Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Kigoma
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Tanzania Bara Abdulrahman Kinana ameelezwa kuwa Kampuni ya Huduma za Meli katika tawi la Kigoma kwa sasa inatekeleza mradi wa ukarabati wa meli ya kusafirisha shehena ya mafuta ya petrol , dizeli na mafuta ya taa.
Aidha Kampuni hiyo imesema mradi wa ukarabati wa meli kongwe ya MV.Liemba bado haujaanza rasmi na sasa wako hatua ya kutangaza zabuni kwa ajili ya kupata mkandarasi na katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 Serikali imetenga jumla ya Sh.bilioni 8.1 kwa ajili ya ukatabati huo.
Kinana ameelezwa hayo leo Septemba 1,2022 alipotembelea mradi wa ukatabati wa MT.Sangara na MV.Liemba zilizopo Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma.
Kaimu Meneja Tawi la Kigoma Allen Butembero amesema kuhusu mradi wa ukarabati wa meli ya kusafirisha shehena ya mafuta mkataba ulisainiwa Mei 26,2021 na gharama ya mradi ni Sh.bilioni 8.4 wakati tarehe ya kuanza mradi ni Novemba 8, 2021.
“Mradi ulipofikia mpaka sasa ni asilimia 66.47 .Fedha ambazo zimeshalipwa na Serikali ni Sh.bilioni 1.2 ambazo ni sawa na asilimia 15 ya fedha zote zonazotakiwa kulipwa katika mradi huu.Mradi utachukua miezi 12 mpaka kukamilika kwake, hivyo tunategemea mkandarasi kukabidhi mradi huu mwisho wa Novemba 2022,”amesema.
Akielezea miradi mingine inayotarajiwa kutekelezwa na Serikali kwenye Mkoa wa Kigoma kwa upande wa Kampuni ya huduma za meli ni ujenzi wa meli mpya ya mizigo itakayokuwa na uwezo wa kubeba tani 3000 na kiasi cha Sh.bilioni 12 zimetengwa kwa ajili ya mradi huo.
Aidha amesema ujenzi wa mradi mpya ya abiria na mizigo itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 400 za mizigo ambapo serikali imetenga Sh.bilioni 12.Pia ujenzi wa chelezo itakayotumika kujenga meli hizo mbili ambapo jumla ya fedha Sh.bilioni 12 zimetengwa.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa ya mradi wa ukarabati wa meli hizo , Kinana ameishauri Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) kujiendesha na kuanza kufikiri kibiashara ikiwemo kuomba dhamana za serikali Ili kukopa fedha na kununua meli mpya ili kukidhi mahitaji ya huduma za usafiri na usafirishaji katika ziwa Tanganyika.
“Sikilizeni ndugu zangu msisubiri fedha kutoka bajeti ya serikali, ombeni dhamana ya serikali mkakope mnunue meli mpya.. pesa za namna hiyo ziko nyingi duniani.” Amesema Kinana.
Akizungumzia meli ya MV.Liemba ambayo nayo ipo kwenye mpango wa kukarabatiwa kwa kiwango kikubwa na Serikali katika mwaka huu wa fedha 2022/2023 amesema meli hiyo ina umri wa zaidi ya miaka 100 na imeingia kwenye orodha ya urithi wa dunia chini ya UNESCO.
Pamoja na hayo Kinana ametumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi wa Mkoa Kigoma kuuwa wamoja kwani kufanikiwa kwao kutokana na mshikamano ambao ndio msingi wa maendeleo.
.jpeg)
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana, akiwa ndani ya Meli kongwe ya Mv Liemba ambayo inafanyiwa ukarabati mkubwa. Kulia kwake ni Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...