Said Mwishehe, Michuzi TV

JESHI la Polisi nchini limeendesha oparesheni maalumu na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa sugu 167 maarufu kwa jina la ‘Panya road’ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya uhalifu vya kuvunja nyumba na kupora mali wakiwa na silaha za jadi katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.

Akizungumza leo Septemba 24,2022 , Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Afande Awadhi Haji amesema hivi karibuni katika kipindi cha Septemba 2022, jijini Dar es Salaam kumeibuka wimbi la vitendo vya kiuhalifu vya unyang’anyi wa kutumia silaha za jadi( mapanga, nondo, na visu).

“Vitendo hivyo vinafanywa na kundi la wahalifu wanaokadiriwa kuwa na umri wa miaka 14 hadi 30 na ambao wanakuwa kwenye makundi kati ya watu 10 had 30 ambao wanavunja nyumba usiku kuanzia saa saba na saa 10 .Wanapora mali baada ya kujeruhi watu mbalimbali.

“Kutokana na vitendo hivyo Jeshi la Polisi tumefanya operesheni na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao 167.Watu hao wamegawanyika kwenye makundi ambapo kuna kundi la watuhumiwa wanaoshiriki moja kwa moja kuvunja kwa kufanya uporaji na kundi jingine linapokea na kununua mali hizo za wizi,”amesema.

Ameongeza kwenye operesheni hiyo wamefanikiwa kukamata mali zilizoibiwa katika maeneo mbalimbali Dar es Salaam , mali hizo ni televisheni flat screen 23, redio sub-woofer mbili, compyuta za mezani mbili pamoja na spika mbili za sub-woofer.

Aidha amesema miongoni mwa watuhumiwa waliokamatwa wamekutwa wakiwa na mapanga 19 , vifaa vya kuvunjia , mikasi minne, nondo saba na jeki mbili . Pia Polisi wamefanikiwa kukamata magari matatu aina ya Toyota Carina namba T 314 BVY,Toyota Noah namba T 218 BYS,Toyota Noah namba T 260 BEP.

Pia wamekamata pikipiki tano ambazo ni aina ya Boxer MC 913 DEH, Boxer MC 405 CVM, MC 856 DFY, MC 206 DDK na pikipiki moja isiyokuwa na namba walizokuwa wakizitumia wahalifu kubeba zana za kufanyia uhalifu pamoja na kusafirisha mali za wizi baada ya uporaji.

“Watuhumiwa hao wamekamatwa na dawa za kulevya aina ya heroine gramu 35, bangi kilo 63.6, mirungi yenye uzito wa kilo 09.3.Operesheni hii ni endelevu na inafanyika nchi nzima ili kukabiliana na vitendo vya kiuhalifu vikiwemo vilivyokuwa vikitendeka hapa Dar es Salaam ambavyo kwa sasa vimedhibitiwa kwa kiwango kikubwa.

“Hali ya Jiji la Dar es Salaam ni shwari , wananchi wanaendelea na shughuli zao kama kawaida bila hofu yoyote .Upelelezi watuhumiwa hao unakamilishwa hara ili wafikishwe mahakamani haraka na sheria ichukue mkondo wake, jeshi la polisi linaendelea kutoa tahadhari na onyo kali kwa watu wote wanaojihusisha na vitendo vya kiuhalifu kwa namna moja au nyingine waache mara moja,”amesema.


Pia Jeshi la Polisi halitasita kuwachukulia hatua za kisheria wazazi au walezi wanaowaficha na kuwakumbatia watoto wao wanaojihusisha na matukio ya kiuhalifu ya unyang’anyi, wizi na uporaji huku akitoa mwito kwa wananchi na wadau kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa sahihi za uhalifu na wahalifu ili hatua stahili zichukuliwe kabla ya vitendo vya uhalifu kufanyika .

“Jeshi la Polisi linawahimiza wananchi kuanzisha na kuimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi ili kuimarisha ulinzi kwenye maeneo yao ,pia linawashukuru raia wema walioshiriki kutoa taarifa zilizofanikisha kupatikana kwa watuhumiwa na mali mbalimbali za wizi zilizokamatwa.

“Tunatoa mwito kwa wananchi waliobiwa mali zao kujitokeza kwenye vituo vya Polisi kuzitambua mali hizo kwenye vituo vya Buguruni, Stakishari, Mbagala, Kawe na Kimara.







 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...