Ofisa Mtendaji Mkuu wa NICOL Investment PLC, Erasto Ngamilaga
Mwenyekiti wa Bodi ya NICOL Investment PLC, Dk. Gideon Kaunda

Kampuni ya NICOL yazidi kupaa
* Hisa zake DSE hazikamatiki

Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya NICOL Investment (PLC), imeendelea kupata faida na hisa zake kuendelea kufanya vizuri katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

Kwa mujibu wa hesabu zilizokaguliwa za Kampuni hiyo, faida ya Kampuni hiyo imepanda kutoka shilingi bilioni 1.5 mwaka 2020 mpaka bilioni nne mwaka 2021.

Hisa za Kampuni hiyo kwenye soko la hisa nazo zimeonekana kuendelea kupanda kwa kasi kutoka shilingi 200 mwaka 2020 hadi shilingi 360 mwaka huu.

Akizungumzia siri ya mafanikio hayo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa NICOL, Erasto Ngamilaga, alisema ni kweli mapato ya kampuni hiyo ya kizalendo yanaendelea kupaa kwa kasi.

Alisema wakati kampuni hiyo inasajiliwa kwenye soko la hisa la Dar es Salaam mwaka 2018 ilikuwa na changamoto nyingi sana lakini kwa sasa mambo yako safi na wanahisa wanafurahia kampuni yao kuendelea kufanya vizuri huku wakilipwa magawio na kupata taarifa za kampuni kwa uwazi.

Alitaja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni kampuni kufanya mikutano ya kila mwaka na kwa mfululizo kuanzia mwaka 2018 wanahisa kuendelea kupata gawio la faida mfululizo.

Ngamilaga alisema hivi karibuni walitangaza hesabu zilizokaguliwa zinazoonyesha kuwa faida ya kampuni hiyo imekua kutoka Sh bilioni 1.5 mwaka 2020 hadi bilioni 4 mwaka 2021

Alisema hilo ni sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 144 na kwamba mafanikio hayo yamechangiwa na mapato wanayopata kutoka kwenye magawio na mapato yanayotokana na riba baada ya kufanya uwekezaji kwenye hati fungani.

“Mafanikio haya yamekuja kutokana na jitihada za makusudi tunazoendelea kuzifanya katika kipindi cha kuanzia mwaka 2018 hadi sasa na kuendelea, hayo yamewezekana baada kuchukua juhudi za kutawanya uwekezaji wetu kwenye maeneo yenye faida kubwa has kwenye hati fungani,” alisema

Alisema wanaendelea na jitihada za kutawanya uwekezaji wa kampuni ili kuufanya uwianne na malengo ambayo kampuni imejiwekea kwa kuzingatia mkakati wa kukuza mapato na faida kwa manufaa ya Wanahisa wake.

Alisema hivi karibuni ulifanyika mkutano wa dharula wa Wanahisa ili kuthibitisha uchaguzi wa Wakurugenzi wapya wa kampuni, ambapo wanahisa walithibitisha na kuteua wakurugenzi wapya.

“Tumefanikiwa kujaza nafasi kwa mujibu wa maazimio ya Wanahisa yaliyofikiwa katika mkutano mkuu wa saba, ni matumaini ya Wanahisa kwamba Wakurugenzi walioteuliwa wataongeza chachu ya maendeleo ya kampuni pamoja na kukidhi matakwa ya sheria katika uendeshaji bora wa makampuni unaoziingatia weledi,” alisema.

Mtendaji huyo alisema yapo maeneo mengine makubwa ya kimkakati ambayo kampuni inaendelea kuwekeza mbali na kuhakikisha kwamba mapato yanayopatikana kwenye gawio na hati fungani yanarejeshwa katika uwekezaji mwingine.

Alisema NICOL inatathmini kuingia kwenye uwekezaji wa viwanda na maeneo mengine, tunaendelea kufanya tathmini ya kufanya uwekezaji katika maeneo mengine kama vile uwekezaji katika sekta ya gesi, real estate, madini pamoja na uanzishwaji wa mifuko mbalimbali itakayo ongeza tija kwa wanahisa wa NICOL.

Alisema mwaka 2021 wanahisa walithibitisha gawio la muda la Sh 17 ambalo lililipwa tarehe 30 Desemba 2021 na kwamba wanahisa waendelee kuwa na matumaini makubwa.

“Ni matarajio yetu kwamba kulingana na mafanikio makubwa tuliyo nayo wanahisa waendelee kutarajia mazuri kwenye mkutano wa wanahisa unaokuja tutakaoufanya, tarehe ya mkutano huo itatangazwa, “ alisema

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...