MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango leo tarehe 30 Agosti 2022 amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Singapore nchini Tanzania Mhe. Douglas Foo, Mazungumzo yaliofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.
Katika Mazungumzo hayo, Makamu wa Rais amesema Tanzania ipo tayari kushirikiana na Singapore katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya Bandari, Afya, Viwanda, Elimu, Kilimo, Biashara, Uchumi wa Buluu pamoja na Tehama kupitia uwekezaji katika vifaa vya kielekroniki.
Amesema serikali ya awamu ya sita imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara hapa nchini ikiwa ni pamoja kushirikiana na mataifa katika masuala mbalimbali na kuhakikisha sera zilizopo ni thabiti na zisizobadilika badilika.
Makamu wa Rais amesema serikali imeweka mkazo katika kuboresha rasilimali watu ikiwemo kuhakikisha elimu ya msingi na sekondari inatolewa bila malipo, kujenga miundombinu ya elimu pamoja na msisitizo wa elimu ya sayansi husasani kwa wanafunzi wa kike. Pia amesema uwekezaji unafanyika katika sekta ya afya, upatikanaji wa maji safi na salama, ujenzi wa miundombinu ya barabara kuunganisha mikoa na vijiji, kuhakikisha upatikanaji wa nishati pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa.
Halikadhalika, Makamu wa Rais amewakaribisha wawekezaji kutoka nchini Singapore kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini ikiwemo katika miundombinu ya utalii, kuwekeza katika viwanda na teknolojia rafiki za kuongeza thamani ya mazao ya kilimo pamoja na madini. Aidha amesema kutokana na mafanikio yaliopatikana nchini Singapore katika sekta ya bandari, ipo haja ya kuongeza ushirikiano utakaowezesha mafunzo ya watendaji wa Bandari pamoja upatikanaji wa mitambo ya kisasa.
Kwa Upande wake Balozi wa Singapore nchini Tanzania Mheshimiwa Douglas Foo amesema Singapore inatarajia kuongeza ushirikiano na Tanzania katika maeneo mbalimbali hususani biashara na uwekezaji. Ameongeza kwamba kutokana na nchi hiyo kuwa eneo dogo kwaajili ya shughuli za kilimo hivyo ipo tija kubwa katika ushirikiano na Tanzania kwenye sekta hiyo itakayowezesha kuongezwa thamani ya mazao na kufikia soko la nchi hiyo na nchi zinginezo za bara la Asia.
Aidha ameikaribisha Tanzania kushirikiana na Singapore katika sekta ya utalii, Uvuvi na uchumi wa Buluu kwa ujumla. Amesema nchi hiyo sekta ya uzalishaji wa viwandani inachangia asilimia 20 katika pato la taifa hivyo ipo tayari kushirikiana na Tanzania kwa kuanzisha viwanda vya uzalishaji pamoja na kutoa elimu ya ufundi hapa nchini itakayoongeza tija katika viwanda hivyo.
Pia Amesema Singapore imeendelea na uwekezaji katika teknolojia unaorahisisha ufanyaji kazi pamoja na ufuatiliaji wa masuala mbalimbali ikiwemo masuala ya kiafya na kielimu. Ameongeza kwamba nchi hiyo imeweka mkazo katika utunzaji wa mazingira ikiwemo kuwaka faini kubwa kwa wachafuzi wa mazingira huku ikitarajia kuondoa kabisa uzalishaji wa hewa ukaa ifikapo mwaka 2050.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akifanya mazungumzo na Balozi wa Singapore nchini Tanzania Mhe. Douglas Foo, Mazungumzo yaliofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma leo Tarehe 30 Agosti 2022
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Singapore nchini Tanzania Mhe.Douglas Foo mara baada ya Mazungumzo yaliofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma leo Tarehe 30 Agosti 2022
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...