Na Mwandishi Wetu
BAADHI ya Wanachama wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wameeleza kuwa na mashaka kuhusu matumizi ya michango yao hususan kwa kipindi cha miezi 42 ya uongozi wa aliyekuwa katibu mkuu wao, Deus Gracewell Seif.
Kwa nyakati tofauti, wanachama hao wamesema hawana imani kama michango yao bado ipo salama kutokana na hali ya mambo ilivyokuwa ikiendeshwa ndani ya CWT chini ya Deus.
Mmoja wa wanachama hao ambaye hakutaka jina lake kutajwa mtandao, amesema kuwa mwaka jana Deus na Mweka Hazina wa Taifa wa Chama hicho, Abubakari Alawi walishikiliwa na TAKUKURU na kushtakiwa kwa kosa la uhujumu uchumi na matumizi mabaya ya ofisi.
Mwanachama huyo amesema kesi hiyo ya jinai namba 39/2021 iliyofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, moja ya tuhuma zilizowakabili ni kutumia fedha za chama hicho zaidi ya Sh. Milioni 13 kama gharama za usafiri, malazi na gharama za kujikimu kwenda kuangalia mechi ya mpira wa miguu kati ya Timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ na Cape Verde iliyofanyika nchini Cape Verde.
"Ukiangalia katika kipindi cha miezi 42 ambayo mtendaji mkuu alikuwa madarakani na Mweka Hazina, walimu tumechangia zaidi ya Sh. bilioni 30 ambazo zilitokana na kukatwa asilimia mbili kwenye mshahara wa kila mwalimu, hatujui hizi fedha kama zipo au lah hasa tunapoona viongozi ambao walihukumiwa kifungo cha miezi sita ndani kuwa nje wakitumikia kifungo cha nje,” alisema Mwalimu huyo.
Mwanachama huyo amesema Mahakama katika hukumu yake Juni 28, mwaka huu (Nakala ya hukumu tunayo), iliagiza watuhumiwa hao mbali na kutumikia kifungo cha miezi sita jela pia walitakiwa kurejesha fedha hizo.
“Sasa wapo nje inasemekana wanatumikia kifungo cha nje, binafsi sina utaalamu wa sheria lakini hii haijakaa sawa, vipi fedha walizotakiwa kurejesha? Lakini katika michango ambayo tunachanga kila mwezi asilimia 30 inaingia kwenye uwekezaji wa Chama, lakini tangu kuingia madarakani aliyekuwa katibu wetu ambae alikaa kwa miezi 42 hakuna uwekezaji wa wazi ulioonekana, je fedha za michango yetu zipo?,” alihoji.
Mwanachama mwingine ambaye ni mwalimu kutoka mkoani Mbeya, alidai kuwa wanachama walipaswa kutengenezewa fulana,walimu wa nchi nzima lakini haikufanyia hivyo kipindi cha Mei Mosi ya mwaka huu .
“Baadae wakatuambia kwa kuwa chama kinajipanga kujenga makao makuu yake jijini Dodomaa, fulana zitanunuliwa kwa walimu waliopo jijini Dodoma pekee, hata hivyo baada ya hapo hatujaona ujenzi wa makao makuu ya Chama, haya yote tunahitaji ufafanuzi kwa sababu ni michango yetu inayotumika,” amesema.
Akitoa mtazamo wake, mwalimu mwingine kutoka Lushoto mkoani Tanga, ambaye pia hakutaka jina lake litajwe, amesema kila mwanachama wa chama wa CWT anakatwa asilimia mbili ya mshahara wake kama ada ya uanachama na walimu wasio wanachama wanakatwa asilimia mbili ya mishahara yao kama ada ya uwakala kwa mujibu wa sheria ya ajira na mahusiano kazini na michango hiyo inaingia katika mfuko wa Chama chao kila mwezi.
Amesema kwa mwezi chama chao kinaingiza zaidi ya Sh. Bilioni 4.5 na kwa utaratibu wa CWT, asilimia 30 ya mapato ya kila mwezi ni kwa ajili ya uwekezaji unaohusisha ujenzi wa majengo mapya na kuyakarabati mengine yaliyopo.
“Tunataka kujua tangu Katibu Mkuu (Mwalimu Deus) kuingia madarakani na kumkuta mweka hazina wake mwaka 2019 mpaka 2022 ni miezi 42 ambapo kwa hesabu ya kawaida zinakusanywa sh milioni 720 kila mwezi, ukiangalia kwa miezi 42 ni zaidi ya Sh. Bilioni 30, walimu wanataka kujua ziko wapi?.
Alipoulizwa kuhusu malalamiko ya walimu hao, Ofisa habari wa CWT, Bathlomeo Chilwa alisema ameyasikia malalamiko hayo na kumtaka mwandishi wa habari hizi kuwasiliana na Kaimu Rais wa chama hicho Mwalimu Dinah Mathamani.
Kwa upande wake Mathalani, amesema walimu wanapaswa kusubiri mkutano mkuu kuweza kupata taarifa sahihi za mapato na matumizi.
Aidha, amesema michango yote ya CWT inatumika kulingana na utaratibu wa katiba ya chama hicho na maelezo yanatolewa kwenye mikutano ya chama hicho kuanzia ngazi ya chini hadi juu.
Mathamani amesema kuelekea mikutano hiyo, tayari wanatarajia kutumia Sh. bilioni 2.5 awamu ya kwanza kwenda katika wilaya kwa ajili ya mikutano hiyo, pia awamu ya pili wataziingizia wilaya Sh bilioni 1.2 kufanikisha hatua hiyo.
“Kuhusu ujenzi wa Makao Makuu ya chama ni kweli mpango huo upo, awali Baraza kuu la chama lilipitisha kuchukuliwa mkopo wa Sh. Bilioni tano ambapo katika fedha hizo, Sh.bilioni mbili zilipangwa kutumika kwenye hatua ya awali ya ujenzi wa makao makuu ya Chama Dodoma, bahati mbaya mkopo huo hakuchukuliwa.
"Taratibu hazikuwa zimekamilika kwa sababu aliyekuwa akifuatilia ni mtendaji mkuu wa chama ambaye ni Katibu Mkuu, kama tunavyofahamu Katibu Mkuu (Mwalimu Deus) alipata matatizo na kufungwa hivyo mchakato ule ukawa umesimamia pale, hiyo ndio sababu ya kuchelewa kuanza mradi ule wa ujenzi wa Makao Makuu ya chama Dodoma,” amesema Mathalani.
Amesema fedha nyingine walizokuwa nazo wamezitumia katika maandalizi ya mikutano ya wilaya nchi nzima.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...