Balozi wa Marekani nchini Donald J. Wright na Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Exaud Kigahe, wamezindua rasmi ziara ya makampuni ya Kimarekani kutembelea Tanzania Bara na Zanzibar kujionea fursa za kibiashara na uwekezaji (Business Fact-Finding Mission). Makampuni 20 ya Kimarekani yalijisajili kushiriki katika ziara hii inayolenga kuangazia biashara za kilimo, nishati, huduma za afya na viwanda vya teknolojia ya habari na mawasiliano.

Katika hafla ya uzinduzi wa ziara hiyo, Balozi Wright aliyapongeza makampuni hayo kwa uamuzi wao wa kuiangalia Tanzania kama mahali wanapoweza kuwekeza katika sekta muhimu za uchumi na kupanua biashara zao.  “Tunakaribisha ushiriki zaidi wa Wamarekani katika uchumi wa Tanzania – kwa hakika, hili ni mojawapo ya malengo ya msingi kabisa ya ubalozi wetu.  Makampuni ya Kimarekani huja na ubunifu, ujuzi na mtaji lakini pia nia ya kuwafundisha Watanzania jinsi ya kusimamia na kuendesha biashara zao. Nafasi za ajira wanazozizalisha nchini Tanzania sio zile za kada za chini tu, bali pia zile zinazohitaji stadi za juu za kiteknolojia na kiutawala,” alisema Balozi Wright.


Naye Naibu Waziri Kigahe alisema; “Marekani na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimekuwa na uhusiano mzuri wa kirafiki tangu mwaka 1961, uhusiano uliojengeka katika kuheshimiana, maadili na matazamio ya pamoja ya kuwa na mustakabali wenye amani na ustawi zaidi. Marekani ni ya tatu miongoni mwa wawekezaji wakubwa zaidi wa kigeni nchini Tanzania na imekuwa ikitoa msaada wa maendeleo na msaada mwingine katika kujenga uwezo wa kushughulikia masuala ya afya na elimu, kuchochea ukuaji mpana wa uchumi na kuimarisha usalama wa kikanda na wa humu nchini ili kudumisha maendeleo.”


Siku ya kwanza ya ziara hii itahusisha kupata maelezo kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania, Chama cha Wafanyabiashara na Makampuni ya Kimarekani nchini Tanzania na Umoja wa Watendaji Wakuu wa Taasisi nchini Tanzania (CEO Roundtable of Tanzania). Aidha, washiriki watakuwa na majadiliano na wawakilishi wa serikali ya Tanzania. Ziara hii imeandaliwa na Vyama vya Wafanyabiashara na Makampuni ya Kimarekani (“AmCham”) katika nchi za Kenya, Tanzania and Afrika ya Kusini.


Kesho, 28 Septemba, ujumbe wa wafanyabiashara hawa utaelekea Zanzibar ambako utapokea maelezo kutoka kwa wawakilishi wa serikali na kufanya majadiliano na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar na kuhudhuria mkutano utakaohutubiwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Othman Masoud Othman.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...