* Ni zoezi la 'Temeke Afya Check' lililolenga kusogeza huduma za kibingwa kwa wananchi
MENEJIMENTI
ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke kwa kushirikiana na ofisi ya
Mkurugenzi wa Manispaa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke wameandaa timu ya
madaktari bingwa itakayoendesha zoezi la upimaji wa afya na matibabu
bila malipo kwa wananchi wa Temeke kwa lengo la kuwasogezea wananchi
huduma za kibingwa kadri inavyowezekana.
Akizungumza
na Michuzi TV leo jijini Dar es Salaam Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya
Rufaa ya Mkoa wa Temeke Dr. Joseph Kimaro amesema, zoezi hilo kubwa la
'Temeke Afya Check' litafanyika katika hospitali hiyo kuanzia tarehe 9
hadi 11 Septemba mwaka huu na huduma za upimaji wa afya bila malipo kwa
wananchi wote wa Temeke zitatolewa kwa kushirikiana madaktari bingwa
kutoka ndani na nje ya hospitali ya Temeke.
''Hii
ni fursa nzuri kwa wananchi wa Temeke kupata huduma za kibingwa na
tunafanya zoezi hili kwa lengo la kuhakikisha huduma za kibingwa
zinawafikia wananchi wengi kwa kadri inavyowezekana....Tunafahamu wapo
wananchi wengi wenye matatizo mbalimbali na wanahitaji kuonana na
madaktari bingwa hivyo tukaona tushirikiane na wadau mbalimbali na
kutoa huduma hii bila malipo kwa wananchi wetu ili waweze kunufaika na
jitihada za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu
Hassan katika kuboresha huduma za afya.'' Amesema. Dr. Kimaro.
Pia
amesema gharama za matibabu hayo yatakayotolewa bure kwa wananchi
yatagharamiwa na hospitali pamoja na wadau mbalimbali zikiweo kampuni za dawa
(Pharmacy) ambao watatoa dawa, vitendanishi na wataalam pamoja na kulipa
gharama za matibabu kwa wagonjwa watakaotakiwa kufanyiwa upasuaji na
ushirikiano huo na wadau umelenga kusogeza huduma za kibingwa karibu na
wananchi pamoja na kuunga mkono jitihada za Serikali ya kuhakikisha
wananchi wanakuwa na afya bora ya kuzalisha na kuchangia ukuaji wa
uchumi wa Taifa.
Dr.
Kimaro amesema, zoezi hilo limefadhiliwa kwa ukaribu na wadau
mbalimbali wakiwemo MDH, Haidery Plaza, Shamshu pharma, MFAA, Nebula,
CCBRT, TAI, Consolation Medicare pamoja na Tindwa medical Health ambao
watatoa madaktari bingwa wa kutoa huduma katika zoezi hilo, pamoja na
wadau wengine wakiwemo NMB, CRDB, Serengeti na NBC ambao pia wameshiriki
katika kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya zoezi hilo la 'Temeke
Afya Check' na Daktari bingwa wa Kinywa na Meno Dr. Twisibilega
Mwakasungule amesema huduma zitakazotolewa bure malipo kuanzia tarehe 9
had 11 Setemba mwaka huu ni pamoja na magonjwa ya wanawake na uzazi,
magonjwa ya watoto, magonjwa ya pua, koo na masikio, magonjwa ya mifupa
na majeraha ya ajali, magonjwa ya njia ya mkojo na tezi dume, magonjwa
ya sukari, figo, shinikizo la damu, magonjwa ya macho na uoni hafifu,
magonjwa ya kinywa na meno, upasuaji mkubwa na mdogo pamoja na magonjwa
ya akili.
Dr.
Twisibilega amesema madaktari bingwa wa magonjwa hayo watakuwepo
hospitalini hapo na watatoa huduma na ushauri wa kitaalam na kuwataka wananchi kujitokeza kupata huduma hizo
walizosogeza karibu yao bila malipo, na wanategemea kuwahudumia wagonjwa
wapatao 5000 ambao wataonana na madaktari bingwa na kupatiwa huduma.
Pia
Daktari bingwa wa magonjwa ya macho na mratibu wa huduma za Tiba katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke Dr. Husna Msangi amesema huduma
hizo zitatolewa kuanzia saa mbili na nusu asubuhi hadi saa tisa na nusu
jioni na wateja wenye bima za afya watapokelewa na kupatiwa matibabu na
kueleza kuwa katika katika zoezi hilo watapokea wananchi wanaotumia kadi za bima za afya ikiwemo NHIF.
Awali Daktari bingwa wa upasuaji na
mratibu wa zoezi hilo Dr. Kelvin Rogathe amesema idara kwa
kushiirikiana na wadau wamejipanga kufanya uchunguzi na kutoa matibabu
kwa wananchi hasa katika magonjwa ya mdomo sungura kwa watoto, vichwa
kujaa maji, majeraha yaliyotokana na moto na henia na wote watachunguzwa
na kupatiwa huduma.
Daktari
bingwa wa mifupa kutoka hospitali hiyo Dr. Kiandiko Liseki amesema
wamejipanga kufanya uchunguzi na kutoa matibabu bure kwa wagonjwa wenye
matatizo ya mifupa ikiwemo miguu kufa ganzi, majeraha ya kuvunjika, majeraha
yaliyotokana na ajali ambapo watafanya uchunguzi, kutibu na kuunga mifupa kwa wagonjwa ambao mifupa yao iliunga vibaya na kupelekea
kutembea kusiko sahihi kwa kuwafanyia upasuaji.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke
Dr. Joseph Kimaro akizungumza na Michuzi TV na kueleza kuwa, zoezi hilo kubwa la 'Temeke Afya Check'
litafanyika katika hospitali hiyo kuanzia tarehe 9 hadi 11 Septemba
mwaka huu na huduma za upimaji wa afya bila malipo kwa wananchi wote wa
Temeke zitatolewa kwa kushirikiana madaktari bingwa kutoka ndani na nje
ya hospitali ya Temeke.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke
Dr. Joseph Kimaro (kulia,) akiteta jambo na Daktari bingwa wa upasuaji na mratibu wa zoezi hilo Dr. Kelvin Rogathe (kulia,) wakati walipozungumzaa na waandishi wa habari kuhusiana na zoezi hilo kubwa la 'Temeke Afya Check'
litakalofanyika katika hospitali hiyo kuanzia tarehe 9 hadi 11 Septemba
mwaka huu na huduma za upimaji wa afya bila malipo kwa wananchi wote wa
Temeke zitatolewa kwa kushirikiana madaktari bingwa kutoka ndani na nje
ya hospitali ya Temeke.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...