Adeladius Makwega-DODOMA
Katika simulizi yangu ya” Hili ni Jambo Gumu” nilieleza kuwa tulikuwa katika kikao cha awali kuelekea mahafali ya shule fulani, kikao hicho kilimalizika na wakati ukafika tukaingia katika mahafali ya kidato cha sita siku hiyo hiyo.
Ukiweka kando nyimbo, maigizo na matukio kadhaa yaliofanyika ukumbini hapo kulifanyika harambee ya ujenzi wa mabweni na madarasa mapya ya shule hii, huku kila mmoja aliyeshiriki hapo alichangia kwa tasilimu au ahadi. Harambee hii ilikuwa ya namna yake, hasa hasa kwa wazazi wa wahitimu ambapo mtoto alipotajwa jina tu baba na mama wa mtoto walisimama na kufika mbele na kutaja kiasi wanachochangia kwa ujenzi huo.
Mtoto wako anahitimu anapata daraja la kwanza kwa alama A zote, usipochangia kwa shule hiyo itakuwa si jambo jema, kwako mwenyewe na hata kwa Mungu wetu.
Wakati harambee inaendelea, jina la binti mmoja likatajwa, akatoka mbele akapokea zawadi kadhaa za taaluma, baba akasimama na akinamama wawili. Baba huyu hakuwa na papara, mikrofoni ikachukuliwa na mama mmoja akataja mchango, alafu akachukua mikrofoni mama mwingine, huku majina na familia yao yalikuwa ya kikristo.
“Mimi ndiyo mama mzazi wa huyu mtoto, huyu kando ni mama mlezi tu. Huyu mwanaume alikuwa mme wangu. Nashukuru sana mwanagu amefanya vizuri, nina hakika atapata A zote kama alivyofanya mtihani ywa majaribio(mock), mimi ni mama mzazi(alirudia), dada huyu alikuwa rafiki yangu, alinipokonya mume wangu tu, bado ni mume wangu hata kwa Mungu, bado nampenda.”
Ukumbini kukaibuka kelele, miluzi, kuzomea huku wengine wakipiga makofi kwa kuwa hayo yanayozungumzwa hayahusiani na harambee na wala mahafali hayo. Kelele zilipopungua huyu mama alitaja mchango wake mkubwa sana, huku umati ukimlipa kwa makofi ya pongezi kwaa ,kwaa , kwaa…Bado akiwa ameikamata mikrofoni kama mwanasiasa anayeomba kura na mwishoni akijitambulisha kuwa ni yeye Mbunge wa Viti Maalumu(CCM) katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati huo.
Mahafali yalimalizika salama huku tukio hilo likiwa gumzo, ikisemekana kuwa Mheshimiwa mbunge hakuwa anakaa na binti huyu, hata ukuwaji wote wa binti hadi kupevuka mama wa kambo ndiye aliyeshiriki kwa karibu na ndiyo maana mahafali hayo mama wa kambo hakuyakacha. Huku shubiri ikiingizwa na mama mzazi (mheshimiwa mbunge) hadharani. Huyu binti aliyehitimu kwa kuwa alikuwa ni mtu mazima aliyejitambua alionekana kumnong’oneza mama wa kambo wakati mama mzazi akiongea.
Mwanakwetu kwa nini siku ya leo ninakisimulia kisa hiki ?
Msomaji wangu tambua ulimwengu wa mchezo wa riadha utaukumbuka mno mwezi wa Julai 2022 ambapo mwanariadha wa kike wa Naijeria Oluwatobiloba Avomide maarufu kama Tobi Amusan aliyenyakua medali za dhahabu katika riadha ya kuruka viunzi ya umbali wa mita 100 katika mshindano yaliyomalizika nchini Marekani.
Amusan aliyezaliwa Aprili 27, 1997 alivunja rekodi ya mbio hizo za mita 100 katika nusu fainali kwa kukimbia mwendokasi wa sekunde 12.12 na kumalizia maajabu hayo katika fainali kwa kutumia sekunde 12.06, matokeo hayo ya kuvunja rekodi yake mwenyewe ndani ya siku moja lakini hayakutambuliwa kwa kuwa iliaminika kuwa upepo ulikuwa ukivuma kwa kasi ya ziada ya sekunde 2.5. Amusan ni Mnaijeria wa kwanza kuwa mwanariadha bingwa wa dunia kwa mita 100. Kabla ya mashindano hayo Amusan alikuwa na rekodi ya kutumia mwendokasi wa sekunde12.40 katika mashindano ya riadha ya Afrika.
Kumbukumu za mchezo huu uliowahi kuipa sifa kubwa hata Tanzania miaka za nyuma zinaonesha kuwa mwendokasi wa juu wa awali kwa mita 100 ulikuwa ni wa mwanariadha Karry Harrison wa Marekani katika mashindano ya mwaka 2016 akitumia sekunde 12.20. Waswahili wanasema macho hayana pazia, kwa hakika sote tumeshuhuhudia mwanariadha huyu wa Naijeria akishiriki mashindano hayo, akishinda medali hizo na hata wimbo wa taifa hili ukichezwa hadharni mbele ya ulimwengu na mashabiki wa riadha duniani
Tanzania tuliambulia patupu. Labda kifuta machozi ni michezo ya jumuiya ya madola ambapo Julai 30, 2022 Mtanzania Alphonce Simbu alinyakua medali ya Shaba katika mbio za marathoni. Lakini hiyo haiwezi kubadilisha rekodi yetu ya mashindano yaliyomaliza huko Marekani kwa kuambulia patupu.
Je mzigo wa lawama wa kufanya vibaya tunamtwika nani? Viongozi wa michezo nchini Tanzania? Vyama vya michezo vya Tanzania? Kila wanamichezo walioshiriki mashindano hayo?Au Watanzania sote?
Kwa mawazo yangu -kila mmoja anawajibu wa kubeba lawama hizo hili tuweze kufanya vizuri mashindano mengine. Atakayekwepa lawama hizo iwe kwa siri au wazi huyo si mwenzetu.
Kuna mtu alinimbia kuwa shida ya Tanzania ni moja, tulio wengi tunafanya mambo kwa kuwa tupo katika eneo hilo kwa wakati huo. Akatolea mfano wa waziri wa kilimo analima kwa kuwa sasa ni waziri wa kilimo, waziri wa mifugo atafuga kwa sasa kwa kuwa anasimamia mifugo. Waziri habari atasoma taarifa ya habari kwa kuwa sasa ni waziri wa habari. Kwa utaratibu waziri wa habari anapaswa kuisoma taarifa ya habari kabla ya kuwa na nafasi hiyo.
Akimaanisha tukiyafahamu mambo mapema, tutayasimamia na kufanya vizuri wakati tukiwa katika utekelezaji, UPO? Hilo ni kwa kila mmoja wetu. Hakuna kukwepa.
Ifahamike wazi kuwa kisa cha mahafali cha familia hiyo nilichokisimulia, wazazi walishiriki kwa pamoja mahafali ya binti yao kwa kuwa binti huyu mwenye akili sana shuleni alifanya vizuri, kwa hiyo kila mmoja alitamani kuwa sehemu ya mafanikio ya binti huyu. Kinyume chake kushindwa hakukuweza kuwakutanisha pamoja. Ndiyo kusema Watanzania tunatakiwa kwa pamoja tuwe sehemu ya kushindwa na kwa pamoja tena tuwe sehemu ya mafanikio.
Mafanikio yoyote yale huwa yanawakutanisha watu pamoja, wawe wanaelewana hata wale ambao hawaelewani. Kama mafanikio yakitukutanisha pamoja tunaweza kuzungumza, kuombana misamaha na likija jambo lingine litafanyika vizuri sana. Pata picha binti huyu mwenye akili , akifunga ndoa wazazi wote watatu watakutana tena katika mafanikio hayo.
Msomaji wangu hicho ndicho kinachoendelea sasa nchini Naijeria baada ya Tobi Amusan kuchukua medali hizo za dhahabu Wanaijeria wote kwa pamoja wanayashangilia mafanikio hayo.
0717649257
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...