataka wakazi wa Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani na Tanzania nzima kwa ujumla kutoa ushirikiano kwa Makarani wa Sensa kwa kujibu maswali ipasavyo.

"Natoa wito kwa wakazi wa maeneo yote pindi Makarani watakapopita majumbani mwao kutoa taarifa sahihi."

Anne Makinda amesema hayo leo Agosti 3, 2022 alipokuwa akizindua zoezi la Sensa lililofanyika Wilayani Kibaha katika Kongamano la Viongozi wa Dini la kuhamasisha sensa ya watu na makazi iliyofanyika Wilayani Kibaha Mkoani Pwani.

Kamisaa huyo wa Sensa ndiye alikua mgeni rasmi kwenye Kongamano hilo lililofanyika kwenye viwanja vya Halmashauri ya Mji Kibaha.

Amewataka Watanzania wote kushiriki kikamilifu kwenye zoezi la Sensa ya watu na makazi itakayofanyika Agosti 23 mwaka huu kwa kutoa taarifa sahihi kwa makarani huku akiwatoa hofu kwamba taarifa zao zitabaki kuwa Siri.

"Serikali inahitaji kupata idadi ya watu huku lengo likiwa ni kuimarisha huduma za kijamii kwa urahisi na kwa kizingatia idadi ya watu" amesema Kamisaa Anne Makinda.

Kupatikana kwa taarifa sahihi za idadi ya watu na makazi, ikiwemo watu wenye ulemavu, wajane taarifa zote hizi ni muhimu na zitasaidia katika kuimarika kwa huduma muhimu za kijamii" amesema Anne Makinda.

Anne amesema kuwa jamii isiwafiche watu wenye ulemavu ili idadi yao iweze kujulikana na aina ya ulemavu wao ili kuweza kutengeneza mazingira ya kuimarisha huduma muhimu kwa watu wenye ulemavu kwa ujumla.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge amesema kuwa Mkoa wa Pwani tayari umefanya maandalizi ya kutosha ikiwemo utoaji wa elimu na kutenga maeneo muhimu kwa ajili ya zoezi hilo la Sensa ya watu na makazi, hivyo kupitia Kongamano hilo amewaomba viongozi wa dini kuendelea kuhamasisha Sensa kwa waumini wao huku pia akieleza mikakati mbalimbali ya kuhamasisha wananchi kushiriki Sensa na ametoa tahadhari dhidi ya UVIKO 19 kuwa bado upo huku akiwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari.

Kongamano hilo limeandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Sara Msafiri wakati huo huo akazungumzia Kongamano hilo amesema kuwa ni matokeo ya mikakati ya Kamati ya Amani ya Viongozi wa dini kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha wananchi kushiriki Sensa ambapo viongozi hao wametambua umuhimu wa Sensa na wamejitolea kuhamasisha jamii kwa kupitia nyumba zao za ibada ikiwemo Misikiti na Makanisani pamoja na madhehebu mengine ya dini.

DC Sara alitoa shukrani kwa wadhamini wa Kongamano hilo ambao ni Benki ya CRDB, NMB na OSHA.

DC Sara amewashukuru viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na Viongozi ambao kwa upande dini ya Kiislam walioongozwa na Shekh wa Mkoa wa Pwani Hamisi Abbas Mtupa aliyemwakilisha Mufti wa Tanzania na Father Beno Kikudo aliyemwakilisha Askofu Mkuu wa Kanisa la Kilutheri Tanzania Askofu Malasusa.

Sheikh Mtupa amesema kuwa Sensa ni suala ambalo limeelekezwa katika mafundisho ya dini hivyo amewataka waumini kushiriki ipasavyo.

Wakati huohuo DC Sara amesema kuwa wamefanya mazungumzo na mabasi ya Usafirishaji UDART yanayokwenda na kurudi Kimara Kibaha kuwa watakuwa wanazicheza nyimbo za hamasa yakushiriki Sensa wakati wakiwa wakitoa huduma kwa wananchi.

"Tumeshafanya mazungumzo na Uongozi wa UDART wanaotoa huduma ya usafiri kutoa matangazo hayo pia nyimbo za hamasa katika sehemu za Masoko, stendi za mabasi na maeneo mbalimbali yenye mikusanyiko wa watu". amesema DC Sara.

Zoezi la sensa hufanyika kila baada ya miaka kumi nchini kote.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...