Mkurugenzi Mkuu wa Pesapal Tanzania, Bupe Mwakalundwa (kushoto), akipokea leseni iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa ajili ya kufanya biashara ya kutoa huduma kwa mifumo ya malipo ya kidijitali kutoka kwa Meneja Msimamizi wa Wateja wa kampuni hiyo, Ally Abdul. Hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam jana.
Na Mwandishi Wetu
Kampuni ya Pesapal Tanzania imepewa leseni na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kufanya biashara nchini kama mtoa huduma wa mifumo ya malipo ya kidijitali.
Pesapal ambayo ni taasisi ya teknolojia za huduma za kifedha (fintech) imesema jana kuwa imepewa idhini hiyo chini ya sheria ya Mifumo ya Malipo ya Taifa ya Mwaka 2015.
Tayari Pesapal inafanya biashara Kenya na Uganda ambako inazihudumia zaidi ya biashara ndogo na za kati 50,000. Dira yake ni kuziwezesha nchi za Kiafrika kutoa huduma za kifedha za kidijitali zenye bei nafuu, salama na zinazozingatia mahitaji ya soko husika kwa ajili ya kuchochea ukuaji uchumi endelevu.
Maafisa wake waandamizi wamesema hivyo ndivyo kampuni hiyo itakavyofanya Tanzania baada ya kupata leseni ya BoT ambapo kimsingi ni kutoa huduma ya malipo mtandaoni na kusaidia kufanyika malipo kwa ufanisi.
“Kuweza kupenya na kupanua shughuli zake nchini Tanzania ni hatua kubwa ya kimkakati yenye tija kwa Pesapal, ambayo ina matarajio ya kufanya vizuri sokoni na kuwawezesha Watanzania kupata thamani kutoka kwenye suluhisho za kifedha bunifu za kidijitali zilizosalama na zenye manufaa makubwa,” kampuni hiyo ilisema katika taarifa kwa vyombo vya habari.
Katikati ya mwaka jana, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) iliipa baraka kampuni hiyo kufanya biashara nchini ambazo ni muhimu kabla ya kukubaliwa kufanya hivyo na Benki Kuu.
Akizungumzia kupatikana kwa leseni hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Pesapal Tanzania, Bi Bupe Mwakalundwa, alisema kupatikana kwa leseni hiyo kutaiwezesha kampuni yao kupanua wigo wa upatikanaji wa bidhaa zao barani Afrika.
Kama ilivyo BoT, alifafanua, Pesapal ni muumini wa matumuzi ya teknolojia kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya huduma jumuishi za kifedha.
“Kwetu sisi Pesapal, lengo letu ni kuimarisha teknolojia ili kutengeneza suluhisho za malipo zinazorahisisha jinsi wateja na baishara mbalimbali wanavyolipwa,” alisema.
Bi Bupe aliongeza kuwa Pesapal inataka kuwapa Watanzania fursa ya kupata huduma bunifu za kifedha na kidijitali ambazo zinafaa kwa kada na biashara zote.
Wanufaika wengine wa uwekezaji huo watakuwa ni wafanyabiashara wa mtandaoni, watu binafsi, na wale wote ambao kwa sasa hawajafikiwa na mifumo rasmi ya kawaida ya malipo.
Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji Mkuu na Mwanzilishi wa Pesapal Group, Agosta Liko, kampuni hiyo imekuwa kinara wa fedha kidijitali katika ukanda huu wa Afrika Mashariki kwa kuchangia pakubwa uboresha wa huduma za malipo.
“Sisi kama kampuni ya kutoa huduma na iliyojikita zaidi kutumia teknolojia kwenye uendeshaji na uzalishaji wake tunazo zana hitajika kuleta mabadiliko katika upatikanaji wa huduma za fedha kidijitali,” Bw Liko alinukuriwa kwenye taarifa ya Pesapal Tanzania kwa vyombo vya habari.
Alisema hilo litawezekana kwa wao kuja na suluhisho zinazozingatia huduma bora kwa wateja, kusaidia watu kuboresha matumizi ya fedha na kuzisaidia biashara kutatua changamoto zote zinazohusiana na malipo.
Pesapal ilianzishwa mwaka 2009 lengo lake kuu likiwa ni kuchangia kusaidia kurahisisha kulipana na katika miaka 11 iliyopita imefanikiwa katika hilo kwa kiasi kikubwa kutokana na uwekezaji ambao imekuwa inafanya.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...