Na Mwandishi Wetu, Singida

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umewataka wadau wake wote kuulinda uhai wa Mfuko kwa wivu mkubwa kwa kutoa taarifa za udanganyifu unaofanywa na baadhi ya watoa huduma, wanachama na wananchi wengine wasio waaminifu.

Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF Juma Muhimbi wakati akifungua mkutano wa wadau wa Mfuko wa Mkoa wa Singida ambao una lengo la kujadili maboresho mbalimbali yanayofanywa na kupokea mrejesho wa huduma kutoka kwa wanachama wake.

“Ndugu zangu mtakubaliana na mimi kuwa tunauhitaji huu Mfuko ili utuhudumie lakini kumekuwepo na wimbi kubwa la udanganyifu, niwaombe sana kila mmoja awe mlinzi wa huduma zinazotolewa na Mfuko ili uzidi kuwa imara zaidi,” alisema Muhimbi.

Akizungumzia watoa huduma amewataka waendelee kutoa huduma bora kwa wanachama na kujiepusha na vitendo vya udanganyifu ili kuwezesha Mfuko kulipa madai halali lakini pia kuwa mabalozi wa kutoa taarifa sahihi na sio kuelekeza lawama kwa Mfuko pale inapoonekana huduma fulani haipo.

“Wanachama niwaombe sana kila mmoja ahakikishe kadi yake matibabu haitumiki na mtu mwingine kwani kwa kufanya hivyo ni sawa na kuhujumu Mfuko huu lakini pia kwa Waajiri wahakikishe wanawasilisha  michango ya Watumishi wao kwa wakati ili kuepukana na usumbufu kwa wafanyakazi na wategemezi wao kukosa huduma kutokana na kukosekana kwa michango,” alisisitiza Muhimbi.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko Bw. Bernard Konga, aliwahakikishia wanachama kuwa, uhai wa Mfuko uko imara na unaendelea kuwahudumia wanachama wake kwa huduma wanazozihitaji.

“Mfuko uko imara sana na kwa sasa tunajivunia sana uimarishaji wa huduma ambao umefanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Hassan Suluhu hususan kwa kuweka vifaa tiba vya kisasa katika hospitali mbalimbali nchini...

"Ambayo inarahisisha zaidi upatikanaji wa huduma kwa wanachama wetu hivyo kama Mfuko tunaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali na kuhakikisha tunawafikia wananchi wengi zaidi ili wajiunge na Mfuko,” alisema  Konga.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...